Tanzania yaweka mipaka mkataba wa afya na MarekaniTanzania yaweka mipaka mkataba wa afya na Marekani

Dar es Salaam. Tanzania imewahakikishia wananchi italinda masilahi ya Taifa na kuhakikisha pande zote zinanufaika kwa usawa wakati mazungumzo yanaendelea kuhusu pendekezo la makubaliano (MoU) mapya ya ushirikiano wa afya kati yake na Marekani.

Mkataba huu unakuja baada ya kuondolewa kwa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Februari 2025. Hata hivyo, baadhi ya nchi za Afrika zilikataa pendekezo la mkataba huo na Marekani baada ya kuibuka hofu kuhusu faragha na data.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Mei 18, 2026 akiwa Geneva nchini Uswisi, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania imeingia katika mazungumzo hayo ikiwa na msimamo wazi wa kuepusha baadhi ya mijadala iliyoibuka katika mikataba kama hiyo kwenye  nchi nyingine za Afrika.

Mchengerwa amesema mkataba huo ni kama mikataba mingine ya Afrika, “Lakini huu wa kwetu ni bora na wa mfano Afrika kwani umezingatia masilahi ya Taifa kwanza.”

Alipoulizwa kwa nini wa mfano, Mchengerwa amesema umezingatia masilahi ya pande zote mbili pasipo nchi moja kunufaika zaidi ya nyingine.

Amesema miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa na mijadala katika nchi zingine ametolea mfano kama masuala ya madini na kubadilishana taarifa.    “Sisi kama nchi, tuliweka msimamo katika mambo haya na tumeyaweka pembeni.”

“Ni kutokana na msimamo huo wa Tanzania, ndiyo maana Washington wametuma mwakilishi ambaye ni mtu wa karibu kabisa na Rais Trump kuja hapa Geneva kuzungumza na mimi na niwahakikishie Watanzania tutalinda na kusimamia masilahi yetu,” amesisitiza Mchengerwa.

Alipoulizwa manufaa ya mkataba huo utakapoanza, Mchengerwa amesema unakwenda kuwanufaisha wananchi moja kwa moja kwenye nyanja mbalimbali za afya kama ujenzi wa viwanda, bima ya afya kwa wote, malaria, maabara pamoja na miradi ya Pepfar ya mapambano ya VVU/Ukimwi.

“Mkataba huu unakwenda kumgusa Mwananchi wa kawaida kabisa pindi utakapoanza na sisi tuko makini kama nilivyosema kulinda maslahi yetu,” amesema Mchenegrwa.

Kuhusu mkataba

Pendekezo la mkataba huo wa afya kati ya nchi hizo mbili, ambao mazungumzo yake yalianza Dar es Salaam wiki iliyopita kabla ya kuendelea Geneva Mei 18, unatarajiwa kuimarisha ushirikiano katika ufadhili wa huduma za afya, bima ya afya kwa wote, uzalishaji wa ndani wa vifaatiba na kinga dhidi ya magonjwa.

Mazungumzo ya karibuni Geneva yaliwahusisha Mchengerwa pamoja na Brad Smith, ambaye ni Mshauri wa Global Health na Mshauri Mwandamizi katika Kitengo cha Global Health Security and Diplomacy cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Tanzania, pande hizo mbili zimekubaliana kuharakisha mazungumzo kuhusu pendekezo la mkataba wa ushirikiano wa afya wa pande mbili unaolenga kuwa mfano wa ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote barani Afrika.

Moja ya maeneo muhimu yanayojadiliwa ni utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 nchini Tanzania, ambayo inalenga kupunguza gharama za matibabu zinazolipwa moja kwa moja na wananchi pamoja na kupanua upatikanaji wa huduma za afya nchini kote.

Mazungumzo hayo yanafanyika wakati baadhi ya nchi za Afrika zimeonyesha wasiwasi kuhusu mikataba mingine ya afya inayoungwa mkono na Marekani chini ya sera mpya ya “America First” katika ufadhili wa afya duniani.

Nchini Ghana, mamlaka zilipinga pendekezo la mkataba wa afya na Marekani baada ya kuibuka hofu kuhusu faragha ya taarifa na upatikanaji wa taarifa nyeti za afya za taifa.

Zimbabwe nayo ilikataa mkataba mwingine wa afya wa Marekani wenye thamani ya dola milioni 367 mapema mwaka huu baada ya kuibuka wasiwasi kuhusu upatikanaji wa sampuli za kibailojia na taarifa nyeti za afya.

Rais Emmerson Mnangagwa anaripotiwa kuuelezea mkataba huo kuwa hauna usawa.

Nchini Zambia, mazungumzo kuhusu makubaliano tofauti ya ufadhili wa afya yalikwama baada ya kuibuka wasiwasi kuhusu masharti ya kushirikishana taarifa, wajibu wa kifedha na madai kwamba msaada wa afya ulihusishwa na ushirikiano wa madini muhimu kama shaba na cobalt.

Ingawa Washington ilikanusha kuhusisha misaada ya afya na upatikanaji wa madini, maofisa wa Zambia walisisitiza baadhi ya masharti yalikuwa kinyume na masilahi ya taifa na mamlaka ya nchi.

‘Tanzania iwe makini’

Mwanasheria wa haki za uzazi nchini Tanzania, Martha Serengi, amesema matukio yaliyotokea katika nchi nyingine za Afrika yanaonyesha umuhimu wa Tanzania kuwa makini katika mazungumzo hayo.

“Katika kipindi hiki, Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea zinafanya kazi katika mazingira yenye ushindani mkubwa wa kisiasa na kiuchumi, ambapo nchi washirika zinatumia mikakati madhubuti kuchukua faida ya changamoto za kiuchumi ili kuongeza manufaa yao wenyewe,” amesema.

Serengi amesema Serikali lazima ihakikishe kuwa mikataba inayosainiwa katika sekta nyeti kama afya inaweka mbele ustawi wa wananchi na manufaa ya muda mrefu ya taifa.

“Serikali lazima iwe makini kuhakikisha kuwa mikataba wanayosaini inanufaisha zaidi wananchi wa Tanzania,” alisema.

Pia alitaka kuwepo uwazi mkubwa zaidi na wananchi kufahamishwa kinachoendelea wakati wa mazungumzo na utekelezaji wa makubaliano hayo.

Zaidi ya hayo, Wakili wa kujitegemea Peter Majanjala ameitaka Serikali kuweka hadharani maudhui ya makubaliano hayo yanayopendekezwa ili wananchi waelewe manufaa yake pamoja na hatari zinazoweza kujitokeza kabla ya kuanza kutekelezwa.

Walichokisema madaktari

Wakati huohuo, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, ameyapokea kwa matumaini makubaliano hayo yaliyopendekezwa, akisema Tanzania na Marekani zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya afya.

“Kama viongozi katika sekta ya afya, tunaona hili kuwa ni fursa muhimu ikiwa litatekelezwa ipasavyo kwa sababu linaweza kuimarisha huduma za afya na kusaidia maendeleo ya viwanda nchini,” amesema.

Naye Mshauri na mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema, “Huu mkataba una mambo mengi ndani yake ikiwemo afya, kuhusu afya tunaelewa inafuatilia magonjwa mbalimbali lakini pia wanaangalia suala la data, wanatoa fedha nyingi lakini lazima ufanye nao biashara, lazima tuwe makini.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *