
Kupitia wavuti wake, MONUSCO imesema kikosi chake cha kujibu mashambulizi au (FIB) ndio kimefadhili mradi huo wenye gharama ya dola takribani 40,000, ukijumuisha kisima kimoja na mikondo sita yenye mabomba ya maji.
MONUSCO inasema kwa miaka kadhaa, upatikanaji wa maji kwenye vitongoji hivyo ulikuwa changamoto kubwa na hivyo “kukamilika kwa mradi huu kumeleta ahueni kubwa kwa kaya ambazo awali wanafamilia walilazimika kutembea umbali mrefu kusaka maji safi.”
“Maji haya ni masafi mno, hayana vijidudu. Tulikuwa tunateka maji bondeni, lakini leo hii tunakunywa maji kutoka hapa kijijini. Tunatarajia kupata idadi kubwa ya watu hapa. Ni furaha kubwa leo,” amenukuliwa Astride Kahambu Vagheni, mwanamke mkazi wa eneo hilo huku tabasamu ikiwa dhahiri kwenye uso wake.
Mradi huu utalinda wanawake
Pamoja na kuboresha mazingira, mradi huu pia unalenga kulinda raia. Katika eneo hilo ambalo limegubikwa na ukosefu wa usalama, safari ndefu za kusaka maji mara nyingi hutumbukiza wanawake na wasichana kwenye mashambulizi kutoka makundi yaliyojihami.
Flavien Nzanzu Muhindo, ambaye ni Chifu wa eneo hilo amesema, “Haya maji ni muhimu sana kwa sababu yanapunguza hatari. Ukatili wa kijinsia ni miongoni mwa hatari tunazopambana nazo hivi sasa. Wanawake mara nyingi wanalazimika kusindikizwa na wanaume pindi wanapokwenda kuteka maji umbali mrefu. Tuna zaidi ya wakazi 4,000 ambao watanufaika na mradi huu.”
Miezi minne ilitumika kukamilisha mradi huu ambao unanufaisha watu ambao wengi wao wamefurushwa makwao kutokana na mapigano mashariki mwa DRC.