
Kupitia taarifa iliyotolewa Ijumaa jioni mjini New York Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unaunga mkono juhudi zote za kusitisha mapigano na kupunguza mateso ya wananchi wanaoishi pande zote za Blue Line, mpaka unaotenganisha Israel na Lebanon.
Katibu Mkuu pia ametoa wito kwa pande zote kuheshimu kikamilifu usitishaji huo wa mapigano, kusitisha mashambulizi yoyote zaidi na kutekeleza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, ikiwemo sheria za kimataifa za kibinadamu wakati wote.
Aidha, Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa utaendelea kuunga mkono juhudi zote za kidiplomasia zinazolenga utekelezaji kamili wa Azimio 1701 la Baraza la Usalama la mwaka 2006, ambalo lilipitishwa kwa lengo la kuimarisha amani na usalama katika eneo hilo.
