Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imepangwa katika kundi L la kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zitakazofanyika hapa nchini kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Mabingwa mara tatu wa AFCON, Nigeria ipo katika kundi hilo ambalo linajumuisha pia washindi wa pili wa fainali za CHAN 2024, Madagascar na Guinea Bissau.
Taifa Stars mwaka jana mwishoni ilikutana na Nigeria katika mechi ya hatua ya makundi ya fainali za AFCON 2025 zilizochezwa Morocco na kupoteza kwa bao 1-0.
Hata hivyo, Taifa Stars hata isipofanya vizuri katika mechi za kufuzu, tayari ina uhakika wa kucheza AFCON mwakani kwa vile ni timu ya nchi mwenyeji.
Wenyeji wenza wa AFCON 2027, Kenya wao wamepangwa katika kundi D la mashindano hayo ya kufuzu.
Kundi hilo D mbali na Kenya pia lina timu za Afrika Kusini, Guinea na Eritrea.
Uganda ambayo pia ni miongoni mwa waandaaji wa Fainali za AFCON 2027, wao katika mashindano ya kufuzu wamepangwa katika kundi H likiwa na timu za Tunisia, Libya na Botswana.
Mabingwa watetezi wa AFCON, Morocco wao wameangukia katika kundi A ambalo pia linajumuisha timu za Gabon, Niger na Lesotho.
