Tabora yaongoza uzalishaji wa asali TanzaniaTabora yaongoza uzalishaji wa asali Tanzania

Tabora. Mkoa wa Tabora umeendelea kuongoza kwa uzalishaji wa asali yenye ubora nchini, ukichangia takriban asilimia 50 ya asali yote inayozalishwa Tanzania, pamoja na mazao mengine yatokanayo na nyuki.

Hayo yameelezwa leo Mei 18, 2026 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, John Mboya, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelekea maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani, ambayo kitaifa yatafanyika mkoani humo.

Mboya amesema ubora wa asali ya Tabora unatokana na uwepo mkubwa wa misitu ya miti ya jamii ya miyombo, ambayo imeelezwa kuwa chanzo kikuu cha asali ya asili na yenye viwango vya juu vya ubora.

“Tabora tuna asali bora na yenye viwango vya kimataifa. Ni asali ya asili kabisa inayotokana na miti ya miyombo ambayo inapatikana kwa wingi katika mkoa wetu,” amesema.

Ameongeza kuwa takriban asilimia 65 ya misitu ya Tabora imefunikwa na miti ya miyombo, hali inayochangia moja kwa moja ubora wa asali inayozalishwa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, John Mboya, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani, ambayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024, Tanzania ilizalisha zaidi ya tani 33,000 za asali, ambapo sehemu kubwa inatoka mkoani Tabora, jambo linaloendelea kuipa mkoa huo nafasi ya kipekee katika sekta hiyo.

“Tanzania inasifika duniani kwa uzalishaji wa asali bora, lakini fahari kubwa ni kwamba ubora huo kwa kiasi kikubwa unatoka Tabora,” ameongeza.

Mboya ametoa wito kwa wawekezaji kuwekeza katika uchakataji wa mazao ya nyuki, akisema mkoa huo una fursa kubwa ya kuongeza thamani ya asali badala ya kuiuza ikiwa ghafi.

“Tunahitaji wawekezaji kuja Tabora ili kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki. Malighafi tunayo ya kutosha,” amesema.

Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Tabora wamesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kiuchumi na kielimu, hasa kwa wafanyabiashara wadogo wanaonufaika na shughuli hizo.

Naye mkazi wa eneo hilo, Juma Mgondi, amesema asali imekuwa na mchango mkubwa katika afya yake, akidai ilimsaidia kupona majeraha.

“Mimi niliungua moto na nilikuwa napakwa asali asubuhi na jioni, nikapona haraka,” amesema.

Mkoa wa Tabora utakuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani, yatakayofanyika Mei 20, 2026, ambapo wadau mbalimbali, taasisi na wananchi wanatarajiwa kushiriki.

Kabla ya kilele hicho, Mei 19 kutakuwa na matembezi ya kutangaza asali ya Tabora, huku Mei 22 yakitarajiwa kuwa kilele cha maadhimisho hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *