WUF13 yang’oa nanga Baku mawaziri wajadili mgogoro wa makazi dunianiWUF13 yang’oa nanga Baku mawaziri wajadili mgogoro wa makazi duniani

Washiriki wa mkutano huo wa mawaziri wamejadili namna ya kufanya miji iwe salama zaidi, imara dhidi ya majanga na kuhakikisha makazi yanakuwa nafuu zaidi kwa wananchi.

Majadiliano hayo yanatokana na Ajenda Mpya ya Miji iliyopitishwa miaka kumi iliyopita katika mkutano wa Habitat III mjini Quito, Ecuador, unaoweka misingi ya maendeleo ya miji hadi mwaka 2036.

Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-Habitat, Anaclaudia Rossbach amesema mwaka 2026 haupaswi kuwa tu mwaka wa tathmini bali mwaka wa kurekebisha mwelekeo.” Amesisitiza umuhimu wa kupitia sera zilizofanikiwa na zile zinazohitaji kufikiriwa upya.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, nchi nyingi zimepiga hatua zinazoonekana. Takribani nchi 160 tayari zimepitisha au zinaandaa sera za kitaifa za maendeleo ya miji, huku zaidi ya theluthi mbili ya nchi duniani zikiwa zimeanzisha programu za kuhakikisha upatikanaji wa nyumba nafuu.

Hata hivyo, Rossbach ameonya kuwa juhudi hizo bado hazitoshi. “Sekta ya makazi inaonesha hali hii wazi kabisa,” amesema. “Leo zaidi ya watu bilioni 1.1 wanaishi katika makazi holela au duni duniani.” Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 120 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita walizaliwa au walihamia katika makazi hayo duni.

Kupambana na umaskini kupitia makazi

Majadiliano hayo yamegawanywa katika mada kuu tatu. Kikao cha kwanza kilijikita katika makazi kama nyenzo ya kujumuisha jamii na kupunguza umaskini. Washiriki wamejadili namna ya kupanua programu za nyumba za kijamii, kuboresha makazi holela na kulinda makundi yaliyo hatarini zaidi.

Uangalizi maalum umeelekezwa kwa nchi zinazojijenga upya baada ya vita na uharibifu. Meya wa mji wa Homs nchini Syria, Bashar Al Sebaai ambaye mji wake umeharibiwa vibaya wakati wa miaka ya vita, ameeleza changamoto kubwa zinazoukabili mji huo leo katika mahojiano na UN News.

“Watu 400,000 walirejea mjini baada ya vita. Walirudi katika maeneo yaliyoharibiwa vibaya,” amesema. “Ni vigumu sana taka ngumu, miundombinu, umeme ni vigumu kupata suluhisho kwa matatizo haya yote.”

Kwa mujibu wa meya huyo, mji huo unahitaji kwa haraka siyo tu mawazo na utaalamu, bali pia ufadhili wa kurejesha huduma za msingi na miundombinu.

UNICEF Mji wa Homs nchini Syria uliosambaratishwa na vita

Makazi kama chachu ya uchumi

Majadiliano ya pili yamechunguza sekta ya makazi kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi. Washiriki wameeleza kuwa sekta hiyo inaweza kusaidia kuunda ajira, kuongeza uzalishaji na kupanua fursa kwa wanawake na vijana.

Wazungumzaji wamesisitiza mara kwa mara umuhimu wa kuwa na mtazamo wa pamoja katika kushughulikia changamoto hiyo.

“Ni suala la ardhi. Ni suala la miundombinu. Ni suala la fedha, utawala, hatua za kukabiliana na tabianchi, na haki za binadamu,” amesema Rossbach.

Mabadiliko ya tabianchi na miji

Kikao cha tatu kimejikita katika uhusiano kati ya makazi na mabadiliko ya tabianchi. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza kuwa sekta ya ujenzi bado ni moja ya vyanzo vikubwa vya uzalishaji wa gesi chafuzi duniani, huku mamilioni ya watu wanaoishi katika makazi yasiyo salama wakiwa wa kwanza kuathiriwa na mafuriko, mawimbi ya joto na majanga mengine yanayohusiana na tabianchi.

Mawaziri wamejadili ujenzi wenye kiwango kidogo cha hewa ukaa, upangaji wa miji unaostahimili majanga na kuboresha makazi holela kwa kuzingatia athari za tabianchi. Kwa mujibu wa Rossbach, zaidi ya asilimia 80 ya miji duniani sasa ina joto kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa miongo miwili iliyopita.

Siku ya kwanza ya jukwaa hilo pia imekumbwa na mvua kubwa za muda mrefu mjini Baku, hali iliyolazimisha mamlaka za jiji kuchukua hatua za haraka kuondoa maji katika barabara zilizofurika. Wakazi wa eneo hilo wamebainisha kuwa matukio kama hayo ya hali mbaya ya hewa yalikuwa nadra nchini Azerbaijan miaka michache iliyopita, hasa katika kipindi hiki cha mwaka.

Mkutano wa mawaziri mjini Baku unatarajiwa kusaidia maandalizi ya kikao cha Julai cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kitakachofanya tathmini rasmi ya utekelezaji wa Ajenda Mpya ya Miji.

© UN-Habitat Baku, Azerbaijan, mwenyeji wa Kikao cha Kumi na Tatu cha Jukwaa la Miji Duniani (WUF13) kuanzia tarehe 17–22 Mei 2026, kilichoandaliwa na UN-Habitat na Serikali ya Azerbaijan.

Matukio mengine siku ya kwanza ya WUF13

Sambamba na mikutano ya mawaziri, makongamano mbalimbali ya mada maalum yameanza mjini Baku yakiwakusanya wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa. Makongamano hayo yanajadili masuala mbalimbali kuanzia wanawake na vijana hadi nafasi ya mashirika ya kiraia na kampuni binafsi katika maendeleo ya miji.

Mmoja wa washiriki wa makongamano hayo, msanifu majengo kutoka New York na mwanzilishi wa Consortium for Sustainable Urbanization, Lance Jay Brown ameiambia UN News kuwa mgogoro wa makazi umeacha kuwa tatizo linaloathiri nchi maskini pekee.

“Sekta ya makazi imekuwa kama treni inayokwenda kasi bila udhibiti,” amesema. “Bado tuko katika hali hiyo.”

Brown amebainisha kuwa katika maisha yake idadi ya watu duniani imeongezeka karibu mara nne, huku upatikanaji wa nyumba nafuu kwa jamii zenye kipato cha chini ukiendelea kuwa mgumu zaidi.

“Siyo tu kuwa na paa juu ya kichwa,” amesema. “Inamaanisha elimu, usafiri, afya.”

Ameitaja Marekani kama mfano unaoonesha ukubwa wa mgogoro huo.

“Tunapokuwa na mamia ya maelfu ya watu wasiokuwa na makazi wanaoishi mitaani nchini Marekani, wakati tunachukuliwa kuwa taifa tajiri” amesema. “Huko New York, hali inaonekana kama mgogoro mkubwa kwa sasa.”

Brown ameeleza matumaini yake kuwa majadiliano na maamuzi yatakayotokana na mkutano wa Baku yatasaidia kuibua suluhu za vitendo kwa mgogoro wa makazi duniani.

“Tumieni makongamano haya kujenga ushirikiano utakaoendelea hata baada ya wiki hii. Leteni uzoefu wa maisha halisi mezani. Unganisheni fedha, sera na utekelezaji,” Rossbach amewaambia washiriki wakati wa ufunguzi wa makongamano hayo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *