Kwa miaka 50 wanawake wamekuwa wengi zaidi miongoni mwa vifo vya EbolaKwa miaka 50 wanawake wamekuwa wengi zaidi miongoni mwa vifo vya Ebola

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Mei 22 katika Ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa UN Women, Sofia Calltorp, amesema historia imeonesha mara kwa mara kwamba wanawake hubeba mzigo mkubwa zaidi wakati wa milipuko ya Ebola.

Katika mlipuko wa Ebola wa mwaka 2018–2019 nchini DRC, wanawake na wasichana walichangia takriban theluthi mbili ya wagonjwa wote walioripotiwa. Nchini Liberia mwaka 2014, wanawake walikuwa hadi robo tatu ya vifo vya Ebola katika baadhi ya jamii, huku miaka 50 iliyopita nchini DRC wakichangia asilimia 56 ya waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Sababu?

Calltorp amesema hali hiyo haitokani na Ebola kuwa hatari zaidi kwa wanawake wanapoambukizwa, bali ni kwa sababu maambukizi ya ugonjwa huo yanafuata uhalisia wa majukumu ya kijamii. Wanawake wana uwezekano mkubwa zaidi wa kufariki kutokana na Ebola kuliko wanaume kwa sababu wako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa ugonjwa huo, inasema UN Women kwa kutumia uzoefu wa nyuma.

“Virusi hivi huenea kupitia njia zinazohusiana na utoaji wa huduma kwa wagonjwa, kazi za nyumbani, kazi za afya zilizo mstari wa mbele, pamoja na taratibu za mazishi,” amesema.

© WHO Vifaa vya tiba na msaada muhimu zimefikishwa Bunia DRC ili kuimarisha hatua dhidi ya mlipuko wa Ebola huko Ituri.

Kwa mujibu wa UN Women, wanawake mara nyingi ndiyo walezi wakuu wa ndugu wagonjwa, watoto na wazee katika familia. Pia wanawakilisha sehemu kubwa ya wauguzi, wahudumu wa usafi na wakunga katika vituo vya afya, jambo linalowaweka katika mawasiliano ya karibu na wagonjwa wakati wa hatua hatari zaidi za maambukizi.

Wanawake pia mara nyingi huwa na jukumu la kuandaa miili ya wapendwa wao kwa ajili ya mazishi, hali inayoongeza hatari ya kuambukizwa virusi hivyo.

Wanawake wajawazito wanakabiliwa na hatari zaidi kutokana na mawasiliano yao ya mara kwa mara na huduma za afya. Taarifa za kihistoria zinaonesha kuwa maambukizi ya Ebola wakati wa ujauzito yanahusishwa na ongezeko la vifo na madhara ya kiafya kwa mama, pamoja na karibu asilimia 100 ya matokeo mabaya ya ujauzito.

UN Women pia imeonya kuwa wanawake na wasichana hukabiliwa na hatari kubwa zaidi ya ukatili wa kijinsia wakati wa dharura za kiafya, hasa jamii zinapowekwa kwenye karantini.

Wasiwasi wa UN Women

Shirika hilo limeeleza wasiwasi wake kwamba kupunguzwa kwa ufadhili wa shughuli za kibinadamu kunadhoofisha mifumo ya afya na ulinzi iliyo mstari wa mbele katika kipindi muhimu kama hiki, na limetoa wito wa kuwepo kwa ufadhili endelevu na unaobadilika kulingana na mahitaji kwa mashirika yanayoongozwa na wanawake.

“Mashirika haya yanaendelea kufanya kazi za kuokoa maisha kwa kulinda jamii, kupambana na taarifa potofu na kuhimiza mbinu salama za utoaji wa huduma,” amesema Calltorp.

Nini kifanyike?

UN Women pia inataka uwekezaji mkubwa zaidi katika programu za huduma za msingi za afya zinazokidhi mahitaji ya wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa kinga binafsi, vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi, pamoja na mafunzo ya uelimishaji na kinga dhidi ya Ebola katika jamii.

Shirika hilo linasisitiza kuwa wanawake wanapaswa kushiriki kikamilifu katika uamuzi na utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mlipuko huo, huku likibainisha kuwa takwimu zinazogawanywa kwa jinsia, umri na hali ya ulemavu ni muhimu ili kuboresha mipango ya hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.

UN Women imesema inaendelea kufanya kazi katika nchi zilizoathiriwa na Ebola kwa kushirikiana na serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya wanawake ili kusaidia juhudi za kuzuia maambukizi na kuimarisha hatua za kupona, huku ikihakikisha wanawake wanashiriki katika mchakato wa kufanya maamuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *