
Akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Alhamisi, Bwana. Guterres amesema mageuzi hayo ni muhimu kwa sababu “kutochukua hatua wakati huu wa misukosuko ya kisiasa duniani kutazidisha mateso ya binadamu.”
Mpango huo ulizinduliwa mwezi Machi mwaka 2025 ukiwa na lengo la kuhakikisha kwamba “kila jukumu, kila dola na kila uamuzi” unaleta matokeo makubwa zaidi kwa watu na sayari, wakati ambapo mahitaji yanaongezeka huku rasilimali zikipungua.
Katibu Mkuu ameueleza mradi huo kama “mabadiliko makubwa ya namna mfumo wa Umoja wa Mataifa unavyopanga kazi zake na kushirikiana ili kuleta matokeo makubwa zaidi,” na kutangaza kuwa sasa umeingia katika hatua mpya muhimu ya maamuzi na utekelezaji.
Kazi tayari zinaendelea
Taarifa ya maendeleo iliyotolewa Jumanne wiki hii imeainisha hatua ambazo tayari zimechukuliwa ili kuongeza ufanisi, kupitia namna mamlaka na majukumu yanavyotekelezwa, pamoja na kuchunguza uwezekano wa kufanya mabadiliko katika muundo wa ndani wa Umoja wa Mataifa, ikiwemo uwezekano wa kuunganisha baadhi ya mashirika yake.
Kazi za kurahisisha shughuli ndani ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa na maeneo mengine tayari zinaendelea, ikiwemo hatua za kupunguza kurudiwa kwa kazi zinazofanana na kuboresha uratibu. Hatua hizo ni sehemu ya juhudi pana za kuuboresha mfumo wa utendaji wa Umoja wa Mataifa.
Mpango huo pia unalenga kurahisisha michakato ya kiutawala na kuimarisha huduma ndani ya mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kutoa msaada wa haraka zaidi na wa gharama nafuu kwa nchi wanachama.
Kuimarisha mamlaka na uwajibikaji
Nguzo nyingine muhimu ya mageuzi hayo inalenga jinsi mamlaka na majukumu yanayotolewa na nchi wanachama yanavyobuniwa, kutekelezwa na kutathminiwa.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa tayari kuna kazi inayoendelea kwa kushirikiana na serikali za kitaifa ili kuongeza uwazi, kupunguza mzigo wa utoaji taarifa na kuhakikisha kuwa mamlaka hayo yanaendana na rasilimali pamoja na matokeo yanayotarajiwa.
Kwa kuwa Umoja wa Mataifa una maelfu ya majukumu yanayoongoza shughuli zake, mchakato wa kuyapitia unalenga kuhakikisha yanaendelea kuwa muhimu, yenye mshikamano na yanayolenga kutoa matokeo yanayopimika.
Nchi wanachama kuwa kiini cha hatua zinazofuata
Mapendekezo ya mabadiliko ya muundo wa Umoja wa Mataifa yanajumuisha kuimarisha ushirikiano kati ya idara na mashirika mbalimbali pamoja na kuongeza uratibu kati ya taasisi zinazoshughulikia amani na usalama, maendeleo na haki za binadamu.
Mpango huo umebaini umuhimu wa kupunguza utendaji wa kila taasisi kufanya kazi kivyake na badala yake kuimarisha mifumo ya pamoja, sambamba na matumizi ya zana mpya kama mifumo ya pamoja ya takwimu na mbinu bora za uratibu.
Hata hivyo, maamuzi kuhusu mabadiliko ya muundo wa Umoja wa Mataifa yako mikononi mwa nchi wanachama ambazo zitakuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu vipaumbele na utekelezaji wake.
Akielezea mpango wa UN80 kama “kazi inayoendelea,” Katibu Mkuu amesema ushiriki endelevu ndio njia ya kujenga Umoja wa Mataifa wenye mshikamano na ufanisi zaidi.
Kadri mpango huo unavyoendelea, vipengele vyake mbalimbali vinatarajiwa kuunganishwa ili kuunda mfumo mmoja utakaowezesha hatua madhubuti zaidi na zenye uratibu bora.
Mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa
- Kupunguza kwa asilimia 21 nafasi za kazi katika bajeti ya mwaka 2026 huku athari kwa wafanyakazi zikidhibitiwa.
- Timu 11 zimeunganishwa katika jukwaa moja la pamoja la kiutawala linalohudumia wafanyakazi 6,000 mjini New York, huku vituo vingine vitano vikitarajiwa kufuata.
- Kituo cha Kidijitali kimezinduliwa Valencia, Hispania, kusaidia utoaji wa huduma za kidijitali katika Sekretarieti nzima.
- Vituo 10 vya mishahara vimeunganishwa kuwa timu moja.
- Nafasi 220 za Sekretarieti zimehamishwa kutoka maeneo yenye gharama kubwa, pamoja na takribani nafasi 1,900 zaidi katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa.
- Mchakato wa kupunguza nafasi za viongozi wa ngazi za juu unaendelea, huku matarajio ya kupunguzwa zaidi yakitarajiwa kuonekana katika bajeti ya mwaka 2028.
- Utekelezaji wa majaribio wa Mpango Mpya wa Mkataba wa Kibinadamu umeanza katika mazingira matano ya migogoro, Afghanistan, Haiti, eneo la Palestina linalokaliwa, Somalia na Sudan ukiwa unahusisha kuunganishwa kwa mifumo ya usambazaji bidhaa ambayo inachangia asilimia 70 ya matumizi yote ya misaada ya kibinadamu.
