
JUMLA ya timu 36 kutoka Zanzibar zinatarajiwa kushiriki mashindano ya Yamle Yamle Cup 2026 yenye lengo la kutoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao vya soka.
Mwenyekiti wa mashindano hayo, Sadiq Ali amesema timu 24 zinatoka Unguja ambazo ni Alphard, Alqaida, Jang’ombe, Kajengwa, Karakana City, Kipungani City, Kundemba, Kwahani, Mahonda, Magomeni City, Mambosasa City na Mazombi.
Nyingine ni Mborimborini, Mfenesini Sports Club, Melitano City, Muembe Makumbi City, Mwene Combine, Nyamanzi City, Pwani Mchangani, Soko la Mwanakwerekwe, Tilalila, Ubinadamu Kazi, Welezo na Yuscom FC.
Kwa upande wa Pemba, timu 12 zitashiriki ambazo ni Alzaar, Kiwani Combine, Kojani Sports Club, Kwale City, Machomane, Mazombi City, Mkoani Sports Club, Ole United, Pochinki City, Shamash United, Team Voxy na Wete City.
Sadiq amesema timu zote zilizokidhi vigezo na kukamilisha taratibu za usajili zimepewa nafasi ya kushiriki, huku akibainisha kuwa baadhi ya timu zilichelewa kuwasilisha fomu zao ndani ya muda uliopangwa na hivyo kukosa nafasi.
Amesema mashindano hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji, kuimarisha maendeleo ya soka Zanzibar na kuibua wachezaji watakaofikia ngazi za juu za mchezo huo.
“Ushiriki wa timu hizi unaendelea kuimarisha dhamira ya mashindano ya kuwaunganisha vijana kupitia michezo na kukuza vipaji vya soka kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar,” amesema.
Alieleza kuwa mchakato wa usajili ulikuwa wazi na wa haki kwa timu zote, huku ushiriki ukizingatia utekelezaji wa masharti yaliyowekwa na waandaaji. Sadiq amesema awali kulikuwa na mpango wa kushirikisha timu 10 kutoka Pemba, lakini kutokana na mazingira yaliyokuwepo zikaongezwa mbili baada ya wadau kujadiliana na kukubaliana kabla ya kufungwa kwa usajili. Aliongeza kuwa licha ya kuwepo kwa maoni tofauti kuhusu idadi ya timu zinazoshiriki, lengo kuu ni kupanua fursa kwa vijana na kukuza vipaji vya michezo nchini.
Sadiq amesema mashindano hayo yanalenga kuwapa nafasi wachezaji, hususani wale wasiopata fursa katika mashindano makubwa, kuonyesha uwezo wao na kuchangia maendeleo ya soka nchini.