Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza haja ya kuundwa kwa mfuko wa kuwawezesha wafungwa wanapotoka gerezani, wadau wamependekeza muundo wa mfuko huo ukijumuisha ufuatiliaji wa karibu kwa wanaonufaika.

Kwa mujibu wa wadau hao, mfuko huo unapaswa kuwa wa kitaasisi wenye mfumo wa fedha unaojitegemea, huku michango ikitoka serikalini, sekta binafsi na mapato yatokanayo na shughuli za uzalishaji magerezani.

Akizungumza Mei 9, 2026 wakati akifunga mafunzo ya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania, Rais Samia alisema Serikali inapaswa kufikiria sera ya kuanzisha mfuko maalumu wa kuwasaidia wafungwa wanaotoka gerezani wakiwa na ujuzi ili waanze maisha mapya.

Kauli hiyo ilitokana na maoni ya mfungwa, Lista Charles, aliyesema ukosefu wa mitaji huwafanya baadhi ya waliotoka gerezani kurejea katika vitendo vya uhalifu.

Pendekezo hilo pia liliwahi kuibuliwa katika ripoti ya Tume ya Haki Jinai iliyoongozwa na Jaji Othman Chande, iliyoshauri kuwepo kwa mfumo wa kuwawezesha wafungwa wanapotoka jela waweze kuhimili maisha ya kawaida katika jamii.

Muundo wa mfuko

Mtaalamu wa sera, Dk Kelvin Magesa, anasema mfuko huo haupaswi kuwa wa misaada, bali taasisi yenye mfumo endelevu wa kifedha.

Anasema fedha zinaweza kutoka serikalini, sekta binafsi, taasisi za dini na mapato ya bidhaa zinazozalishwa magerezani.

“Ili mfuko huu usigeuke mradi wa kisiasa wa kugawa fedha, uwe chini ya bodi huru yenye wataalamu wa fedha, sheria, saikolojia na maendeleo ya jamii,” anasema.

Anasisitiza wafungwa wanaotoka gerezani wanahitaji zaidi mfumo wa ufuatiliaji kuliko fedha pekee.

“Ukimpa mtu mtaji bila mfumo wa kumlinda dhidi ya unyanyapaa na mazingira yaliyomrudisha kwenye uhalifu awali, unakuwa umetupa fedha gizani,” anasema.

Dk Magesa anasema nchi kama Norway na Canada zimefanikiwa kupunguza kurejea kwa wafungwa magerezani kwa kuunganisha mafunzo, mikopo midogo, ushauri wa kisaikolojia na ajira za mpito.

Kwa upande wake, Profesa Esther Nyangine anasema mfuko huo uwe wa kitaifa, lakini utekelezaji wake ushuke hadi ngazi ya halmashauri ili kurahisisha usimamizi.

Anasema sehemu ya fedha inaweza kutoka kwenye mapato ya shughuli za uzalishaji ndani ya magereza kama useremala, kilimo, ushonaji na ufundi.

“Tunapaswa kuacha kufikiri wafungwa wakitoka jela wanaanza maisha kutoka sifuri. Wengi tayari wanakuwa na ujuzi, kinachokosekana ni daraja la kuwaunganisha na uchumi rasmi,” anasema.

Mtaalamu wa sheria, Neema Chusiku, anasema uwezeshaji huo usiegemee kutoa fedha taslimu moja kwa moja.

Anashauri waliotoka gerezani wapewe kwanza vifaa vya kazi, mafunzo ya matumizi ya fedha na maeneo ya kufanyia kazi kabla ya kupewa mitaji mikubwa.

“Mtu aliyekaa gerezani kwa muda mrefu anaweza kushindwa kuendana haraka na mabadiliko ya kijamii, hivyo kumpa fedha nyingi bila maandalizi ni kuongeza hatari ya kushindwa tena,” anasema.

Aidha, anapendekeza mfumo wa ushirika kwa wafungwa wenye fani zinazofanana ili waunde vikundi vya uzalishaji vinavyoweza kusaidiwa na Serikali kupitia zabuni ndogondogo.

Naye, Mtaalamu wa Saikolojia, Dk Baraka Mwinuka, anasema uwezeshaji huo uwe wa hatua tatu– tathmini ya kisaikolojia, mafunzo ya maisha ya uraiani na mtaji unaofuatiliwa kwa karibu kwa angalau miaka miwili.

Anasema changamoto kubwa kwa wafungwa wanaotoka gerezani si fedha pekee bali pia kukataliwa na jamii.

“Kama jamii itaendelea kumuona mtu aliyewahi kufungwa kama takataka, hata ukimpa Sh20 milioni atarudi kule kule. Tunahitaji kurejesha utu wake kwanza,” anasema.

Mchambuzi wa sera na maendeleo, Sophia Mrema, anasema hatua hiyo inaweza kuwa mageuzi makubwa katika mfumo wa haki jinai nchini ikiwa itasimamiwa vizuri.

Kwa mtazamo wake, mfuko huo unaweza kusaidia kupunguza msongamano magerezani, gharama za kuwahudumia wafungwa na kuongeza uzalishaji wa kiuchumi kwa kuwa baadhi yao watakuwa wafanyabiashara na waajiri.

“Haya yakifanyika vizuri, Tanzania inaweza kujenga kizazi cha watu waliowahi kukosea lakini wakageuka kuwa ushuhuda wa pili wa maisha,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *