
Katika mkutano huo unaolenga “Kulinda Upatikanaji wa Nishati na Minyororo ya Ugavi: Kusaidia Maendeleo ya Dunia Kupitia Ushirikiano wa Kimataifa”, Rais wa ECOSOC, Locke Tapa, amesema kupanda kwa gharama za mafuta, usafirishaji na chakula kunaongeza mzigo wa kifedha kwa mataifa yaliyo hatarini, hususan nchi maskini na mataifa ya visiwa vidogo.
Naye Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya uchumi na jamii, Li Junhua, amesema kuwa hali hiyo inaongeza mfumuko wa bei, kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuzifanya nchi nyingi kushindwa kukabiliana na madeni makubwa.
Uhakika wa chakula na utalii uatarini
Washiriki wameonya kuwa kuendelea kwa changamoto katika minyororo ya ugavi kunaweza kuongeza zaidi bei za mbolea na chakula, hali itakayohatarisha uzalishaji wa kilimo na kuongeza ukosefu wa uhakika wa chakula, hasa katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia Kusini. Mataifa yanayotegemea utalii pia yanatarajiwa kupata hasara kubwa kutokana na kupanda kwa gharama za nishati na usafirishaji.
Wito wa ushirikiano wa kimataifa
Umoja wa Mataifa umetaka kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa ili kuhakikisha masoko ya biashara na nishati yanaendelea kuwa wazi, kuongeza ufadhili, na kuwekeza katika mifumo endelevu ya nishati. Li Junhua amesema hatua za pamoja za kimataifa zinahitajika ili kujenga minyororo ya ugavi iliyo imara zaidi na kusaidia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu ya muda mrefu.