Washiriki WUF13: Tanzania imejipanga kuhakikisha wananchi wake wanakabili changamoto ya nyumbaWashiriki WUF13: Tanzania imejipanga kuhakikisha wananchi wake wanakabili changamoto ya nyumba

Wakizungumza na Nargis Shekinsky wa UN News kandoni mwa jukwaa hilo washiriki hao umetumia nafasi hiyo kueleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na seikali na wadau wengine kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora, huduma muhimu na miundombinu inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Tanzania yashiriki kubadilishana uzoefu -Rehema

Rehema Kishoa kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Tanzania amesema Tanzania imehudhuria mkutano huo ikiwa na ujumbe mkubwa kwa lengo la kushirikishana uzoefu kuhusu namna nchi inavyoboreshwa sekta ya makazi na huduma za jamii.

“Tumekuja kushirikiana uzoefu wa nini Tanzania inafanya katika kuhakikisha tunakuwa na nyumba, lakini pia miundombinu katika maeneo ambayo huduma za makazi na huduma nyingine zinapatikana,” amesema Rehema.

World Bank/Hendri Lombard Huduma za usafiri wa mwendokasi jijini Dar es salaam nchini Tanzania ni miongoni mwa mipango ya miji ya kuimarisha huduma kwa wakazi kadri inavyozidi kukua

Ameeleza kuwa juhudi za Serikali hazilengi tu kujenga nyumba zenye “kuta nne”, bali kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira yanayowajengea utu na kuwapatia huduma muhimu kama afya, elimu na miundombinu ya usafiri inayorahisisha maisha ya kila siku pamoja na kukuza uchumi wao.

Serikali na sekta binafsi zashirikiana kupunguza changamoto ya nyumba

Kwa mujibu wa Rehema, changamoto ya makazi ni ya dunia nzima, lakini Tanzania imeendelea kuweka mikakati mbalimbali kupitia taasisi za Serikali na ushirikiano na sekta binafsi ili kuongeza upatikanaji wa nyumba bora na za gharama nafuu.

Amesema Shirika la Nyumba la Taifa NHC, pamoja na wadau wengine wamekuwa wakijenga nyumba zinazolenga wananchi wote, hasa wenye kipato cha chini.

Dodoma kuwa mfano wa mafanikio ya miradi ya makazi

Akizungumzia mafanikio hayo, Rehema amesema ujenzi mkubwa wa nyumba katika Makao Makuu ya Tanzania Dodoma umesaidia kupunguza changamoto za makazi zilizotokana na kuhamia kwa shughuli za Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

“Bila miradi hii mikubwa ya ujenzi wa nyumba kungekuwa na changamoto kubwa ya makazi kwa watumishi na wananchi waliohamia Dodoma,” amesema.

Ameongeza kuwa miradi hiyo haijawanufaisha watumishi wa serikali pekee, bali pia wananchi wa kawaida waliopata nafasi ya kumiliki au kuishi kwenye nyumba zilizojengwa.

UN News Constantine Yuda -Ushirikiano wa kitaifa wa makazi Tanzania.

Shirika la Nyumba la Taifa lajenga mamia ya nyumba-Yuda

Kwa upande wake, Yuda Constantine kutoka Shirika la Nyumba la Taifa NHC, amesema taasisi hiyo ipo mstari wa mbele kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kwa sasa shirika hilo lina miradi mingi Dar es Salaam na Dodoma, hasa kutokana na ongezeko kubwa la watu wanaohamia makao makuu ya nchi.

“Tunaendelea kujenga nyumba nzuri na bora zinazofaa kwa wananchi wote wanaohamia Dodoma,” amesema Yuda.

Ameeleza kuwa miradi hiyo inajumuisha maendeleo ya makazi katika eneo la Medeli, Iyumbu pamoja na mradi mkubwa wa nyumba Dar es Salaam ambapo zaidi ya nyumba 500 zinaendelea kujengwa.

Mpango wa kuboresha makazi holela

Yuda pia amesema Tanzania inaendelea kutekeleza mipango ya urasimishaji na uboreshaji wa makazi kupitia Wizara ya Ardhi ili kubadilisha maeneo yasiyo rasmi kuwa salama na yenye huduma bora.

Mfano alioutaja ni mradi mkubwa wa maendeleo wa Bonde la Msimbazi jijini Dar es Salaam, eneo ambalo limekuwa likikumbwa na mafuriko mara kwa mara.

Kwa mujibu wake, mpango huo unalenga kufanya eneo hilo kuwa salama zaidi na linalofaa kwa makazi na matumizi mengine ya maendeleo ya miji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *