Nchini Zimbabwe, serikali imetangaza nia yake ya kurudisha mashamba 67 kwa wamiliki wa zamani wa kigeni waliopoteza sehemu zao za ardhi katika miaka ya 2000. Chini ya utawala wa Robert Mugabe, wakulima elfu kadhaa wazungu walinyang’anywa ardhi, kwa manufaa ya watu weusi walionyang’anywa ardhi wakati wa ukoloni. Sera hii yenye utata ilisababisha kuanguka kwa uchumi wa nchi nzima.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Na mwandishi wetu wa kikanda, Claire Bargelès

Serikali ya Emmerson Mnangagwa inasisitiza kwamba hatua hizi mpya hazitii shaka mpango wa mageuzi ya ardhi wa Mugabe, bali ni ishara ya kubadilisha ukurasa kuhusu migogoro iliyoanza miaka ya 2000. Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Kilimo mbele ya Bunge. Mashamba haya yatarejeshwa kwa wakulima kutoka Denmark, Uswisi, Ujerumani, na Uholanzi, ili kuheshimu makubaliano ya uwekezaji kati ya nchi hizi na Zimbabwe.

Lakini mashamba haya yaliyotelekezwa yatakuwa magumu kuyarejesha, kulingana na Johan Willemse, profesa wa uchumi wa kilimo kutoka Afrika Kusini: “Miundombinu mingi iliyokuwa kwenye mashamba haya haipo tena. Mashamba haya yangelazimika kuendelezwa upya kuanzia mwanzo; si kama watu wangeyapata katika hali ile ile waliyoyaacha. Kwa hivyo itakuwa vigumu sana kuchukuwa mashamba hayo, kuwaondoa watu ambao wanayashikilia kwa sasa, kuwekeza tena, na kuyafanya yawe na tija tena. Baadhi ya watu huniambia hawako tayari kuchukua hatari hizo hivi sasa.”

Kulingana na Johan Willemse, ambaye baba yake alikuwa na shamba nchini Zimbabwe, hatua hiyo inalenga hasa kutuliza nchi za Magharibi, wakati Harare ikitafuta makubaliano ya kurekebisha deni: “Nadhani kuna mashaka mengi yanayozunguka tangazo hili na kwamba kimsingi ni ishara kutoka kwa serikali kuonyesha kuwa iko tayari kuzungumzia suala hili.”

Zaidi ya mashamba 800 yatarudishwa kwa Wazimbabwe Weusi walioyamiliki kabla ya enzi ya ukoloni, kulingana na waziri, na wakulima wazungu wapatao 400 wataruhusiwa kununua tena sehemu zao za ardhi ili waendelea kuzimiliki. Kuhusu mengine, serikali ya Zimbabwe, mnamo mwaka 2020, ilitangaza makubaliano ya fidia ya dola bilioni 3.5 kwa wakulima wote walionyang’anywa mashamba yao, lakini bila kuwa na uwezo wa kufadhili hatua hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *