Sababu mbili… Aziz KI kurudi JangwaniSababu mbili… Aziz KI kurudi Jangwani

WAKATI wowote usishangae wala kushtuka kumwona kiungo Aziz KI akirejea nchini na kujiunga na Yanga, kwani pande hizo mbili bado zinahitajiana na kuna ishu kati yao inaendelea chinichini.

Kabla ya kuondoka Yanga, Aziz KI alikuwa staa muhimu wa kikosi hicho akichukua mataji tisa yakiwamo mawili ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB (2), Ngao ya Jamii (2), Kombe la Muungano (1), Kombe la Toyota (1) na Kombe la Mapinduzi (1). Pia akabeba tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara na mchezaji bora wa ligi hiyo msimu wa 2023-2024.

Msimu wa 2023-2024, Aziz KI aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu akiitumikia Yanga ambapo alifanikiwa kufunga mabao 21 yakiwa ni mawili mbele ya mshindani wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Msimu wa 2025-2026, staa huyo aliachana na kikosi hicho na kujiunga Wydad Athletic ya Morocco kwenye usajili ambao uliifanya Yanga kuingiza kitita kikubwa cha fedha Sh755 milioni, lakini huko hakufanikiwa kufanya makubwa ambapo alifunga mabao mawili kwenye michezo 13 aliyopata nafasi ya kucheza.

Staa huyo raia wa Burkina Faso, alidumu kwenye timu hiyo kwa miezi minane akiwa hana nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza, hata hivyo, mapema mwaka huu aliuzwa kwenda kikosi cha matajiri wa Al Ittihad ya Libya.

Iliripotiwa kuwa Al Ittihad ilifanikiwa kulipa kitita cha dola 300,000 (Sh780 milioni za Tanzania) ili kuipata saini ya kiungo huyo mshambuliaji mwenye uwezo wa juu wa kupiga mipira ya faulo.

Taarifa za ndani kutoka Yanga zililiambia Mwanaspoti kuwa, Aziz KI, anafikiria kurejea Tanzania kufanya mazungumzo na Yanga ili ajiunge tena na timu hiyo ambayo ilimpa umaarufu mkubwa.

Hata hivyo, mambo mawili yanatajwa kuwa sababu kuu ya kiungo huyo kurudi Yanga, moja ikiwa ni usalama nchini Libya na nyingine ni kuungana na mkewe Mwanamitindo Hamisa Mobetto ambaye kwa sasa yupo hapa nchini akiendelea na biashara zake.

“Aziz KI anataka kurudi Yanga, kuna mambo yanaendelea chinichini, bado ana mkataba na timu yake kwa kuwa Januari ndiyo alijiunga nayo na kusaini miaka miwili.

“Tunaweza kuwa na timu imara msimu ujao, kuna wachezaji wazuri wanataka kuja hapa kwetu. Aziz KI hafurahii maisha ya kule Libya, tunalifikiria hili pia,” kilisema chanzo kutoka Yanga. Mei 14, 2026, wakati mchezo wa Ligi Kuu ya Libya ukiendelea kati ya Al Ittihad dhidi ya Al Swahli, ilisikika milio ya risasi pembeni ya uwanja na kulazimika mechi hiyo kusimama kwa muda jambo ambalo liliwashtua baadhi ya wachezaji wageni kwenye kikosi hicho.

Ikumbukwe kuwa, Februari 16, 2025, Aziz Ki alifunga ndoa na mwanamitindo Mobeto jijini Dar es Salaam, lakini staa huyo amekuwa akifanya biashara zake hapa jijini Dar es Salaam na amekuwa akienda Libya mara chache kuungana na mume wake.

“Ukiacha hilo kuna suala la familia yake, unakumbuka Aziz ameoa hapa, amekuwa mbali na familia yake, hili linamtesa, anaona ni bora arejee hapa kuwa karibu na mke wake.”

Hata hivyo, chanzo hicho kinasema kuwa Yanga inapambana kuhakikisha inampata mchezaji huyo kwa mkopo wa msimu mmoja na baadaye kufanya uwezekano wa kumsajili moja kwa moja kutoka na hofu ya gharama kubwa ambazo wanaweza kupewa na Al Ittihad, au kumsubiri hadi mkataba wake umalizike mwakani wamchukue jumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *