
Majadiliano yamejikita katika swali la nani atatawala Gaza na kwa namna gani, wakati kukiwa hakuna dalili za kuondolewa kwa silaha na juhudi za ujenzi mpya zikikabiliwa na changamoto kubwa.
“Hali ya eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel inazidi kuwa tete,” amesema Ramiz Alakbarov, Naibu Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mashariki ya Kati.
Ameonya kuwa katika Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Jerusalem Mashariki, ongezeko la makazi ya walowezi, vurugu na uchochezi vinaendelea kuchochea mivutano.
Gaza kwenyewe, kuchelewa kutekelezwa kwa Azimio 2803 (2025), ghasia za kila siku na mgogoro wa kibinadamu vimefuta matumaini ya awali yaliyotokana na usitishaji vita.
“Watu wa Gaza hawawezi kustahimili vita zaidi,” amesisitiza. “Hali hii lazima iepukwe kwa gharama yoyote.”
UN: Tekelezeni Azimio 2803 (2025) bila kuchelewa
Alakbarov amesisitiza kuwa Azimio 2803 (2025) haliwezi kusubiri. Mpango wa kina wa kumaliza mzozo wa Gaza lazima utekelezwe kikamilifu, ikiwa ni pamoja na:
- Kupokonywa kwa silaha za Hamas na makundi mengine yenye silaha
- Kujiondoa kwa vikosi vya Israel
- Kupelekwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Uimarishaji
- Kuwezesha Kamati ya Kitaifa ya Utawala wa Gaza
Ameonya kuwa mashambulizi ya Israel yanaendelea karibu kila siku, yakisababisha vifo vya makumi ya raia, sambamba na shughuli za kijeshi za Hamas na makundi mengine.
Kwa mujibu wa duru za habari, Israel sasa inadhibiti takriban asilimia 60 ya Gaza.
Hali ya kibinadamu Gaza: vizuizi, ukosefu wa fedha na njaa kali
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameonya kuwa operesheni za kibinadamu Gaza zimezidi kuzuiwa na uhaba wa fedha, vizuizi vya usafiri na miundombinu iliyoharibiwa.
Mpango wa haraka wa misaada kwa 2026 umefadhiliwa kwa asilimia 12 pekee, huku misafara ya misaada ikikabiliwa na ucheleweshaji na vikwazo vya mafuta na vifaa muhimu.
Upungufu wa chakula unaendelea kuwa mkubwa, ambapo sasa washirika wa misaada wanatoa takriban milo milioni 1 kwa siku, ikishuka kutoka milioni 1.8 mwezi Februari.
Ripoti zinaonesha kuwa familia moja kati ya tano hula mara moja tu kwa siku, huku akina mama wengi wakijinyima chakula ili watoto wapate kula.
Usitishaji vita ndio msingi wa ujenzi upya: Baraza la Amani
Nickolay Mladenov, Mwakilishi Mkuu wa Gaza katika Baraza la Amani, amesema baadhi ya maendeleo yameonekana baada ya usitishaji vita.
“Silaha zimepungua kwa kiasi kikubwa kunyamaza kwa mara ya kwanza katika miaka miwili,” amesema.
Amebainisha kuwa usaidizi wa chakula umeongezeka na njaa imepungua kiasi, huku watu wanaopata msaada wakiongezeka kutoka 400,000 hadi takriban milioni 2.
Hata hivyo, amekiri kuwa hali bado si ya kuridhisha kutokana na ukiukaji wa mara kwa mara wa usitishaji vita na vizuizi vya misaada.
“Hakuna chaguo la tatu”: wito wa kidiplomasia kuendelea
Mladenov amesema ramani ya utekelezaji wa mpango wa vipengele 20 ni ya kuaminika na inapaswa kuungwa mkono kikamilifu na Baraza la Usalama.
Amesisitiza kuwa:
- Mabadiliko na uondoaji wa silaha ni muhimu
- Israel na Hamas lazima waheshimu makubaliano ya usitishaji vita
- Diplomasia lazima iendelee bila kukoma
“Kuna machaguo mawili tu, hali inayoendelea kuzorota au mwanzo mpya. Hakuna chaguo la tatu,” amesema.
Mgogoro wa makazi Gaza: maelfu bado wamelazimika kuhama
Takriban asilimia 80 ya majengo Gaza yameharibiwa au kubomoka, huku karibu watu wote milioni 2.1 wakiwa wamekimbia makazi yao.
Takriban watu 900,000 wanahitaji makazi ya dharura, huku mashirika ya misaada yakijaribu kuanzisha makazi ya muda na miundombinu ya afya inayoweza kutumika kwa shule na kliniki.
Sekta ya afya pia iko chini ya shinikizo kubwa, huku wagonjwa wengi wakihitaji matibabu ya haraka nje ya Gaza.
Serikali na mashirika ya misaada wanaendelea kuhimiza kuongezwa kwa vifaa vya tiba na upatikanaji wa huduma muhimu.
