
Amir Saeid Iravani Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa nchi za kusini mwa Ghuba ya Uajemi na Jordan zinabeba dhima ya kuzisaidia Marekani na Israel katika uvamizi wao dhidi ya Iran.
Katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama siku ya Ijumaa, Iravani amenukuu taarifa za karibuni za maafisa wa Marekani, akiwemo rais wa nchi hiyo na kamanda wa CENTCOM zinazothibitisha kuwa baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi zilisimama “bega kwa bega na Marekani” wakati wa mashambulizi dhidi ya Iran.
Balozi Iravani ameeleza kuwa, Qatar, Bahrain, Kuwait, Saudi Arabia, Imarati na Jordan zilitoa kambi za kijeshi, msaada wa kilojistiki na kiutendaji, zilikuwa zikipeana taarifa za kiitelijinsia, zikishirikiana kwa upande wa ulinzi wa anga na ziliziruhusu Marekani na Israel kutumia anga zao kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran.
Balozi wa Iran UN ametaka Iran ilipwe fidia kamili kutokana na hasara na uharibifu uliosababishwa na vita vya Marekani na Israel.
“Licha ya Baraza la Usalama kushindwa kuziwajibisha nchi hizo za pwani ya kusini mwa Ghuba ya Uajemi na Jordan kwa vitendo vyao haramu dhidi ya Iran kwa mujibu wa sheria za kimataifa, zina wajibu kama nchi zinazopasa kubeba dhima ya jinai dhidi yake kuilipa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran fidia, ikiwa ni pamoja na kufidia uharibifu wote na hasara za kimaada n.k uliosababishwa na vitendo vyao viovu,” imeeleza barua ya Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa aliyowaandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo siku ya Ijumaa.
