
“Tunatarajia kuona watu zaidi wakipona, hasa wale wanaogunduliwa mapema na kupata huduma za afya kwa wakati, huku juhudi za kudhibiti mlipuko zikiongezwa kasi,” limesema Shirika la Afya la Umoja wa Mataiffa Duniani (WHO) katika taarifa yake ya jana Jumapili.
Kwa jumla, watu watano wamepona virusi hivyo, shirika hilo lilisema, likitaja pia mfanyakazi wa maabara ambaye alitangazwa kuwa amepona kabisa Alhamisi iliyopita.
Tangazo hilo ni habari njema wakati juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo zikiendelea kuongezwa. Hali hii ni muhimu zaidi kwa sababu hakuna chanjo au tiba iliyoidhinishwa kwa sasa, na WHO imeeleza ugonjwa huo kama “ugonjwa unaoweza kuupata unapomhudumia mtu mwingine”.
Idadi ya waathirika inaongezeka
Kufikia jana Jumapili, kulikuwa na wagonjwa 210 waliothibitishwa wa maambukizi ya Ebola nchini humo, pamoja na vifo 17 vilivyothibitishwa.
Takriban wagonjwa 350 wanaoshukiwa wanaendelea kuchunguzwa, huku wahudumu wa afya 16 wakithibitishwa kuambukizwa Ebola katika mlipuko huu wa karibuni nchini DRC.
Tangu kutangazwa kwa mlipuko wa Ebola tarehe 15 Mei, hatua muhimu za kukabiliana nao zimejumuisha upimaji wa maabara, ufuatiliaji wa ugonjwa, kuzuia na kudhibiti maambukizi, ushirikishwaji wa jamii na uhamasishaji wa rasilimali.
Katika mji wa Bunia, unaoaminika kuwa kitovu cha mlipuko huo na mji mkuu wa jimbo la Ituri, WHO imekabidhi Kituo cha Matibabu ya Ebola kilichokarabatiwa kwa mamlaka za afya.
Kituo hicho kina vitanda 24 na uwezo wa jumla wa vitanda 60. WHO pia inaandaa jengo la nyongeza litakalokuwa na hadi vitanda 42.
Changamoto za kudhibiti mlipuko
Juhudi za kudhibiti mlipuko huo zimekuwa ngumu kutokana na hali mbaya ya kibinadamu katika eneo la mashariki mwa DRC lenye utajiri mkubwa wa rasilimali.
Miongo kadhaa ya migogoro imewaacha watu milioni 1.2 katika jimbo la Ituri pekee wakihitaji msaada wa kibinadamu.
Maambukizi yamejikita zaidi katika jimbo la Ituri pamoja na majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Tiba zinazoendelea kufanyiwa utafiti
Ingawa hakuna chanjo au tiba iliyoidhinishwa kwa virusi vya Bundibugyo vinavyosababisha Ebola, vikundi vya ushauri vya WHO vimeeleza kuwa baadhi ya tiba na chanjo zinazofanyiwa utafiti zinaonesha matumaini makubwa kiasi cha kupewa kipaumbele katika majaribio ya kitabibu.
Jukumu la WHO ni kushirikiana na mamlaka za afya za DRC na Uganda ili kuhakikisha majaribio hayo yanafanyika.
Kwa wagonjwa waliothibitishwa kuambukizwa, tiba tatu zinazopewa kipaumbele kwa majaribio ya kitabibu ni kingamwili za monokloni MBP 134 na maftivimab, pamoja na dawa ya kuzuia virusi ya remdesivir.
Kwa upande wa kinga, dawa ya kuzuia virusi inayotumiwa kwa njia ya mdomo iitwayo obeldesivir inapewa kipaumbele katika utafiti wa kitabibu kama hatua ya baada ya kuambukizwa kwa wale waliokutana na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola.
Kwa mujibu wa WHO, chanjo mbili zinazotarajiwa zimechaguliwa kwa ajili ya tathmini mara tu dozi zitakapopatikana.
Wito wa mshikamano kutoka kwa Tedros
Wakati huo huo, WHO imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika kukomesha maambukizi ya virusi hivyo, ambavyo vina kiwango cha vifo kati ya asilimia 30 na 50.
“Ebola inayosababishwa na virusi vya Bundibugyo inaweza kuokolewa kwa huduma bora za matibabu, na baadhi ya watu hapa Ituri tayari wamepona. Kutafuta matibabu mapema kunaleta tofauti kubwa sana. Bado kuna matumaini,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, akizungumza na waandishi wa habari mjini Bunia mwishoni mwa wiki.
Katika taarifa ya Ijumaa, WHO ilieleza kuwa mlipuko huo nchini DRC na nchi jirani ya Uganda unaendelea kubadilika kwa kasi, ukiwa na ongezeko la wagonjwa, kuenea kwa maambukizi katika maeneo mapya, na maambukizi yanayovuka mipaka.
Pia, mgonjwa mwingine aliyethibitishwa ni raia wa Mrekani ambaye alikuwa akiwatibu wagonjwa nchini DRC. Mtu huyo bado anaendelea kupatiwa matibabu nchini Ujerumani.