Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga MheMkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita Mei.18.2026 amefungua rasmi mafunzo ya utoaji wa elimu ya uraia, utawala bora pamoja na ulinzi na usimamizi wa mali na rasilimali asilia za nchi yanayotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa serikali mkoani humo.

Mafunzo hayo yanawakutanisha Kamati za Usalama nchini, Sekretarieti za Mkoa, Menejimenti za Halmashauri, Maafisa Madini, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata pamoja na Watendaji wa Vijiji na Mitaa kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya sheria, utawala bora na usimamizi wa rasilimali za taifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Mhita amesema serikali inaendelea kuweka mkazo katika utoaji wa elimu ya sheria na uraia ili kuwajengea uwezo viongozi na watendaji katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, uwajibikaji na maslahi ya wananchi.

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuimarisha utawala bora pamoja na kuhakikisha mali na rasilimali asilia za nchi zinalindwa na kusimamiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Tunahitaji viongozi na watendaji wenye uelewa wa kutosha kuhusu sheria na misingi ya utawala bora ili kuongeza uwajibikaji na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema Mhita.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Katiba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ambaye pia ni Wakili wa Serikali, Prosper Kisinini, amesema timu ya wataalamu wa serikali inayotekeleza mpango huo inalenga kuwafikia viongozi na watendaji katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza uelewa kuhusu masuala ya sheria, uraia na usimamizi wa rasilimali za taifa.

Amesema kupitia mafunzo hayo, washiriki wanapatiwa elimu kuhusu wajibu wao katika kulinda mali za umma, kuzuia matumizi mabaya ya rasilimali asilia pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wananchi katika kusimamia maendeleo ya taifa.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *