
Miongoni mwa waliowapokea walinda amani hao kutoka Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS ni Bibiana Dimitri, ambaye hakuficha mshangao wake.
“Mmewezaje kufika huku?” alihoji huku akieleza kuwa wakazi wengi walikuwa wamepoteza matumaini ya kupata msaada kutoka nje kutokana na hali ngumu ya eneo hilo.
“Wakati mwingine ni rahisi kuhisi kana kwamba dunia imetusahau. Tulipokuwa karibu kukata tamaa kabisa, ghafla tuliona magari haya yakija,” alisema.
Barabara inayounganisha Ezo na mji wa Yambio, kitovu kikuu cha jimbo hilo, imeharibika kwa miaka mingi kutokana na mvua na ukosefu wa matengenezo. Hali hiyo imezuia usafirishaji wa bidhaa muhimu, ikiwemo dawa na vifaa vya afya wakati ambapo eneo hilo linakabiliwa na ongezeko la wagonjwa wa mpox.
Hali ni mbaya kuliko matarajio
Baada ya safari ngumu ya kilomita 180, kiongozi wa doria ya UNMISS, Meja Pie Claude Sezikeye, alisema hali waliyoikuta ilikuwa mbaya zaidi kuliko walivyotarajia.
“Tulijua kuwa kulikuwa na changamoto za kibinadamu, lakini hatukujua kwamba hali ilikuwa mbaya kiasi hiki,” alisema.
Kwa wakazi wengi, changamoto za usalama na ukosefu wa huduma muhimu zimeacha majeraha makubwa. Mariata John, mama wa watoto sita anayewalea pia yatima wanne, alikimbia machafuko yaliyotokea huko Tambura miaka michache iliyopita. Mume wake aliuawa katika vurugu hizo.
“Hakukuwa na jambo lolote ambalo ningeweza kufanya. Sasa nina hofu kwamba sitamudu kuwahudumia watoto wangu na kuhakikisha afya na ustawi wao,” alisema akiwa nje ya makazi yake yaliyotengenezwa kwa karatasi za plastiki zilizochakaa.
Afisa wa ufuatiliaji wa afya wa Kaunti ya Ezo, Abraham Danadiri, ametoa wito kwa UNMISS kuwasilisha taarifa ya hali halisi waliyoishuhudia kwa serikali na wadau wengine wa masuala ya kibinadamu.
“Tafadhali fikisheni mliyoyaona kwa Wizara ya Afya na mashirika yanayoweza kusaidia. Tunahitaji msaada kwa dhati,” alisema.
Walinda amani hao wameahidi kurejea tena katika eneo hilo na kufuatilia mahitaji yaliyobainishwa.
Wakati msafara wao ukiondoka, Bibiana aliwaaga kwa maneno yaliyoonesha shukrani za jamii nzima. “Bado sijui mmewezaje kufika huku, lakini najua ujio wenu unaonesha jinsi mnavyojali watu wa eneo hili,” alisema.