Utoaji ripoti polisi kuhusu unyanyasaji wa mtandaoni dhidi ya wanawake wanahabari umeongezeka mara mbili tangu mwaka 2020, huku mwanamke 1 kati ya 4 akikabiliwa na hofu au msongo wa mawazo unaohusiana na unyanyasaji huyo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake, UN-Women kuelekea siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani Mei 3 mwaka huu.

Kupitia uchambuzi wake na wadau, uliotolewa leo jijini New York, Marekani, UN Women inasema kutokana na unyanyasaji huo, wanawake wanahabari wanalazimika kujidhibiti wao wenyewe kwenye mitandao ya kijamii, huku asilimia 22 katika kazi zao.

UN Women na washirika kadhaa ikiwemo mtandao wa TheNerve wametoa ripoti hiyo iliyohusisha utafiti wa mwka 2025 katika nchi 119, ikiangazia ongezeko na mbinu zinazozidi kuwa za kisasa za unyanyasaji wa mtandaoni unaowakumba wanawake katika maisha ya umma – hasa wanawake wanahabari na wataalamu wa vyombo vya habari.

Aina za unyanyasaji wa mtandaoni zinazoibuka, ‘Deepfakes’

Kwa mujibu wa uchambuzi huo uitwao Kipindi Muhimu: Unyanyasaji mtandaoni – Athari, Namna Unavyojitokeza na Njia za Kupata Haki katika Zama za Akili Mnemba (AI),  asilimia 12 ya wanawake watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati, wanahabari, wafanyakazi wa vyombo vya habari na mawasiliano ya umma wanasema wamewahi kukumbana na kusambazwa kwa picha zao binafsi bila ridhaa, ikiwemo picha za faragha au za kingono. Asilimia 6 wanasema wamekuwa waathiriwa wa “deepfakes,” au picha zilizohaririwa na kupachikwa sauti au sura za wahusika, huku takribani 1 kati ya 3 akipokea maombi ya kingono yasiyotakiwa kupitia ujumbe wa kidijitali.

Mkakati wa kuwanyamazisha wanawake

Ripoti inaonesha kuwa unyanyasaji huu mara nyingi hufanywa kwa makusudi na kwa uratibu, ukiwa na lengo la kuwanyamazisha wanawake watumishi wa umma huku ukidhoofisha uaminifu wao wa kitaaluma na sifa zao binafsi.

Mkakati huu tayari una madhara: asilimia 41 ya wanawake wote waliojibu walisema wanajidhibiti kwenye mitandao ya kijamii ili kuepuka unyanyasaji, huku asilimia 19 wakiripoti kujidhibiti katika kazi zao kutokana na unyanyasaji wa mtandaoni.

Hali mbaya zaidi kwa wanawake wanahabari

Kwa wanawake wanahabari na wafanyakazi wa vyombo vya habari, hali ni ya kutia wasiwasi zaidi ambapo asilimia 45 ya kundi hili waliripoti kujidhibiti kwenye mitandao ya kijamii mwaka 2025 (ongezeko la asilimia 50 tangu mwaka 2020), na karibu asilimia 22 waliripoti kujidhibiti katika kazi zao.

Kuongezeka kwa hatua za kisheria

Mwelekeo mwingine unaonesha ongezeko la hatua za kisheria kwani hivi sasa wanawake wanahabari na wafanyakazi wa vyombo vya habari wanaripoti visa hivyo kwenye vyombo vya sheria.

Mathalani mwaka 2025, watendaji hao walikuwa na uwezekano mara mbili zaidi (asilimia 22) wa kuripoti matukio ya unyanyasaji wa mtandaoni kwa polisi ikilinganishwa na asilimia 11 mwaka 2020.

Takribani asilimia 14 sasa wanachukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika, wanaowezesha unyanyasaji huo au waajiri wao, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 8 mwaka 2020.

Athari mbaya kwa afya na ustawi

Uchambuzi huo unasema kuwa unyanyasaji huu una athari mbayá kwa afya na ustawi wa wanawake.

Ripoti inaonesha kuwa karibu robo (asilimia 24.7) ya wanawake wanahabari na wafanyakazi wa vyombo vya habari walioulizwa wamegundulika kuwa na wasiwasi au msongo wa mawazo unaohusiana na unyanyasaji wa mtandaoni walioupata, na karibu asilimia 13 waliripoti kugundulika kuwa na ugonjwa wa mfadhaiko baada ya tukio (PTSD).

Onyo kuhusu athari mbayá za teknolojia ya AI

“AI inafanya unyanyasaji kuwa rahisi zaidi na wenye madhara makubwa, na hii inachochea kudhoofika kwa haki zilizopatikana kwa juhudi kubwa katika mazingira yanayoonesha kurudi nyuma kwa demokrasia na chuki dhidi ya wanawake mtandaoni. Wajibu wetu ni kuhakikisha mifumo, sheria na majukwaa yanachukua hatua kwa haraka kulingana na uzito wa mgogoro huu,” amesema Kalliopi Mingerou kutoka UN Women.

Mapengo katika ulinzi wa kisheria

Bado kuna pengo kubwa katika ulinzi wa kisheria dhidi ya unyanyasaji wa mtandaoni. Kama Benki ya Dunia ilivyobainisha mwaka jana, chini ya asilimia 40 ya nchi zina sheria za kulinda wanawake dhidi ya unyanyasaji wa mtandaoni au ufuatiliaji wa mtandaoni (Cyberstalking).

Matokeo yake, asilimia 44 ya wanawake na wasichana duniani – takriban watu bilioni 1.8 – bado hawana upatikanaji wa ulinzi wa kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *