NI siku nyingine tena ya Simba kuikimbia zaidi Azam na kuendelea kuifukuzia Yanga katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Baada ya Ijumaa Azam kuchapwa 4-1 na TRA United, matokeo ambayo yameifanya timu hiyo kuwa nyuma kwa pointi tatu dhidi ya Simba, yametoa mwanya kwa Wekundu wa Msimbazi kuongeza tofauti na kufikia pointi sita itakaposhuka dimbani Jumapili hii ambapo kuna mecho tatu.

Mechi hizo tatu za Ligi Kuu Bara zinazochezwa Jumapili hii jijini Dar es Salaam na Mwanza, ndani yake kuna vita mbili, ya kuwania ubingwa, pia kupambana kuepuka kushuka daraja.

SIMBA VS TZ PRISONS

Mechi hii itakayochezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar, Simba itakuwa mwenyeji ikiikaribisha Tanzania Prisons ambayo ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikipambana kukimbia presha ya hatari ya kushuka daraja wakati Wekundu hao wakiutaka ubingwa wakikamata nafasi ya pili.

Ikitoka kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya JKT Tanzania, Simba imelazimika kuhama uwanja na sasa itaanza maisha mapya kwenye Uwanja wa KMC Complex ambao msimu huu ulikuwa unatumiwa na mtani wake Yanga na wenye uwanja huo KMC FC, pia Simba iliutumia kabla ya kuhamia Meja Jenerali Isamuhyo.

Simba iliyopo nafasi ya pili kwa pointi 46, inautaka ubingwa wa ligi ikiwa na hesabu za kuendelea kuifukuzia Yanga ambayo ndio bingwa mtetezi na kinara wa msimamo.

Kabla ya Yanga kucheza na Coastal Union, tofauti yao na Simba ilikuwa pointi tano, hivyo Wekundu wa Msimbazi wanataka kuendelea kutoa presha kuagalia wapi mpinzani wake ataangusha pointi lakini yenyewe ikiendelea kushinda mechi zake.

Historia inaonyesha timu hizo zimekutana mara 19 kwenye ligi lakini Simba ndio timu iliyofanya vizuri ikishinda jumla ya mechi 12 wakati wanajeshi hao wa Magereza wakishinda nne zikitoa sare michezo mitatu.

Simba ndani ya mechi tano za mwisho imeshinda tatu  ikizifunga JKT Tanzania, Namungo na Fountain Gate lakini ikatoa sare mbili dhidi ya Yanga na TRA United, wakati Prisons yenyewe ikiwa na mwendo mbovu kwenye mechi tano za mwisho ikipoteza nne dhidi ya Mbeya City, TRA United, Yanga na Singida Black Stars huku ikiambulia pointi kwenye mechi moja pekee ya sare dhidi ya KMC.

Mara ya mwisho Prisons kupata ushindi ilikuwa Februari 14, 2026 iliposhinda nyumbani kwa mabao 3-2 dhidi ya Namungo lakini bahati mbaya kwao ni kwamba tangu kocha mpya wa kikosi hicho Shadrack Nsajigwa apewe timu hiyo hajafanikiwa kushinda mechi yoyote.

Kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola akizungumzia mchezo huo alisema wanatarajia dakika 90 ngumu za ushindani dhidi ya Prisons yenye pointi 14, ugumu ambao hautatokana na nafasi ya mgeni wao kwenye mechi hiyo bali utatokana na historia ya timu hizo zinapokutana.

“Siku zote hakuna mechi rahisi kati yetu Simba na Prisons, mechi hii itakuwa ngumu, tumejipanga kukabiliana na ugumu huo, tumejiandaa vizuri kutafuta ushindi ili kuendelea kuutafuta ubingwa msimu huu,” alisema Matola.

Simba itawakosa wachezaji wawili, nahodha Shomari Kapombe ambaye ameumia lakini pia licha ya winga Anicet Oura kuanza mazoezi lakini bado hakuna uwezekano mkubwa wa kurudi katika mechi hii.

Prisons hata kama itashinda mechi hiyo bado itaendelea kusalia nafasi ya 15 kutokana na tofauti kubwa ya pointi kati yake na mahasimu wao Mbeya City yenye pointi 21 kwenye nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi.

Kocha wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa akizungumzia mchezo huo licha ya kukiri kuwa kikosi chake kipo kwenye hali mbaya, lakini akasema bado hawakati tamaa na wamejiandaa kutafuta pointi dhidi ya Simba.

“Nikweli hatupo kwenye nafasi nzuri lakini hatuna nafasi ya kukata tamaa, lolote linaweza kutokea, haitakuwa mechi rahisi kwetu dhidi ya Simba lakini tumejiandaa kukabiliana nao, tunataka kutafuta pointi yoyote kesho (leo),” alisema Nsajigwa.

KMC VS FOUNTAIN

Mchezo wa mapema kabisa saa 8:00 mchana utakuwa ni kati ya KMC inayoshika mkia kwenye msimamo wa ligi, ikikutana na Fountain Gate iliyozinduka ikiwa chini ya kocha Fred Felix Minziro.

Hali ya KMC sio nzuri na kama ikipoteza mechi zake mbili zijazo kuanzia kwa Fountain Gate, itakuwa imekata tiketi ya kusubiri kupanda gari kuelekea kushiriki Ligi ya Championship msimu ujao.

KMC imefungwa mechi nne kati ya tano za mwisho na ikiwa na sare moja tu, ikibaki nafasi ya 16 na pointi zake tisa. Fountain Gate nayo haipo nafasi nzuri sana ikiwa ya 13 kwenye msimamo lakini ikishinda mechi mbili, ikipoteza tatu kwenye mechi tano za mwisho.

PAMBA JIJI VS DODOMA JIJI

Mchezo mwingine utakuwa kati ya Pamba Jiji itakayokuwa mwenyeji wa Dodoma jiji, utakaopigwa saa 10:00 jioni pale CCM Kirumba jijini Mwanza, timu zote zikiwania pointi tatu za kujiweka sehemu nzuri zaidi.

Pamba dhidi ya Dodoma itakuwa dabi ya majini huku zote zikisaka kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo ambapo wenyeji wakiwa juu na pointi 29,  chini yao wapo walima zabibu na alama 28 ambapo ushindi wa timu yoyote utaiweka pazuri.

Pamba Jiji imeshinda mechi moja tu kati ya tano za mwisho iliposhinda ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya Fountain Gate, ikipoteza tatu dhidi ya Singida Black Stars, TRA United na Yanga wakati ikipata sare moja ilipocheza na Mashujaa.

Dodoma Jiji imeshinda mechi mbili katika tano za mwisho dhidi ya Fountain Gate (2-1) na Mtibwa Sugar (1-0) zote ugenini, ikipoteza mbili dhidi ya Coastal na Azam, ikiambulia sare kwa Namungo.

Dodoma Jiji inaingia kwenye mechi hii ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi ya duru la kwanza kwa kanuni kufuatia mechi kuvunjika kulikotokana na taa za Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kutowaka wakati mechi ikiendelea hali iliyofanya kusimama.

Hadi mechi inasimama, Dodoma Jiji ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Yasin Mgaza, lakini kitendo cha mechi kuvunjika, kanuni ikaibeba Pamba Jiji iliyopewa pointi tatu na mabao matatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *