Katika taarifa yake kutoka London Uingereza, Dominguez amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na taarifa zinazoonesha kuwa baadhi ya meli zinaendelea kujaribu kupita katika Mlango bahari wa Hormuz huko Mashariki ya Kati bila kuwa na uhakika wa usalama, licha ya hatari zinazojulikana na matukio ya hivi karibuni yaliyosababisha baadhi ya mabaharia kuuawa, kujeruhiwa na wengine kuzuiliwa.
“Wasiwasi wangu mkubwa ni usalama na maisha ya mabaharia wanaowekwa katika mazingira haya. Hawapaswi kupelekwa katika hali ambayo hatari zake zinajulikana, ni kubwa na haziwezi kudhibitiwa” amesema.
Ameongeza kuwa hali ya sasa bado ni tete na hakuna dhamana za kuaminika za usalama, hivyo njia salama ya kupita haiwezi kusemwa kuwa ipo.
Katibu Mkuu huyo amekumbusha kuwa nahodha wa meli na kampuni inayomiliki au kuendesha meli wanabeba wajibu wa mwisho wa kupanga safari na kufanya tathmini za kina na za kweli za hatari, kwa kuzingatia mifumo iliyowekwa ya usimamizi wa usalama na ulinzi.
Mkuu huyo wa IMO ametoa wito kwa wadau wote kuchukua hatua kwa kiwango cha juu cha uwajibikaji na kujiepusha na vitendo vinavyowaweka mabaharia raia wasio na hatia katika hatari. “Ulinzi wa maisha ya mabaharia lazima ubaki kuwa kipaumbele kikuu wakati wote,” amesisitiza.