Hali ikoje Lebanon? 

“Hali nchini Lebanon inatia wasiwasi mkubwa,” amesema Martha Ama Akyaa Pobee ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kisiasa na ujenzi wa amani, wakati akilihutubia Baraza hilo la Usalama. Amesema “vikosi vya ardhini vya Israel vinaendelea kusonga mbele kuelekea kaskazini mwa Lebanon” na “mashambulizi makali zaidi ya Hezbollah yanayofika maeneo ya ndani zaidi nchini Israel.”

Pobee amesema operesheni za hivi karibuni za Israel zimehusisha kuteka Kasri la Beaufort, kusogea mbele kaskazini mwa Mto Litani katika eneo la “Yohmor Triangle”, pamoja na kuimarisha mashambulizi ya anga huko kusini mwa Lebanon katika Bonde la Beqaa na maeneo ya pembezoni mwa Beirut.

Ameongeza kuwa Israel pia imetoa “maonyo ya dharura” kwa raia kuyahama maeneo yaliyoko kusini mwa Mto Zahrani, huku Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL, kikiripoti shughuli kubwa za kijeshi kaskazini mwa Mstari wa Bluu.

Kwa mujibu wa Pobee, UNIFIL imerekodi makombora 992 yaliyofyatuliwa na Jeshi la Israel tarehe 30 Mei, ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu makubaliano ya kusitisha mapigano ya tarehe 17 Aprili 2026.

Kwa upande mwingine, amesema Hezbollah imeendelea kurusha makombora, yanayoongozwa dhidi ya vifaru na ndege zisizo na rubani, zikiwemo ndege mpya zenye nyaya za mawasiliano. “Maendeleo haya yanaashiria ongezeko hatari na la kutisha la mzozo,” ameonya Pobee, akisema yanadhoofisha makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa Aprili 16 na kuathiri juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano huo.

UN Photo/Eskinder Debebe Martha Ama Akyaa Pobee, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Afrika katika Idara za Siasa na Masuala ya Ujenzi wa Amani na Operesheni za Amani akitoa muhtasari wa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Vikosi vya Israel lazima viondoke na kurejea kusini mwa Mstari wa Bluu

Akizungumzia juhudi za kidiplomasia za kumaliza mzozo huo, Pobee amesema uwepo wa vikosi vya Israel kaskazini mwa Mstari wa Bluu ni “ukiukwaji wa wazi wa mamlaka na mipaka ya Lebanon” pamoja na Azimio 1701 la Baraza la Usalama la mwaka 2006.

Amesisitiza kuwa “vikosi vya Israel lazima viondoke na kurejea kusini mwa Mstari wa Bluu”, huku akiongeza kuwa Hizbullah na makundi mengine yenye silaha yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuvuliwa silaha.

Pobee amesema “Jeshi la Lebanon ndilo jeshi pekee halali lenye mamlaka ya kubeba silaha nchini Lebanon”, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mamlaka ya Serikali ya Lebanon katika eneo lote la nchi hiyo.

Aidha amesema juhudi za kidiplomasia “lazima zipewe nafasi ya kufanikiwa”, akionya kuwa kuendelea kwa ongezeko la mvutano hakukubaliki wakati kukiwa na taarifa za vitisho kutoka Tehran vya kusitisha mazungumzo na Marekani, kuzuia njia ya bahari ya Hormuz na kufungua maeneo mengine ya mapambano.

© UNIFIL/Kandice Ardiel Mlinda amani wa UNIFIL akitazama eneo la Green Hill huko Naqoura, Lebanon.

Kilichosemwa na Ufaransa

Akizungumza katika kikao hicho, mwakilishi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Jérôme Bonnafont ambaye nchi yake ndiyo iliyoomba kuitishwa kwa mkutano huo amesema  ingawa anatambua haki ya Israel kujilinda, “hata hivyo, hakuna kinachoweza kuhalalisha kuendelea na ukubwa wa operesheni zake za kijeshi nchini Lebanon”, ambazo zimesababisha maelfu ya vifo na majeruhi miongoni mwa raia pamoja na kuwalazimu watu wengi kuyakimbia makazi yao.

Amesema kuendelea kwa operesheni hizo na kuongezeka kwa udhibiti wa Israel katika maeneo ya Lebanon ni “kosa kubwa la kimkakati kwa upande wa Israel”. Aidha, amesema hatua hizo zinakiuka ahadi ambazo Israel ilitoa tarehe 17 Aprili 2026 pamoja na maazimio ya Baraza la Usalama, akisisitiza kuwa ni muhimu mapigano yakome mara moja.

