
ILIPOISHIA
Nikaona nimtafute Dastan Lazaro ili nimueleza matatizo yaliyonitokea ili aweze kunipa msaada wake.Nilitegemea nikimpata Dastan anaweza kujua yule msichana aliyeniibia anapatikana wapi.Na Dastan pia anaweza kunisaidia kuzipata pesa zangu hata kama si zote.
Sasa kulikuwa na tatizo la kumpata Dastan kwa sababu nilikuwa sijui anakoishi.Hapo hapo nikakumbuka kwamba aliniambia yeye ni meneja masoko katika kiwanda cha bia.
SASA ENDELEA…
Nikajiambia kuwa ningeweza kuulizia kiwanda hicho kiko wapi kisha nikamfuata na kumweleza matatizo yangu.
Wakati ninaendelea kwenda bila kujua nilikuwa ninaenda wapi, nikaanza kuuliza watu kilipo kiwanda cha bia.
Nikafuata maelekezo ya watu hadi nikatokea Barabara ya Uhuru. Niliambiwa kiwanda hicho kilikuwa Ilala. Nikaendelea kuuliza huku nikitembea kwa miguu mpaka nikafika.
Nilivyofika nilikwenda kwenye geti. Nikamkuta askari ambaye nilimweleza tatizo langu. Yeye naye akanionyesha ofisi ya maulizo, nikaenda.
Nilipofika nilimkuta msichana ambaye aliniuliza nilikuwa ninataka nini.
“Ninamuulizia bwana Dastan Lazaro,” nikamwambia.
“Dastan Lazaro?” msichana akaniuliza akiwa amekunja uso akijaribu kuwaza kana kwamba jina hilo lilikuwa geni kwake.
“Ndiyo, Dastan Lazaro.”
“Anafanya kazi gani?”
“Yeye ni meneja masoko.”
“Meneja masoko?”
“Ndiyo.”
“Hapa hatuna meneja masoko mwenye jina hilo. Kwanza meneja masoko wetu ni mwanamke.”
“Ameniambia kuwa yeye ni meneja masoko. Kwani wapo wangapi?”
“Ni mmoja tu naye ni mwanamke.”
“Sasa sijui, labda nimesahau cheo chake, lakini jina lake ni hilo.”
“Yeye ni mwenyeji wa wapi?”
“Ni mwenyeji wa Muheza.”
Yule msichana akaguna kisha akaniuliza, “Ni nani wako?”
“Ni ndugu yangu. Nilikutana naye juzi akaniambia anafanya kazi kiwanda cha bia. Si ndiyo hiki hapa au kuna kingine?”
“Kiwanda cha bia ndiyo hiki hiki. Hebu subiri nikuulizie.”
Msichana akainua mkono wa simu na kubonyeza tarakimu kisha akasubiri. Baada ya sekunde chache akauliza, “Eti kuna mfanyakazi yeyote kwenye kiwanda hiki anayeitwa Lazaro?”
Msichana akasikiliza kisha akasema, “Kuna mtu hapa amekuja kumuulizia. Anasema ni meneja masoko. Nikamwambia meneja masoko wa kiwanda hiki ni mwanamke. Akasema labda amesahau cheo chake.”
Msichana akasikiliza tena kisha akarudisha mkono wa simu.
“Hakuna afisa yeyote wala mfanyakazi yeyote wa kampuni hii mwenye jina hilo,” msichana akaniambia.
Moyo ukaniripuka. Mshituko ulionipata ulinifanya niduwae.
“Huyo mtu aliyekuambia anaitwa Dastan Lazaro na ni meneja masoko wa kiwanda hiki alikudanganya!” msichana aliendelea kuniambia.
“Alinidanganya?”
“Ndiyo, alikudanganya. Sisi hapa hatuna mfanyakazi anayeitwa Dastan Lazaro.”
Hapo nilijua kwamba ni kweli Dastan Lazaro alinidanganya. Hakuwa mfanyakazi wa kiwanda kile. Na kama alinidanganya basi yeye na wale wasichana lao ni moja. Wote ni majambazi.
“Sasa nitafanyaje?” nikajiuliza.
Kwa kweli sikupata jibu la haraka. Ukweli ni kuwa nilikuwa nimekwama. Sasa sikuwa na haja tena na pesa zangu zilizoibiwa; haja yangu ilikuwa ni kupata pesa ya nauli tu ili nirudi kwetu.
Kuendelea kukaa katika jiji hilo nikiwa sina hata senti tano na sijui nitakula wapi au kulala wapi lilikuwa tatizo. Lakini lilikuwa tatizo kubwa zaidi kwa vile nilijua polisi walikuwa wananitafuta wanikamate. Na watakaponipata sitakuwa na utetezi wowote. Kitendo changu cha kuwatoroka kimeshawadhihirishia kuwa mimi ni mhalifu nisiyestahili msamaha.
“Asante dada, kwaheri,” nilimuaga yule msichana wa maulizo nikiwa sijui ninaenda wapi.
Wazo moja liliniambia kuwa niende Buguruni nikamtafute Dastan Lazaro. Buguruni kwenyewe sikuijua.
Bado nilijiambia, hata kama nitaelekezwa na nitaweza kufika, itakuwa si rahisi kumpata Dastan hasa kwa vile Buguruni ni kubwa na mimi ni mgeni.
Lakini wazo jingine likanijia. Je, kama Dastan alinidanganya na haishi Buguruni?
