
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya Watanzania wanatumia intaneti kupitia laini za simu zaidi ya milioni 90 zilizosajiliwa hadi Desemba mwaka jana.
Hali hiyo inaonyesha namna sekta ya mawasiliano ilivyo kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini kwa kupanua fursa za biashara, hasa kwa biashara ndogo na za kati zinazoweza kuwafikia wateja wengi zaidi kupitia simu na intaneti.
Aidha, mifumo ya miamala ya simu imeendelea kurahisisha malipo, akiba na mikopo bila wananchi kulazimika kwenda benki, jambo lililosaidia hata wananchi wa vijijini kuingia kwenye uchumi rasmi na jumuishi.
Mbali na huduma za kifedha, sekta ya mawasiliano imeendelea kuchochea ukuaji wa kilimo, utalii na biashara za kidijitali.
Wakulima sasa wanapata taarifa za bei za mazao, hali ya hewa na mbinu bora za kilimo kupitia simu zao, huku sekta ya utalii ikinufaika na urahisi wa mawasiliano, uwekaji wa oda za malazi na malipo ya huduma kwa njia ya kidijitali.
Kadhalika, vijana wengi wamejiajiri kupitia biashara za mtandaoni na utayarishaji wa maudhui ya kidijitali, wakati uwekezaji katika minara ya mawasiliano na miundombinu ya fiber optic ukiendelea kuongeza ajira, mapato ya Serikali na kurahisisha biashara pamoja na mawasiliano kati ya Tanzania na nchi jirani.
Akizungumza maendeleo ya mawasiliano nchini Ofisa Mkuu wa Teknolojia na Ufundi wa Yas Tanzania, Emmanuel Malya, alisema kutokana na umuhimu wa mtandao kampuni ya Mawasiliano ya Yas Tanzania hivi karibuni ilizindua kampeni ya zingatia Mtandao wa Viwango ili kuimarisha mawasiliano na kukidhi mahitaji ya Watanzania.
“Baada ya maboresho hayo yaliyoweka msingi thabiti wa huduma zetu, tuna zaidi ya minara 4,800, ambayo ni takribani minara 1,000 zaidi kuliko mtoa huduma yeyote wa mawasiliano nchini. Hivi sasa tunawafikia asilimia 95 ya Watanzania mijini na vijijini,” alisema Malya.
Alisema kampuni yao imefanya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Sh1 trilioni katika upanuzi na maboresho ya miundombinu ya mawasiliano nchini na mbali na ongezeko la minara, imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya fiber optic, kuboresha teknolojia kutoka 2G hadi 4G, sambamba na kuanzisha huduma za 5G katika miji ya kimkakati.
Kuhusu faida za huduma bora za mtandao Emmanuel Simon Mtafya, mfanyabiashara wa mbao katika Soko la Mbao Buguruni, anasema upatikanaji wa huduma bora za intaneti umeongeza ufanisi mkubwa katika biashara yake.
“Awali nilipokuwa naenda Mufindi kufuata mbao, nililazimika kwenda na pesa taslimu kwa sababu maeneo mengi ya vijijini hayakuwa na huduma nzuri za mawasiliano. Ilikuwa vigumu hata kupatikana kwa simu,” alisema na kuongeza kuwa sasa hata miamala inafanyika kwa urahisi.
Ukiachana na Mtafya wafanyabiashara wengine wanasema huduma za intaneti zenye ubora zinasaidia kata katika kutangaza biashara zao na kufanya mawasiliano na wateja kwa urahisi.
Aidha kutokana na maendeleo ya upatikanaji wa mtandao, mbali na kuwanuafaisha wakulima katika sekta ya elimu mtandao umetoa fursa za kujifunza mtandaoni na mawasiliano rahisi kati ya shule, walimu na wazazi.
Katika sekta ya afya, huduma za mawasiliano zimeongeza urahisi wa upatikanaji wa ushauri wa kitabibu na kuimarisha mawasiliano kati ya wataalamu wa afya na wananchi, hali inayodhihirisha namna teknolojia ya mawasiliano inavyoendelea kugusa maisha ya Watanzania katika nyanja mbalimbali.