Bonnafont amesema hatua ya Israel kupandisha bendera yake kwenye ngome ya Beaufort, ambayo ilitumika kama kambi wakati wa uvamizi wa kusini mwa Lebanon hadi mwaka 2000, imeongeza uzito wa mzozo huo. “Israel inarejea katika kipindi ambacho wengi waliamini kimebaki nyuma,” ameonya, akiongeza kuwa “historia hutufundisha kwamba sababu zilezile zina uwezekano mkubwa wa kuleta matokeo yaleyale.”

© UNHCR/Dar Al-Mussawir/Ramzi Haidar Wakimbizi wa ndani ambao wamekimbia mapigano na kuvuka mpaka wanakusanyika karibu na daraja la Qasmiyyeh kusini mwa Lebanon. (Aprili 2026)

Kilichosemwa na Lebanon

Akizungumza kwa niaba ya Lebanon, Balozi Ahmad Arafa amesema kuwa licha ya juhudi za Serikali yake kudhibiti mgogoro wa sasa, Israel imeendelea na kile alichokiita “kujitwalia fursa, kama ilivyo kawaida yake, wakati wa mvutano wa kikanda” kwa kuendeleza ongezeko hatari la operesheni za kijeshi.

Amesema Israel inaendelea na “kampeni yake ya kimfumo ya uharibifu”, akidai kuwa imelenga kwa makusudi wahudumu wa afya, hospitali, waandishi wa habari, shule, vyombo vya usalama, vikosi vya UNIFIL, maeneo ya ibada, maeneo ya kihistoria na “malengo mengine mengi yanayowakilisha kumbukumbu za pamoja na utambulisho wa ustaarabu wa Lebanon”.

Lebanon imelaani vitendo hivyo ambavyo amesema “katika matukio mengi vinakaribia kuwa uhalifu wa kivita”. Balozi Arafa amesema pia ukosefu wa uwajibikaji umechangia kuendelea kwa hali hiyo. Amesisitiza kuwa Israel inapaswa kukubali kusitisha mapigano ili Serikali ya Lebanon iweze kurejesha mamlaka yake katika eneo lote la nchi, akiongeza kuwa mara hilo litakapotekelezwa, “Serikali pekee ndiyo itakayowajibika kwa ukiukwaji wowote utakaotokea baadaye.”

© UNICEF Barabara imejaa vifusi vya majengo yaliyoharibiwa vibaya na mapigano ya hivi karibuni karibu na hospitali huko Tebnine, kusini mwa Lebanon.

Kilichosemwa na Israel 

Akizungumza kwa niaba ya Israel, Balozi Danny Danon amesema nchi yake “haikuamka asubuhi moja na kuamua kuingia Lebanon”, akisisitiza kuwa haikuwa na chaguo jingine baada ya Hezbollah kuanza kushambulia Israel tarehe 2 Machi. Amesema utawala wa Iran unaendelea kuitumia Hezbollah kama kundi wakala wake ili kuendelea kushambulia maeneo ya kaskazini mwa Israel.

Balozi Danon amesema mashambulizi dhidi ya jamii za kaskazini mwa Israel yameongezeka katika siku za karibuni na kufikia “kiwango kikubwa zaidi cha mashambulizi tangu kusitishwa kwa mapigano mwezi Aprili”. Kwa mujibu wake, kwa wakazi wa kaskazini mwa Israel hakujawahi kuwa na usitishaji wa mapigano wa kweli kwa sababu Hezbollah “haikuwahi kusitisha kabisa” kurusha makombora na ndege zisizo na rubani.

Ameongeza kuwa maelfu ya wanafunzi nchini Israel bado wanalazimika kubaki majumbani kwa sababu mazingira si salama kwao kwenda shule. Akimjibu mwakilishi wa Ufaransa, Danon aliyehoji, “Je, ungesubiri hadi ndege zisizo na rubani zianze kuzunguka juu ya Paris?” akisisitiza kuwa Israel ina wajibu wa kuondoa tishio dhidi ya raia wake.

Je mataifa mengine yameeleza nini kuhusu kinachoendelea Lebanon? Fuatilia taarifa hii ya kwa lugha ya kiingereza iliyoeleza kwa kifupi kila aliyezungumza katika kikao hicho kwa kubofya hapa

Pia unaweza kutazama hapa kikao hicho kilichorusha na Umoja wa Mataifa mubashara

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *