YANGA imerejea nyumbani jana ikitokea Singida ilipokwenda kucheza dhidi ya Dodoma Jiji na kusitishiwa rekodi yao ya kutopoteza mechi ya 43 mfululizo, baada ya kuchapwa mabao 3-2, sasa kocha wa muda wa kikosi hicho ametoa kauli ambayo itakwenda kuwatuliza mashabiki wa timu hiyo.
Kabla ya kufungwa na Dodoma Jiji, Yanga mara ya mwisho kupoteza mechi ya Ligi Kuu Bara ilikuwa Novemba 7, 2024 ilipochapwa 3-1 na Tabora United ambayo sasa ni TRA United kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar. Baada ya hapo, imecheza mechi 42 mfululizo za ligi bila ya kupoteza ikishinda 35 na sare saba. Ile ya 43 ikakutana na kichapo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Abdihamid Moallin ambaye amechukua nafasi ya Pedro Concalves ambaye ameachana na timu hiyo hivi karibuni amesema kila mmoja ndani ya timu hiyo ameshtushwa na matokeo hayo, Yanga ikipoteza kwenye mchezo ambao walitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini ikakosa bahati.
Moallin amesema kipigo hicho kimewasitishia rekodi yao ya kutopoteza lakini bado kikosi hicho kipo salama kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kwamba hawatakiwi kuendelea kuinamisha vichwa chini.
“Tumepoteza, kila mmoja unaona namna alivyopata mshtuko wa matokeo haya, kwenye mchezo wa soka matokeo kama haya yanatokea, kinachoumiza ni kwamba tumepoteza kwenye mchezo ambao tuliutawala na kutengeneza nafasi nyingi lakini haikuwa bahati yetu,” amesema Moallin.
“Tulifanya makosa ya kutotumia nafasi lakini pia tukafanya makosa ambayo wenzetu wakayatumia kwenda kurudisha mabao yetu na kuongeza lingine, tunawapa pole mashabiki wetu watusamehe.
“Hakuna nafasi ya kuendelea kuinamisha vichwa chini, hii ni klabu kubwa ambayo haraka tunatakiwa kurudi kwenye njia ya ushindi, tumepoteza mechi moja ya kwanza kwenye ligi,bado tuna nafasi ya kupigania ubingwa.”
Moallin ameongezakuwa, ukomavu wa wachezaji wa timu hiyo anaamini watautumia kujirekebisha na kurudi kushinda mechi zilizosalia ili kuwapa furaha muhimu mashabiki wa timu hiyo kwa kuchukua ubingwa.
“Hatuchezi ligi kwa kutafuta rekodi ya kutokufungwa, kila timu inacheza kwa kutafuta ubingwa, tuna wachezaji wenye uzoefu mkubwa, wameshakutana na mazingira kama haya, tutazungumza nao na kuwarudisha mchezoni.
“Kitu muhimu ambacho kitakwenda kuwatuliza mashabiki wetu ni kupata ubingwa msimu huu, hiki ndio ambacho kila timu inayocheza ligi inakitaka, tutarudi tukiwa imara zaidi.”
Licha ya kipigo hicho, Yanga inaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 54 baada ya mechi 23, inafuatiwa na Simba ambayo jana ilicheza na Mashujaa, kabla ya mechi hiyo ilikuwa na pointi 49 ikicheza mechi 22.