Dar es Salaam. Dirisha la msimu wa pili wa tuzo za uandishi wa habari za ‘Samia Kalamu Awards 2026’ limefunguliwa ambapo tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa Desemba 2026.

Tuzo hizo kwa mara ya kwanza zilianza kutolewa Mei 2025, lengo likiwa kutambua, kuthamini na kuhamasisha uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora, yanayochangia kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha, na kuimarisha taswira chanya ya Taifa, kupitia habari za maendeleo.

Mwaka huu ikiwa ni awamu yake ya pili kufanyika, tuzo hizo zimeratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) na Bodi ya Ithibati kwa waandishi wa Habari (JAB).

Akizungumza  na waandishi wa habari leo Jumapili Mei 31, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, na Mwenyekiti wa tuzo hizo, Peter Mwasalyanda amesema makundi yatakayohusika katika tuzo hizo ni tuzo maalumu za kitaifa, tuzo kwa vyombo vya habari na tuzo za kisekta.

Wakati kuhusu vigezo vya jumla vya ushiriki amesema mwandishi wa habari anapaswa kuwa raia wa Tanzania, awe amethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa upande wa Tanzania Bara, kwa Zanzibar awe anatambuliwa na mamlaka husika.

“Pia awe na kitambulisho cha mwandishi wa habari na asiwe na rekodi ya kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai,” amesema.

Aidha Mwasalyanda amesema kazi itakayowasilishwa inapaswa kuwa iliyochapishwa, kutangazwa au kurushwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza katika vyombo vya habari vya ndani au nje ya Tanzania.

Pia iwe iliyofanyiwa utafiti wa kina, inayohusisha uchambuzi na takwimu na inayohusisha vyanzo vya habari visivyopungua vinne.

Jingine isiwe imeshindanishwa katika tuzo nyingine na iwe imechapishwa, kutangazwa au kurushwa kati ya Julai 01, 2025 hadi Juni 15, 2026.

“Vilevile iwe inayohusu masuala ya maendeleo na kuibua simulizi za wananchi zinazoonesha namna miradi ya kitaifa ilivyofungua fursa na kubadili maisha ya wananchi

“Iwe na maudhui yanayozingatia ulinzi wa haki-miliki na haki shiriki na kwa chombo cha habari kigezo kiwe na leseni hai iliyotolewa na mamlaka husika,” amesema.

Kuhusu uwasilishaji wa kazi za kushindanishwa amesema mchakato wa kuzipokea utaanza rasmi Mei 31, 2026 na kuhitimishwa Juni 30,2026 kupitia tovuti ya tuzo hizo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo kazi zitakazopokelewa ni zilizochapishwa au kurushwa kuanzia tarehe Julai 1, 2025 hadi Juni 30, 2026.

Hata hivyo, amesema kwenye upigaji kura, za wananchi zitachangia asilimia 60 huku za majaji wakichangia asilimia 40.

“Mfumo huo   unalenga kuhakikisha washindi wanatambuliwa kwa kuzingatia ubora wa kazi pamoja na namna kazi hizo zinavyoathiri maendeleo ya wananchi na uchumi wa Taifa letu,”amesema Mwasalyanda

Kwa upande wake Mkurugenzi wa JAB, Patrick Kipangula amesisitiza waandishi wote watakaoshiriki kuhakikisha wanakuwa na ithibati kwa kuwa ni takwa la kisheria.

Pia amehimiza waandishi kushiriki wote wakiwa na habari zilizo na matokeo na zenye weledi.

Naye Mwenyekiti wa Tamwa, Dk Kanael Kaale, amewaondoa wasiwasi wananchi kuwa tuzo hizo zimelenga kuwaweka waandishi mfukoni.

Dk Kanaeli amesema ni lazima habari kuhusu maendeleo nazo ziandikwe badala ya kukosoa tu kwa kuwa hakuna atakayekuja kuziandika isipokuwa Watanzania wenyewe.

“Maendeleo ndio chachu ya Taifa, na sisi kama Tamwa tunaona maendeleo yakiwepo yanamgusa mwanamke moja moja,” amesema Mwenyekiti huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *