
Akizungumza katika makao makuu ya WHO mjini Geneva Ijumaa hii, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema amefanya mazungumzo na Waziri wa Afya wa DRC, Roger Kamba, kuhusu mlipuko huo.
Kwa mujibu wa Dkt. Tedros, ambaye katika mkutano huo ameambatana na Dkt. Mohamed Janabi ambaye ni Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika, hadi sasa visa 13 vya Ebola vimethibitishwa na Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Tiba ya Kibayolojia (INRB) mjini Kinshasa. Tedros ameeleza kuwa WHO ilipokea taarifa za awali za wagonjwa walioshukiwa kuwa na Ebola tarehe 5 Mei na mara moja kutuma timu Ituri kusaidia mamlaka za afya katika uchunguzi wa mlipuko huo pamoja na ukusanyaji wa sampuli.
Vipimo vya awali vilivyofanyika eneo la tukio vilionesha matokeo hasi ya Ebola. Hata hivyo, baadhi ya sampuli zilizotumwa baadaye Kinshasa zilithibitishwa kuwa na maambukizi ya Ebola na INRB siku ya Alhamisi.
“Huu ni mlipuko wa 17 wa Ebola kurekodiwa nchini DRC tangu virusi hivyo vilipogunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976,” amesema Dkt. Tedros, akibainisha kuwa DRC ina uzoefu mkubwa katika kudhibiti na kukabiliana na milipuko ya Ebola.
Mshikamano
Wataalamu wa WHO tayari wanafanya kazi bega kwa bega na mamlaka za afya za DRC katika jimbo la Ituri kuimarisha hatua za kukabiliana na mlipuko huo. Wataalamu zaidi wa mawasiliano ya hatari, ushirikishwaji wa jamii, udhibiti wa maambukizi, huduma za kliniki na usafirishaji wanatarajiwa kujiunga na timu hiyo katika siku zijazo.
Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa pia limepeleka vifaa vya tiba na vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi katika mji wa Bunia, ambao ni makao makuu ya jimbo la Ituri, kusaidia juhudi za kudhibiti maambukizi.
Dkt. Tedros ametangaza kutolewa mara moja kwa dola za Marekani 500,000 kutoka Mfuko wa Dharura wa WHO ili kusaidia kuimarisha mwitikio dhidi ya mlipuko huo.
Hatua za kipaumbele katika kukabiliana na mlipuko huo ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, kutafuta wagonjwa na waliokutana nao, kuzuia maambukizi katika vituo vya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma salama za matibabu pamoja na kuongeza uwezo wa upimaji wa maabara.
WHO imesema itaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali ya DRC pamoja na wadau mbalimbali katika eneo hilo ili kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo na kuhakikisha walioathirika wanapata huduma zinazohitajika.