Nikawaza kwamba kwenda Buguruni kumtafuta Dastan ni kujipa kazi isiyokuwa na manufaa yoyote kwani inawezekana kuwa haishi Buguruni.
Bado nilijiambia, kupanga kumtafuta Dastan ni kujidanganya. Hata kama nitampata Dastan, haitakuwa rahisi kwangu kumfanya anirudishie pesa zangu na vitu vyangu walivyoniibia.
Na haitakuwa rahisi pia kumpeleka polisi ambako ninatafutwa kwa kesi ya kukutwa na kete ya madawa ya kulevya.
Dastan anaweza kudai kuwa ni kete yangu na pia kudai hanitambui.
Kama ni kufanywa bwege, nimefanywa bwege kwa kiwango cha juu. Baya zaidi nimefanywa bwege na ndugu yangu wa nyumbani kabisa. Hivyo nilijiambia ushamba wangu na ulimbukeni wangu ndivyo vilivyoniponza.
Nilijiuliza kwa nini nilikataa nilipoambiwa nisisafiri na pesa, ni hatari. Nikang’ang’ania nipewe pesa mkononi. Huo ulikuwa ni ulimbukeni!
Pia nilijiuliza kwa nini baada ya kupewa pesa hizi sikuenda kupanda basi na kurudi Muheza, badala yake nikazunguka jiji la Dar es Salaam kununua vitu. Huo nao ulikuwa ni ushamba!
Lakini baya zaidi ya yote ni pale nilipoanza kufanya starehe na kwenda katika kumbi za muziki na kunywa pombe hadi kutojielewa.
Matatizo yaliyonikuta niliyataka mwenyewe kwa uzembe wangu. Muda huo ndiyo nilijua nilichofanya kilikuwa ni uzembe. Kama ningerudi Muheza jana ile ile ningekuwa nafurahia pesa zangu. Ningekuwa ninapanga jinsi ya kuzitumia pesa hizo.
Wakati nikiwaza hayo nilikuwa nikitamani kulia kwa uchungu; uchungu wa kufanywa bwege, uchungu wa kuibiwa pesa zangu na uchungu wa kukwama hapa Dar.
Lakini ilibidi nijikaze kiume na nihakikishe kuwa ninafanya mpango utakao niwezesha kurudi Muheza.
Nilikuwa narudi Mnazi Mmoja kwa miguu. Pale kilikuwa kituo cha mabasi ya kwenda Mkoa wa Tanga. Lakini nilikuwa nikitembea nikiwa makini nikiangalia huku na huku. Nilihofia kukutana na wale polisi niliowatoroka.
Kabla ya kufika katika kituo cha mabasi ya kwenda Tanga niliona teksi namba 1000 ikiwa imeegeshwa pembeni mwa Barabara ya Lumumba. Nikakumbuka yule karani wa hoteli niliyokuwa nimepanga chumba alisema teksi tuliyokwenda nayo usiku ilikuwa na namba 1000 ubavuni. Nikaifuata.
Nilimkuta dereva wa teksi akisinzia. Nilipofika karibu na mlango wa teksi alizinduka na kunitupia macho. Aliponiona tu alijua kuwa nilikuwa ninahitaji teksi, akanifungulia mlango wa nyuma.
“Ingia,” akaniambia haraka haraka.
Nikaingia kwenye teksi na kuketi lakini sikufunga mlango.
“Nina mazungumzo na wewe,” nikamwambia.
“Kuhusu nini?”
Niliona kama nitamletea hadithi nyingi angeweza kujifanya hajui chochote, nikamuuliza, “Unamfahamu Dastan Lazaro?”
Nilibahatisha tu kumuuliza kwa hisia kwamba huenda anajuana naye, lakini jibu alilonipa lilinishitua.
“Unamhitaji kwa shughuli gani?”
“Aliniambia kuna kitu anauza,” nikamwambia baada ya kufikiri kidogo.
“Wewe ulikuwa unahitaji nini?”
“Redio kubwa. Aliniambia anayo redio anauza.”
“Sawa. Dastan hakai mbali sana. Yuko mtaa wa tatu tu kutoka hapa. Naweza kukupeleka lakini utalipia teksi yangu.”
“Si kitu, twende,” nikamwambia.
Nikafunga mlango wa ile teksi. Dereva huyo akaipiga moto teksi. Tukaondoka.
Sikuwa na hata senti tano mfukoni mwangu, achilia mbali pesa za kulipia teksi. Lakini nilimwambia twende kwa sababu niligundua yeye na Dastan lao ni moja, wanajuana. Kwa hiyo nilipanga tukifika huko na nikimpata Dastan, yeye ndiye atakayelipia teksi na kunirudishia pesa zangu walizoniibia.
Baada ya dakika chache tu teksi ilisimama mbele ya nyumba moja chakavu.
“Anaishi hapa?” nikamuuliza dereva wa teksi.
“Subiri,” akaniambia huku akishuka.
Alikwenda kwenye mlango ambao ulikuwa wazi, akapiga hodi. Hakukuwa na jibu lakini aliingia hivyo hivyo. Nilipomwona anaingia na mimi nilifungua mlango wa teksi nikashuka na kumfuata.
Niliingia humo ndani. Nyumba ilikuwa kimya. Dereva huyo alikwenda hadi mlango wa uani akatoka nje. Kitu kilichonidhihirishia kuwa alikuwa mwenyeji.
Nilipiga hatua za haraka haraka na mimi nikafika uani. Nilipotupa macho nilimwona akiingia kwenye chumba kimoja miongoni mwa vyumba vitatu vilivyokuwa uani.