Baraza la Famasi lasitisha utambuzi wahitimu kozi ya mwaka mmojaBaraza la Famasi lasitisha utambuzi wahitimu kozi ya mwaka mmoja

Dar es Salaam. Baraza la Famasi limetangaza rasmi kusitisha utambuzi wa wahitimu wa kozi ya mwaka mmoja ya utoaji dawa maarufu kama One-Year Pharmaceutical Dispensers, hatua itakayoanza kutekelezwa kuanzia Desemba Mosi, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 22, 2026 na Msajili wa Baraza la Famasi imeeleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha 57 cha Baraza kilichofanyika Agosti 19 hadi 20, 2025, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya taaluma ya famasi na kuongeza ubora wa huduma za afya nchini.

Baraza la Famasi ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya, yenye jukumu la kusajili wataalamu wa famasi, kusimamia maadili yao pamoja na kuhakikisha wanatoa huduma kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wahitimu wa kozi ya mwaka mmoja wataendelea kuruhusiwa kufanya mitihani ya usajili na taaluma hadi Novemba 2026. Baada ya muda huo, mitihani hiyo itasitishwa rasmi kwa kundi hilo.

Baraza limefafanua kuwa wahitimu ambao hawatakuwa wamefaulu mitihani hiyo ndani ya muda uliotolewa watalazimika kuendelea na masomo hadi kufikia angalau ngazi ya astashahada (certificate) au zaidi ili waweze kutambuliwa na kusajiliwa.

Aidha, watoa dawa ambao tayari wametambuliwa na Baraza wataendelea kufanya kazi kama kawaida chini ya usimamizi wa Baraza, huku wakitakiwa kuhuisha taarifa zao kila mwaka kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

“Baraza litaendelea kuwajengea uwezo wa kitaaluma kupitia Mafunzo Endelevu ya Kitaaluma (CPD) ili kuhakikisha utoaji bora wa huduma za afya kwa wananchi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Pia wanafunzi wanaosomea kozi hiyo kwa sasa wameelekezwa kuendelea na masomo hadi kufikia kiwango cha astashahada au zaidi baada ya Desemba 2026 kama wanataka kupata usajili wa kitaaluma.

Historia ya kada ya watoa dawa

Kada ya watoa dawa wa kozi ya mwaka mmoja ilianzishwa miaka kadhaa iliyopita ili kusaidia kukabiliana na upungufu wa watumishi wa afya, hasa katika maeneo ya vijijini na vituo vya afya vya msingi.

Wahitimu wa mafunzo hayo walikuwa wakipewa ujuzi wa msingi kuhusu utoaji wa dawa, usimamizi wa stoo za dawa pamoja na matumizi salama ya dawa kwa wagonjwa.

Kwa muda mrefu, kada hiyo imekuwa msaada mkubwa katika maeneo yenye uhaba wa wafamasia na wataalamu wa famasi wenye elimu ya juu.

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Fadhili Hezekiah amesema, kuongezeka kwa mahitaji ya huduma bora za afya, maendeleo ya teknolojia ya tiba pamoja na mabadiliko ya mifumo ya utoaji huduma kumeifanya Serikali na wadau wa afya kuona umuhimu wa kuongeza kiwango cha elimu na umahiri wa watumishi wa kada hiyo.

Amesema katika miaka ya karibuni, Serikali imeendelea kuhimiza wataalamu wa afya kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na viwango vya kimataifa vya utoaji huduma za afya.

“Hatua ya Baraza la Famasi inaonekana kuwa sehemu ya mkakati huo wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama, bora na zinazotolewa na wataalamu wenye sifa zinazokidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya afya,” amesema Hezekiah.

Wadau wa afya wanaamini kuwa uamuzi huo utasaidia kuongeza ubora wa huduma za famasi nchini, ingawa unaweza pia kuibua changamoto ya upatikanaji wa watumishi katika baadhi ya maeneo ambayo bado yana upungufu wa wataalamu wa afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *