Gaza: Dawa za kuokoa maisha zazuiwa huku mauaji yakiendelea na magonjwa yakisambaaGaza: Dawa za kuokoa maisha zazuiwa huku mauaji yakiendelea na magonjwa yakisambaa

Akiwa amerejea hivi karibuni kutoka ziara katika eneo hilo lililoharibiwa vibaya, Dkt. Renee Van de Weerdt, mwakilishi wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kuwa, “Hakuna kinachoweza kukuandaa kwa kile unachokiona Gaza.”

“Nilidhani kwenda kwa mara ya pili kungefanya mambo kuwa rahisi zaidi. Lakini sivyo kabisa,” amesema.

Dkt. Van de Weerdt amesisitiza kuwa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas mwezi Oktoba 2025, watu wasiopungua 880 wameuawa katika Ukanda wa Gaza huku zaidi ya 2,600 wakijeruhiwa.

“Kuna huenda moto wa mapigano umepungua, lakini vurugu zinaendelea,” amesema. Tunasikia milipuko ya mabomu karibu nasi. Risasi zinasikika kila siku.”

Nusu ya hospitali zote zinafanya kazi kwa sehemu tu

Mwakilishi huyo wa WHO ameeleza hali mbaya ya afya Gaza, akibainisha kuwa mashambulizi 22 dhidi ya sekta ya afya yameripotiwa mwaka huu pekee na kwamba ni takribani nusu tu ya hospitali zinazofanya kazi “kwa kiwango cha sehemu”, huku hakuna hata hospitali moja inayoweza kusemwa kuwa inafanya kazi kikamilifu.

“Moja ya sababu kuu zinazofanya vituo hivi visiweze kufanya kazi ni uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu,” ameeleza.

Dkt. Van de Weerdt amesema vifaa muhimu na mashine za tiba zimekwama upande mwingine wa mipaka ya Gaza, jambo linaloleta madhara makubwa kwa afya ya wananchi.

“Nchini Jordan kuna hospitali ya muda iliyotengenezwa tayari ambayo imekuwa ikisubiri kwa miezi kadhaa kuruhusiwa kuingia Gaza,” amesema. “Vifaa vya maabara, kemikali za uchunguzi, mitungi ya oksijeni, vifaa vya mifupa, hivi si vitu vya anasa. Hivi ni vifaa muhimu vinavyohitajika ili hospitali na mfumo wa afya ufanye kazi.”

Bila vifaa vya maabara na kemikali za uchunguzi, “hatuwezi kutambua magonjwa wala kugundua milipuko inayoweza kujitokeza,” amesisitiza mwakilishi huyo wa WHO.

Kutoona milipuko ya magonjwa

“Tunazungumzia virusi vya hanta, tunazungumzia virusi vya Ebola. Hivi si vitu vya anasa. Ni vifaa tunavyohitaji kuokoa maisha, kugundua magonjwa, kuutahadharisha ulimwengu kuhusu milipuko inayoweza kutokea na kuhakikisha watu hawafi.”

Amesisitiza kuwa “Unaweza kufikiria hali mbaya ya maisha iliyopo, msongamano mkubwa wa watu, panya, ukosefu wa maji safi na huduma za usafi; vifaa hivi vinahitajika haraka sana”.

Dkt. Van de Weerdt ameeleza kuwa baadhi ya vifaa vinapigwa marufuku chini ya kanuni za Israel kwa kile kinachoitwa vifaa vya “matumizi ya pande mbili”, yaani vinavyodhaniwa kuwa vinaweza kutumika kijeshi.

Hata hivyo amepinga kuhusishwa kwa orodha ya dawa muhimu zinazotambuliwa kimataifa na vikwazo hivyo.

Viungo bandia vyachukuliwa kuwa vya matumizi ya kijeshi

Kwa mfano, viungo bandia vya mwili vinachukuliwa kuwa ni vifaa vya matumizi ya pande mbili. Takribani watu 5,000 waliokatwa viungo huko Gaza wanasubiri si tu kupata viungo bandia bali pia upasuaji maalum wa kurekebisha sehemu za mwili ili viungo hivyo viweze kutumika ipasavyo.

“Kwa sasa upasuaji huo hauwezi kufanyika Gaza,” alisema. “Kwa hiyo watu hawa wenye mateso makubwa wanalazimika kusubiri kwenye orodha ya kuondoka.”

WHO imekuwa ikisaidia mamlaka za afya kuratibu uhamishaji wa wagonjwa kwa matibabu nje ya Gaza kwenda zaidi ya nchi 30.

Tangu kufunguliwa tena kwa mpaka wa Rafah mwezi Februari, kivuko hicho kimekuwa njia muhimu kwa wagonjwa kutoka Gaza kuelekea Misri, amesema Dkt. Van de Weerdt. Aidha kupitia kivuko cha Kerem Shalom ambacho kinaweza kutumika mara moja tu kwa wiki, “wagonjwa wanaweza kupita katika njia ndefu na ngumu kuelekea Jordan.”

Mwakilishi huyo wa WHO amesema kuna changamoto kubwa sana kwa wagonjwa na familia zao wakati wa uhamishaji wa matibabu.

“Mara nyingi ni mwanafamilia mmoja au wawili tu wanaoruhusiwa kuondoka na mazingira ya kurejea si ya uhakika kila wakati,” amesema.

“Tunaendelea kusisitiza umuhimu wa wagonjwa wenye hali maalum kuhamishwa kwa matibabu. Lakini pia tunataka kuhakikisha kuwa maelfu kwa maelfu ya watu wanaohitaji huduma maalum Gaza leo wanaweza kutibiwa ndani ya Gaza yenyewe.”

UNRWA haina mbadala

Mtoa huduma mkubwa wa afya Gaza ni Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, ingawa marufuku zilizowekwa na Bunge la Israel dhidi ya shughuli zake zimezidisha ugumu wa operesheni zake.

Mkurugenzi wa Afya wa UNRWA Dkt. Akihiro Seita amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa mwaka jana shirika hilo lilitoa huduma za ushauri wa kitabibu milioni 4.5 huko Gaza, sawa na asilimia 40 ya huduma zote za matibabu zilizotolewa.

Dkt. Van de Weerdt wa WHO amesisitiza kuwa, “Hakuna anayeweza kuchukua nafasi ya kile UNRWA inachokifanya.”

Dkt. Seita amelalamikia ukweli kwamba “kutokana na sheria za Bunge la Israel dhidi ya UNRWA”, shirika hilo haliwezi kuingiza dawa Gaza na Ukingo wa Magharibi, na pia lilipoteza vituo vyake viwili vya afya Mashariki mwa Jerusalem mapema mwaka huu ambavyo vilikuwa vikihudumia wagonjwa 11,000 kila mwaka.

Afisa huyo wa UNRWA amekumbusha kuwa karibu wafanyakazi 400 wa shirika hilo waliuawa katika vita vya Gaza. Maelfu wengine wanaendelea kuwasaidia wakazi wa Gaza huku wakikabiliwa na hali mbaya sana.

“Wafanyakazi wetu wengi bado wanaishi kwenye mahema,” alisema. “Mmoja wao ameniambia jambo ambalo sitalisahau kamwe… ‘Ninahisi kama nimekuwa yatima wa dunia. Hakuna anayetujali tena. Wametusahau.’”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *