
Musoma. Serikali imetoa zaidi ya Sh1.3 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha vijana zaidi ya 40 kuanzisha miradi ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Akizungumza mjini Musoma leo Alhamisi Mei 28, 2026 wakati wa shughuli ya utoaji wa mitaji kwa vijana hao, Msimamizi wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) upande wa uvuvi, Peter Masumbuko amesema fedha hizo zimetolewa kama mkopo wenye masharti nafuu kwa vijana hao kwa lengo la kusaidia mapambano dhidi ya changamoto ya ajira.
Amefafanua kuwa fedha hizo zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali ikiwemo vizimba, vibanda vya ulinzi, boti mbili za kulishia samaki pamoja na fedha za kujikimu.
“Programu inalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uvuvi sambamba na kuongeza uzalishaji wa mazao ya majini ili kukabiliana na changamoto za kiuchumi na ajira kwa vijana,” amesema.
Ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kuzalisha tani 120 za samaki ndani ya miezi saba, akieleza kuwa kizimba kimoja kina uwezo wa kubeba samaki 1,280 kwa msimu mmoja.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Samwel Mdachi amesema vijana hao ni sehemu ya vijana 500 waliopata mafunzo kuhusu Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora katika sekta za mifugo na uvuvi yaliyoratibiwa na wizara hiyo mwaka 2024/25.
“Vijana hawa wamepata mafunzo mbalimbali na kabla ya kupewa mitaji hii waliandika maandiko yaliyowawezesha kupata mikopo hiyo yenye masharti nafuu,” amesema.
Amesema mafunzo hayo yalilenga kubadili mtazamo wa vijana kuhusu kuajiriwa na kuwahamasisha kujiajiri kwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo nchini.
Mdachi amesema utekelezaji mzuri wa mradi huo utakuwa na matokeo chanya kwa vijana, jamii na Taifa kwa ujumla katika kuboresha maendeleo na uchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amewataka wavuvi wa asili kutokuingilia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa vizimba ili uwekezaji huo uweze kuleta tija.
“Serikali inataka kufungua uchumi kupitia sekta ya uvuvi. Tunataka wale wanaofanya uvuvi wa asili na huu wa vizimba waende pamoja, hivyo tunaomba shughuli za uvuvi wa asili zisifanyike ndani ya mita 100 hadi 200 kutoka eneo la uwekezaji,” amesema.
Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuboresha uchumi na kuibua fursa za ajira kwa wananchi.
Akizindua programu hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewataka wanufaika kusimamia mradi huo kwa kuzingatia kanuni za ufugaji bora na wa kisasa ili uwe na tija kwa jamii.
Amesema Serikali imejipanga kukabiliana na changamoto za kiuchumi kwa vijana kupitia sekta mbalimbali ikiwemo uvuvi, kilimo, mifugo na madini.
Kanali Mtambi pia amewataka vijana kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa ajili ya kutafuta na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
