
Katika ripoti ya tarehe 19 Mei 2026, shirika hilo limesema kuwa licha ya uchumi wa dunia kuingia mwaka 2026 ukiwa na uimara uliotokana na biashara ya kimataifa, uzalishaji wa viwandani katika nchi zinazoendelea na uwekezaji mkubwa katika teknolojia ya akili mnemba (AI), hali ya kisiasa duniani imeanza kudhoofisha kasi hiyo ya ukuaji.
Migogoro ya kisiasa yaongeza shinikizo kwa uchumi wa dunia
Kwa mujibu wa UNCTAD, migogoro ya kisiasa na kijeshi duniani, hususan vita vya Ukraine pamoja na kuongezeka kwa mapigano Mashariki ya Kati, imeongeza bei za mafuta, gharama za usafirishaji na kuyumba kwa masoko ya fedha duniani.
Shirika hilo limeeleza kuwa hali hiyo imeongeza mashaka kwa wawekezaji na kuathiri biashara ya kimataifa pamoja na ukuaji wa uchumi katika mataifa mengi. UNCTAD inakadiria kuwa ukuaji wa uchumi wa dunia utashuka kutoka asilimia 2.9 mwaka 2025 hadi asilimia 2.6 mwaka 2026 kutokana na kupungua kwa uwekezaji na kushuka kwa mahitaji ya bidhaa katika masoko mbalimbali.
Ripoti hiyo imeonya kuwa hali hiyo inaweza kuongeza changamoto za ajira, biashara na maendeleo ya kiuchumi katika nchi nyingi duniani.
Nchi zinazoendelea zatajwa kuathirika zaidi
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi zinazoendelea ndizo zinazoathirika zaidi kutokana na kuongezeka kwa gharama za mafuta, chakula na mbolea.
Aidha, nchi hizo zinakabiliwa na kushuka kwa thamani ya sarafu zao pamoja na ugumu wa kupata mikopo katika masoko ya fedha duniani.
UNCTAD imesema hali hiyo inaweza kuongeza umasikini na changamoto za maisha kwa wananchi katika mataifa mengi yanayoendelea.
Ukuaji wa biashara duniani wachochewa na teknolojia ya Akili mnemba (AI)
Ingawa biashara ya dunia iliendelea kuimarika mwanzoni mwa mwaka 2026, shirika hilo limeeleza kuwa ukuaji mkubwa umetokana zaidi na bidhaa zinazohusiana na teknolojia ya akili mnemba (AI).
Bidhaa hizo ni pamoja na vipitisha umeme, seva na vifaa vya usindikaji data ambavyo vimeongezeka mahitaji yake duniani kutokana na kasi ya matumizi ya teknolojia ya AI.
Hata hivyo, sekta nyingine za kawaida zimeonesha ukuaji mdogo ikilinganishwa na sekta ya teknolojia.
Uhakika wa kupata chakula waendelea kuwa changamoto
UNCTAD pia imeonya kuwa uhakika wa kupata chakula umeanza kuwa tatizo kubwa la kifedha duniani kutokana na kupanda kwa bei za nishati na mbolea pamoja na changamoto katika mifumo ya biashara ya chakula duniani.
Shirika hilo limesema hali hiyo inaweza kuongeza uhaba wa chakula na gharama za maisha katika baadhi ya mataifa ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Mapendekezo ya kukabiliana na changamoto
Katika kupunguza athari hizo siku zijazo, UNCTAD imezitaka nchi duniani kuongeza ushirikiano wa kimataifa na kuhakikisha biashara ya dunia inabaki kuwa yenye utulivu.
Shirika hilo pia limependekeza:
· Kuimarisha mifumo ya kifedha duniani
· Kuongeza ushirikiano wa biashara kati ya mataifa
· Kuwekeza haraka katika nishati safi na nafuu
· Kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa kupata chakula duniani
· Kupunguza vikwazo vinavyoathiri biashara ya kimataifa
Wito wa hatua za pamoja
UNCTAD imehitimisha kwa kusisitiza kuwa hatua za pamoja za kimataifa zinahitajika ili kulinda uchumi wa dunia dhidi ya misukosuko ya kisiasa, kifedha na biashara.
Shirika hilo limeonya kuwa bila hatua za haraka, changamoto hizo zinaweza kuathiri zaidi ukuaji wa uchumi, biashara na maisha ya wananchi duniani.
