
Dar es Salaam. Mganga wa kienyeji, Said Mkomwa (31), Saidini, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam akikabiliwa na shtaka moja la mauaji.
Mkomwa ambaye ni mkazi wa Kitunda, anadaiwa kumuua James Temba (24) aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).
Mshtakiwa huyo amesomewa shtaka lake jana Jumanne Mei 19, 2026 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edith Mauya akishirikiana na wakili wa Serikali Judith Kyamba, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Herieth Mwailolo.
Hata hivyo, kabla ya kusomewa shtaka lake, Hakimu Mwailolo alimueleza mshtakiwa huyo kuwa hatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa sababu Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji isipokuwa Mahakama Kuu pekee.
Pia, shtaka la mauaji linalomkabili mshtakiwa halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo atapelekwa rumande hadi upelelezi utakapokamilika.
Hakimu Mwailolo, baada ya kutoa maelezo hayo, upande wa Jamhuri ulimsomea Mkomwa shtaka lake.
Akimsomea shtaka hilo, wakili Mauya alidai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa la mauaji, kinyume na kifungu 196 na kifungu 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Wakili Mauya alisema mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya mauaji (PI) namba 10927 ya mwaka 2026.
Akimsomea shtaka lake alisema, Mkomwa anadaiwa Aprili 29, 2026 katika Mto Msimbazi, eneo la Karakata lililopo Kata ya Kipawa, wilaya ya Ilala, ulimuua James Temba.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, upande wa mashtaka ulidai kuwa kupelekwa kesi hiyo haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 2, 2026 kwa kutajwa na mshtakiwa amepelekwa rumande kwa kuwa shtaka la mauaji halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Itakumbukwa Aprili 30, 2026 mwili wa Temba ulionekana ukielea katika Mto Msimbazi eneo la Kipawa huku ukiwa haina kichwa.
Hata hivyo, Mei 13, 2026 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kichwa cha Temba kimepatikana eneo la Kitunda Kibeberu kukiwa kimefukiwa ardhini.
