
Ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia 2026 chini ya kaulimbiu “Familia, Ukosefu wa Usawa na Ustawi wa Mtoto,” Umoja wa Mataifa unasema maadhimisho ya mwaka huu yanaangazia jinsi umaskini, ukosefu wa huduma muhimu na msaada mdogo wa malezi vinavyoathiri familia na kudhoofisha maendeleo bora ya watoto.
Maadhimisho haya yanalenga kuhamasisha serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia kuimarisha mifumo ya ulinzi wa kijamii na kupunguza tofauti zinazoendelea kuathiri familia zilizo katika mazingira magumu duniani kote.
Ongezeko la ukosefu wa usawa ni hatari kwa hatma ya watoto
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, familia nyingi zinakabiliwa na ukosefu wa kipato cha uhakika, gharama kubwa za malezi ya watoto pamoja na ukosefu wa huduma sawa za afya, elimu na teknolojia ya kidijitali.
Changamoto hizi zinawaweka watoto katika hatari kubwa ya afya duni, kukatiza masomo na kuendelea kuishi katika umaskini wa muda mrefu.
Hali hiyo Umoja wa Mataifa unasema huwa mbaya zaidi kwa familia zinazokabiliwa na ubaguzi unaohusiana na jinsia, rangi, uhamiaji au ulemavu. “Familia ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, lakini familia nyingi zinaendelea kukumbwa na ukosefu mkubwa wa usawa unaopunguza fursa kwa watoto,”
Umoja wa Mataifa umesema katika taarifa yake. “Bila msaada wa kutosha, ustawi wa watoto na matarajio yao ya baadaye huwekwa hatarini.”
Wito watolewa kuimarisha mifumo ya ulinzi wa kijamii
Maadhimisho hayo yataweka mkazo maalum kwenye hatua jumuishi za ulinzi wa kijamii kama vile ruzuku za watoto, likizo za uzazi zenye malipo, huduma nafuu za malezi ya watoto na elimu ya awali kwa watoto wadogo.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema hatua hizo ni muhimu katika kusaidia familia kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi, kupunguza umaskini na kuhakikisha watoto wanapata fursa sawa za maendeleo.
Maadhimisho haya pia yanatatoa jukwaa kwa nchi wanachama, mashirika ya Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia kubadilishana uzoefu na kuonesha sera zilizofanikiwa katika kuimarisha mnepo wa familia na ustawi wa watoto kulingana na Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.
Mabadiliko ya tabianchi yaongeza mzigo kwa familia maskini
Umoja wa Mataifa pia umeonya kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaongeza ukosefu wa usawa, hasa kwa familia maskini katika nchi zinazoendelea zinazotegemea kilimo na rasilimali za asili.
Mashamba ya familia, ambayo yanaunda karibu asilimia 80 ya mashamba yote duniani, yanaendelea kukabiliwa na kupungua kwa mavuno na kuongezeka kwa uhaba wa chakula kutokana na hali mbaya ya hewa.
“Familia zenye kipato cha chini ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi kwa sababu mara nyingi hazina rasilimali wala miundombinu ya kukabiliana na majanga na mishtuko ya mazingira,” taarifa hiyo imeeleza.
Wakati huo huo, familia zimehimizwa kutumia mbinu rafiki kwa mazingira kama kupunguza matumizi ya nishati, kupunguza taka na kula nyama na bidhaa za maziwa kwa kiwango kidogo ili kusaidia kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi.
Utafiti mpya kuzinduliwa kuhusu mwenendo wa ukosefu wa usawa
Kama sehemu ya maadhimisho hayo, Umoja wa Mataifa leo unazindua utafiti mpya unaochunguza mwenendo wa ukosefu wa usawa duniani pamoja na sera zinazoweza kuboresha ustawi wa watoto na kuimarisha mifumo ya kusaidia familia.
Waandalizi wanasema majadiliano hayo yataonesha umuhimu wa hatua za pamoja kuhakikisha watoto wote, bila kujali asili au mazingira yao, wanapata fursa sawa za kufanikiwa maishani.
“Kuwekeza katika familia ni kuwekeza katika mustakabali wa jamii,” Umoja wa Mataifa umesisitiza huku ukitoa wito wa dhamira kubwa zaidi ya kisiasa katika kutekeleza sera zinazolinda watoto na kupunguza ukosefu wa usawa duniani.