
Dodoma. Wabunge wametaka Serikali ibadili mfumo wa ujenzi wa nyumba ambazo zimekuwa zikisimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Shirika la Nyumba (NHC) ili kuwepo na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
Wamesema mpango huo utasaidia watu wenye vipato vya chini kumiliki nyumba ikiwemo waendesha bodaboda na bajaji ambao hata ikibidi wawe wanalipa kwa mfumo wa kila siku.
Wakichangia kwenye hotuba ya bajeti leo Alhamisi Mei 28, 2026, wabunge hao wametaja maendeleo hayawezi kufikiwa ikiwa hakutakuwa na mikakati ya kubadili mfumo hasa kwa watu wa ngazi ya chini ambao wanaanzisha migogoro.
Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Fadhili Ngajilo amesema nyumba za NHC zimejengwa lakini siyo rafiki kwa watu wa kipato cha chini kwani zinauzwa kwa bei ya juu licha ya matangazo kuwa ni za bei ndogo.
Ngajilo amesema hakuna mtu wa kipato cha chini ambaye anaweza kumudu kununua nyumba za bei ya Sh200 milioni wakati kipato chake ni kidogo akihimiza wahusika kama wataona inafaa wakajifunze katika mataifa mengine.
“Mipango ya NHC ni mizuri, mahitaji ya nyumba ni makubwa na watu wanatamani kuwa na nyumba, lakini hizi bei siyo rafiki, tulisaidie shirika hili ili liweze kuja na mpango mzuri wa kujenga nyumba za hata Sh30 milioni lakini watu wawe wanalipa kidogokidogo hata kwa kila siku,” amesema Ngajilo.
Mbunge wa Vwawa (CCM) Japhet Hasunga amesema Watanzania wanataka kuwa na makazi bora na yenye hadhi lakini wanakwama kwenye gharama za jinsi ya kununua nyumba.
Hasunga amesema shirika hilo likiwezeshwa likawa na mikakati ya kuangalia kipato cha wahitaji, linaweza kuwasaidia Watanzania na wengi watajikuta wanamiliki nyumba bora ambazo mwisho wa siku zitakuwa ni msaada kwa maisha yao.
Mbunge mwingine aliyeomba uwepo mkakati wa nyumba bora za gharama nafuu ni Jafari Chege ambaye ameomba NHC isaidiwe vinginevyo watabaki na nyumba hizo kwa kuwa zinauzwa kwa bei ya juu ambayo inachagua watu.
