Licha yakuwa tumaini bora la amani duniani, Mkataba wa kuanzisha UN unazidi kusiginwa – GuterresLicha yakuwa tumaini bora la amani duniani, Mkataba wa kuanzisha UN unazidi kusiginwa – Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya kuwa dunia inazidi kuingia katika hali ya hatari kutokana na mataifa mengi kupuuza misingi na kanuni za Mkataba ulioanzisha Umoja wa Mataifam waka 1946, hali inayochochea vita, migogoro na kutokuwa na utulivu duniani.

Akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Kudumisha Malengo na Kanuni za Mkataba ulioanzisha UN na Kuimarisha Mfumo wa Kimataifa Unaotegemea Umoja wa Mataifa Guterres amesema Mkataba huo ulipitishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia ili kulinda amani, kuheshimu sheria za kimataifa na kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa njia ya amani badala ya matumizi ya nguvu.

Hata hivyo, amesema kanuni hizo sasa zinapuuzwa huku mataifa yakikiuka uhuru wa nchi nyingine, kuongeza matumizi ya nguvu na kushindwa kuwajibika kwa ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

Ametolea mfano Urusi kuendelea kushambulia Ukraine na Israeli kuendelea na mashambulizi Mashariki ya Kati.

Picha ya UN/Manuel Elías Picha inayoonyesha mtazamo mpana wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano wa wazi kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Migogoro na kasi za kuzalisha silaha vinaongezeka

Guterres amesema dunia sasa inashuhudia kiwango kikubwa zaidi cha migogoro tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, akitaja vita vinavyoendelea Ukraine, Sudan na Mashariki ya Kati.

Pia ameonya kuhusu ongezeko la matumizi ya silaha za kisasa, ndege zisizo na rubani na maendeleo ya haraka ya akili mnemba (AI), akisema teknolojia hizo zinaongeza hatari mpya kwa usalama wa dunia wakati hakuna usimamizi wa kutosha wa kimataifa.

Aidha, ameeleza kuwa haki za binadamu zinazidi kushambuliwa huku tofauti za kiuchumi zikiongezeka na mataifa mengi maskini yakikabiliwa na madeni makubwa na ukosefu wa fedha za maendeleo.

Wito wa kuheshimu sheria za kimataifa

Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa dunia haiwezi kuwa na amani bila kuheshimu sheria za kimataifa na kutumia diplomasia kutatua migogoro.

Amehimiza uwekezaji mkubwa katika kuzuia migogoro, kujenga amani na kuimarisha mazungumzo ya kisiasa badala ya vita.

“Lazima mataifa yaheshimu sheria za kimataifa bila upendeleo na kuhakikisha wanaokiuka sheria wanawajibishwa,” amesema.

Mageuzi ya Baraza la Usalama

Guterres pia ametoa wito wa mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili liweze kuendana na hali ya dunia ya sasa.

amesema kutokuwepo kwa uwakilishi wa kudumu wa Afrika katika Baraza hilo ni “ukosefu wa haki wa kihistoria” unaodhoofisha uaminifu wa Umoja wa Mataifa.

Akihitimisha hotuba yake, amewataka viongozi wa dunia kurejesha imani katika mfumo wa kimataifa na kuhakikisha Umoja wa Mataifa unabaki kuwa chombo muhimu cha kulinda amani, sheria za kimataifa na usalama duniani.

UN Photo/Loey Felipe Nakala halisi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa imeoneshwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York.

‘Chombo kinaenda kusiko’ yasema China Rais wa Baraza la Usalama

“Meli kubwa ya ustaarabu wa binadamu inaelekea katika maji hatari — na amani pamoja na maendeleo ya dunia vipo katika njia panda ya hatari,” amesema Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China ambaye ndiye ameongoza kikao cha Baraza la  Usalama kwa kuwa taifa hilo linashikilia urais wa Baraza kwa mwezi huu wa Mei.

Amesema changamoto za sasa zinapima dhamira ya jumuiya ya kimataifa katika kulinda amani, azma yake ya kusimamia haki, pamoja na ujasiri wake wa kufanya mageuzi makubwa.

“Lazima tusimame kwa umoja na kuchukua hatua pamoja kuilinda, kuifufua na kuiimarisha Umoja wa Mataifa,” amesisitiza.

Wakati Katibu Mkuu amependekeza marekebisho ya muundo wa Baraza ili kuongeza uwakilishi wa kudumu, Bwana Wang yeye amependekeza Baraza hilo kuboresha kanuni zake za utendaji kazi, kuhakikisha mapendekezo yake yanakuwa “ya haki, yasiyo na upendeleo na yanayojumuisha wote,” na kuepuka “kulazimisha” mipango yenye utata.

Mathalani amesema “wanachama watano wa kudumu wa Baraza hilo wanapaswa kuongeza mawasiliano na kutafuta “makubaliano ya pamoja kwa kiwango cha juu zaidi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *