London, England. Beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville amemsifu kaimu meneja wa timu hiyo, Michael Carrick kwa mchango wake lakini ameonya kuwa kazi ngumu ndiyo inaanza sasa huku kocha huyo akikaribia kupata nafasi ya muda mrefu Old Trafford.
Inatarajiwa Carrick atapewa mkataba wa miaka miwili kuendelea kuwa Meneja wa Man United baada ya kuipa uhai upya timu kufuatia kipindi chenye misukosuko cha Ruben Amorim.
Neville alisema kuwa hashangazwi kuona Carrick akipewa mikoba ya kudumu kutokana na kile alichokifanya ndani ya muda mfupi.
Kocha wa Manchester United, Michael Carrick. Picha na Mtandao
“Mabadiliko yamekuwa ya kushangaza. Carrick na benchi lake la ufundi wamefanya kazi kubwa sana, tangu dakika ya kwanza kabisa na katika mechi dhidi ya Man City na Arsenal.
“Sijui ilikuwaje hali ilishuka sana katika kipindi kabla Michael hajaingia, kisha wakafika viwango walivyofikia katika mechi mbili zilizofuata.
“Kisha wamekuwa thabiti sana katika kushinda mechi hata zile ambazo hawakucheza vizuri. Wamekuwa na mshikamano zaidi na wanaonyesha nguvu kubwa zaidi,” amesema Neville.
Neville amempa angalizo Carrick akidai kuwa kutakuwa na ugumu zaidi mara baada ya kupewa mkataba wa kudumu kuliko anaokutana nao sasa.
Kocha wa Manchester United, Michael Carrick. Picha na Mtandao
“Carrick ameleta utulivu klabuni, ndani na nje ya uwanja. Ndani ya uwanja, wachezaji wako huru zaidi. Lakini nje ya uwanja mashabiki wana furaha zaidi. Hiyo inakuja pamoja na matokeo, lakini kwa ujumla wanamfahamu Michael na wanamuamini.
“Baada ya miaka michache yenye misukosuko, hiki kimekuwa kipindi bora zaidi kwa klabu. Anastahili pongezi nyingi kwa hilo.
“Michael ni mtu halisia. Ameona ubora unavyopaswa kuwa katika klabu hii ya soka na ameona katika miezi michache iliyopita timu iliyofanya vizuri chini yake. Lakini atatambua kwamba kazi ngumu na changamoto zinaanza sasa.
“United kwa kiasi kikubwa wamehakikisha nafasi yao, wamepata soka la Ligi ya Mabingwa. Dakika atakayopata kazi rasmi ndiyo mwanzo halisi kwa Michael,” alisisitiza Neville.
Kocha wa Manchester United, Michael Carrick akikumbatiana na kiungo wake Kobbie Mainoo. Picha na Mtandao
Neville aliongeza kuwa presha kwa Carrick sasa itakuwa kubwa hivyo anapaswa kujipanga vilivyo kukabiliana nayo.
“Amefanya kazi kubwa kama kocha wa muda na wa mpito lakini kuwa kocha wa kudumu kunakuja na shinikizo tofauti na kiwango tofauti cha matarajio.
“Manchester United wanahitaji wachezaji wengi. Tuwe wazi kabisa. Michael hatadanganywa na hilo, wala shabiki yeyote wa Man Utd.
“Kuna kiini cha wachezaji watano au sita wa kujenga timu kuzunguka, lakini zaidi ya hapo kunahitajika nyongeza zitakazoongeza ubora, utulivu na uimara. Ukipata majeraha mawili au matatu katika nafasi fulani mambo yanaharibika haraka sana,” aliongeza Neville.
