Kundi la Kimataifa la Mawasiliano lazitaka pande hasimu Kongo kufanikisha juhudi za kukabiliana na EbolaKundi la Kimataifa la Mawasiliano lazitaka pande hasimu Kongo kufanikisha juhudi za kukabiliana na Ebola

Kundi la Kimataifa la Mawasiliano la Eneo la Maziwa Makuu (ICG) limebainisha wasiwasi wake kuhusu kuendelea mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku nchi hiyo ikiwa imeathiriwa na mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola.

Kundi la ICG lina wawakilishi kutoka Ubelgiji, Denmark, Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Uswidi, Uswisi, Uingereza na Marekani.

Kundi hilo limeeleza katika taarifa yao ya pamoja kwamba mlipuko wa Ebola nchini Kongo umezidisha hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.

“Kundi la Kimataifa la Mawasiliano la Eneo la Maziwa Makuu linazitaka pande zote zinazozozana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  kuwezesha juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Ebola. Tishio hili linasisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda ili kutatua changamoto za pamoja,” imeeleza taarifa ya ICG.

Kongo imeshuhudia ongezeko la visa vya Ebola tangu mlipuko huo ulipotangazwa Mei 15 katika jimbo la Ituri, ambapo hadi sasa ugonjwa huo umeenea katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa watu 750 wanashukiwa kuambukizwa Ebola huku wengine 177 wakithibitishwa kupoteza maisha kutokana na Ebola.

Serikali ya Kongo imesema kuwa virusi vya Ebola ni tishio kubwa katika maeneo ya nchi hiyo yanayodhibitiwa na waasi wa M23 kwa sababu kundi hilo halina uzoefu wa kushughulikia magonjwa ya milipuko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *