Moshi. Simanzi na majonzi vimetawala katika Kitongoji cha Mwitini, Kijiji cha Mwasi Kusini, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro baada ya mtoto mwenye umri wa miaka mitatu kufariki dunia kwa kuteketea kwa moto ndani ya nyumba yao.
Mtoto huyo, Francis Andrew David alipoteza maisha katika tukio hilo la Mei 26, 2026 katika Kata ya Uru Mashariki, ambapo moto huo uliteketeza sehemu ya nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na wazazi yake.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremia Mkomagi amesema chanzo cha moto bado kinachunguzwa.
Mwili wa mtoto wa miaka mitatu ulioteketea kwa moto, Francis David ukipakiwa katika gari la Polisi. Picha na Yese Tunuka
Amesema Jeshi la Zimamoto lilipokea taarifa za tukio hilo saa 9:04 alasiri na askari walipofika eneo la tukio walikuta wananchi wamefanikiwa kuuzima moto huo.
“Askari walikuta mwili wa mtoto Francis ukiwa umeungua chini ya kitanda ndani ya nyumba hiyo na ulikabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi,” amesema Mkomagi.
Amesema Jeshi la Zimamoto linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari dhidi ya majanga ya moto na umuhimu wa kutoa taarifa mapema kupitia namba ya dharura 114.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Andrew David ambaye ni dereva wa bodaboda, amesema alipokea taarifa za tukio hilo akiwa barabarani akiendelea na shughuli zake za usafirishaji.
Amesema habari hizo zilimpa mshtuko uliomsababisha aanguke chini kwa huzuni.
“Nilipigiwa simu nikiwa njiani, nikatakiwa nirudi haraka nyumbani kwa sababu kulikuwa na tatizo. Njiani nikakutana na watu wakisema mtoto ameteketea kwa moto, nilishtuka sana hadi nikapiga magoti chini,” amesema akipangusa machozi.
Amesema kabla ya kuondoka nyumbani saa 3 asubuhi alikuwa pamoja na mkewe na mtoto huyo baada ya watoto wengine watatu kwenda shule.
Amesema anaamini huenda chanzo cha moto ni mtoto huyo kuchezea kiberiti baada ya kuachwa ndani peke yake kwa muda mfupi.
“Mtoto alikuwa na tabia ya kushika viberiti na kutishia kuwasha moto. Nafikiri mama yake alipotoka kwenda kwa jirani kutafuta mboga, mtoto alichezea kiberiti ndipo moto ukatokea. Siamini kama ni hitilafu ya umeme au gesi,” amesema.
Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa mashuhuda wa kwanza kufika eneo la tukio, Emanuel Kimambo amesema alibaini kuwepo kwa moto huo baada ya kuona moshi mzito ukifuka, jambo lililomfanya akimbilie kwa jirani kuomba msaada kabla ya kumtafuta mmiliki wa nyumba hiyo ambaye alishtuka na kubainisha kuwa mwanaye alikuwa ndani.
Askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro akiwa ameubeba mwili wa mtoto wa miaka mitatu, Francis David ulioteketea kwa moto. Picha na Yese Tunuka
Amesema mashuhuda na majirani walipambana kwa nusu saa kuzima moto huo kwa maji, lakini walipoingia ndani walimkuta mtoto huyo akiwa amefariki dunia, kabla ya kikosi cha Zimamoto kuwasili na kumalizia kuzima cheche zilizosalia darini.
“Tulipambana sana na majirani kwa karibu dakika 30 kuzima ule moto kwa kutumia maji. Lakini tulivyofungua mlango na kuingia kwenye kile chumba kilichokuwa kinafuka moshi, tulimkuta mtoto akiwa tayari ameshatangulia mbele ya haki,” amesema Kimambo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwitini, Winfrida Kisoli amesema alipokea taarifa za tukio hilo mchana akiwa kwenye shughuli za msiba.
“Niliona gari la Zimamoto likipita likiwa linapiga ving’ora, muda mfupi baadaye, nikapigiwa simu kuhusu tukio hilo. Tulipofika eneo la tukio tulikuta moto tayari umezimwa na mtoto amelala pembeni akiwa amefariki,” amesema.
