
Akizungumzia maendeleo ambayo amesema ni “ya umuhimu mkubwa”, amesema kuwa tarehe 10 Mei, Atef Najib alifikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya uhalifu uliotekelezwa mwanzoni mwa mapinduzi ya Daraa mwaka 2011.
Bashar al-Assad aliyekuwa Rais wa Syria, Maher al-Assad na wengine pia wanahukumiwa kwa kutokuwepo mahakamani katika kesi hiyo hiyo.
Kwa mujibu wa Mjumbe huyo mashtaka hayo yanajumuisha ukandamizaji wa vurugu dhidi ya maandamano ya amani, watu kuwekwa kizuizini kiholela, mateso yakiwemo dhidi ya watoto pamoja na vifo vilivyotokea wakiwa mahabusu.
Amebainisha kuwa hati ya mashtaka inatumia sheria za Syria pamoja na sheria za kimataifa, na kusema “Ni juhudi zinazostahili pongezi kuweka uwajibikaji ndani ya mfumo mpana wa kisheria unaoakisi wajibu wa Syria katika haki za binadamu kimataifa.”
Kukamatwa kwa washukiwa ni mtihani wa dhamira ya Syria kwa haki
Katika kile alichokiita “maendeleo yenye ishara kubwa”, Bwana. Cordone amesema Amjad Yusef mshukiwa mkuu katika mauaji ya Tadamon mwaka 2013 alikamatwa tarehe 24 Aprili.
Na tarehe 29 Aprili, Meja Jenerali wa zamani Adnan Abboud Hilweh alikamatwa kuhusiana na shambulio la kemikali la Ghouta Mashariki mwaka 2013.
“Namna Syria itakavyoshughulikia uhalifu huu itakuwa kipimo muhimu cha dhamira ya nchi hiyo kwa haki na utawala wa sheria,” amesisitiza.
“Pia tunaamini kuwa mwenendo huu wa kesi unaweza kufichua ukweli kamili kuhusu uhalifu huo ambalo ni moja ya madai makuu ya manusura,” amesema.
Hatua za Israel zatishia uthabiti wa Syria, asema Mjumbe wa UN
Katika masuala ya usalama, Bwana. Cordone ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu uwepo unaoendelea na shughuli za kijeshi za Vikosi vya Ulinzi vya Israel mashariki mwa mstari wa kusitisha mapigano, jambo ambalo amesema linakiuka Mkataba wa Kutenganisha Vikosi wa mwaka 1974.
Amesisitiza kuwa “Hatua hizi zinakiuka mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya Syria, zinatishia uthabiti wa Syria na kuwaathiri raia”.
Pia ametaja “tukio la kutia wasiwasi” mjini Idlib lililohusisha wanamgambo wa Uzbekistan, pamoja na shambulio la Daesh lililomuua kiongozi wa dini ya Kishia mjini Damascus.
Aidha, amekumbusha ujumbe alioupata katika mkutano wake wa hivi karibuni na wanawake wa Syria kutoka Idlib kwamba, “Ushiriki wa maana wa wanawake katika maisha ya umma ni muhimu katika kuimarisha mshikamano wa kijamii na kusaidia kupona kwa Syria.”
Mahitaji ya kibinadamu Syria bado ni makubwa: Fletcher
Nchini Syria, “maendeleo yapo kweli, lakini ni dhaifu, tunahitaji msaada wenu wa dhati,” amesema Mratibu Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher mbele ya Baraza la Usalama.
Amesema vurugu zimepungua, vikwazo vimelegezwa na kurejea kwa wakimbizi pamoja na watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi kunaongezeka.
Hata hivyo amesema, “ufadhili unapungua kwa kasi zaidi kuliko mahitaji, huku mahitaji ya kibinadamu yakibaki kuwa makubwa sana.”
Theluthi mbili ya wananchi ambayo ni watu milioni 15.6, wengi wao wakiwa wanawake, wasichana na watoto watahitaji msaada mwaka huu.
“Viwango vya sasa vya ufadhili vinamaanisha tutafikia karibu nusu yao pekee,” amesisitiza.
Bei zapanda kutokana na usumbufu wa Hormuz
Bwana. Fletcher amesema zaidi ya watu 390,000 wamevuka mpaka kutoka Lebanon tangu mapema Machi wengine 90,000 tangu alipolihutubia Baraza mwezi Aprili.
Wakati huo huo, kufungwa kwa muda mrefu kwa Mlango wa Hormuz kumesababisha kupanda kwa gharama za chakula na mafuta, jambo ambalo amesema “lina madhara ya haraka kwa jamii ambazo tayari ziko ukingoni.”
Amesema bei ya dizeli imeongezeka kwa takribani asilimia 17, huku gharama ya umeme ikiongezeka kwa “mamia ya asilimia katika baadhi ya maeneo. Ingawa bei ya mkate wa ruzuku haijabadilika, mikate imepungua ukubwa kwa asilimia 12.”
Kutokana na hali hiyo, amesema ombi la misaada ya kibinadamu limefadhiliwa kwa zaidi kidogo ya asilimia 16 pekee, ambapo dola milioni 480 zimepatikana kati ya mahitaji ya dola bilioni 2.9.
Takribani asilimia 90 ya fedha hizo zinatoka Marekani, Ulaya, Japan na Canada. “Dunia nzima iko wapi?” amehoji.
Syria yataja mafanikio ya kisiasa na taasisi
“Njia ya haki ya mpito inaendelea mbele kama moja ya nguzo za Syria mpya,” amesema Ibrahim Olabi Mwakilishi wa Kudumu wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa.
Amesema majina ambayo zamani yalitajwa kwa hofu sasa “yanatajwa waziwazi mahakamani, huku kesi za hadhara dhidi ya wahusika wa ukiukwaji mkubwa wa haki zikiendelea”.
Akizungumzia mafanikio ya mwezi huu, ameeleza kuwa Syria imepiga hatua 36 katika kiashiria cha uhuru wa vyombo vya habari kilichochapishwa na Waandishi wa habari wasio na mipaka au kwa lugha ya Kiingereza Reporters Without Borders.
Kamati Kuu ya uchaguzi wa Baraza la Watu pia imetoa orodha ya mwisho ya kamati ndogo katika Al-Hasakah, hatua nyingine kuelekea kujenga upya maisha ya kisiasa na taasisi amesema.
Aidha, amesema “zaidi ya wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao milioni 3.5 wamerejea Syria, huku mabilioni ya dola yakiwekezwa katika Syria mpya”, akitaja kongamano la kwanza la uwekezaji kati ya Emarati na Syria.
Pia amezungumzia kurejeshwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Muungano wa Ulaya EU na Syria.
Ameishutumu Israel kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya mwaka 1974, akisema kila mara Syria inapothibitisha dhamira yake kwa diplomasia inayosimamiwa na Marekani, Israel hushambulia. “Wananchi wa Syria wanauliza: dunia itafanya nini?”