Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Marta Pobee, amewasilisha taarifa kuhusu shughuli za (UNOCA). Amebainisha mafanikio kadhaa, yakiwemo kufanyika kwa uchaguzi katika baadhi ya nchi na kuimarika kwa shughuli za ECCAS jumuiya kuu ya ushirikiano wa kikanda (Afrika ya Kati).

Hata hivyo, amesema mafanikio hayo yanafifishwa na mwenendo unaotia wasiwasi wa kuongezeka kwa changamoto za usalama, kuzorota kwa hali ya kibinadamu, matatizo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kuongezeka kwa vikwazo dhidi ya haki za kiraia na kisiasa.

Kwa mujibu wa Pobee, maeneo mawili yanayoibua wasiwasi mkubwa kwa sasa ni mashariki mwa Chad na eneo la Bonde la Mto Chad, ambako migogoro na ukosefu wa utulivu vinaendelea kushamiri.

Janga la kibinadamu linaongezeka

Vita vinavyoendelea nchini Sudan sasa vinaingia mwaka wake wa nne. Tangu Aprili 2023, zaidi ya wakimbizi 900,000 kutoka Sudan na takriban raia 300,000 waliorejea Chad wameingia nchini Chad, hali inayoongeza mzigo mkubwa kwa rasilimali za nchi hiyo na kuzidisha janga la kibinadamu lililokuwepo tayari.

Wakati huo huo, wakazi wa Cameroon na Chad wanaendelea kukumbwa na mashambulizi kutoka kwa makundi yenye uhusiano na Boko Haram pamoja na makundi yaliyotengana nayo, ambayo hutumia udhaifu wa uwepo wa serikali katika maeneo ya mipakani.

Pobee alisisitiza kuwa Kikosi kazi cha pamoja kinachojumuisha wanajeshi kutoka Benin, Cameroon, Nigeria na Chad, kinaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kukabiliana na tishio la makundi yenye msimamo mkali katika Bonde la Ziwa Chad.

Wasiwasi kuhusu haki za kiraia

Pamoja na hayo, Pobee ameonya kuwa matumizi ya nguvu za kijeshi pekee hayawezi kutatua chanzo cha migogoro hiyo. Ametoa wito kwa washirika wa kimataifa na taasisi za kifedha za maendeleo kuunga mkono zaidi mipango ya ushirikiano wa kuvuka mipaka inayoratibiwa na Tume ya Bonde la Ziwa Chad.

Ameeleza pia wasiwasi mkubwa kuhusu kupungua kwa nafasi ya mashirika ya kiraia kufanya kazi katika baadhi ya nchi za Afrika ya Kati.

“Kuna mwenendo unaotia wasiwasi wa kuongezeka kwa vikwazo dhidi ya haki za kiraia na kisiasa katika maeneo kadhaa ya Afrika ya Kati,” amesema.

Ameonya kuwa ikiwa hali hiyo haitabadilishwa, inaweza kusababisha kupungua zaidi kwa nafasi ya wananchi kushiriki katika masuala ya umma, kudhoofisha utulivu wa muda mrefu na kuongeza hatari ya kuzuka kwa migogoro mipya katika siku zijazo.

© MINUSCA Walinzi wa amani UN wakiwa kwenye doria nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Kwa nini ni muhimu

Wajumbe wa Baraza la Usalama wameonya kuwa athari za migogoro kuanzia Sudan na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ugaidi, majanga ya kibinadamu, shinikizo la mabadiliko ya tabianchi na milipuko ya magonjwa, ikiwemo Ebola, vinakutana na kuunda tishio kubwa kwa utulivu wa kanda nzima. Wengi wao pia wameeleza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa vikwazo dhidi ya uhuru wa kisiasa na ushiriki wa wananchi katika masuala ya kiraia.

Hitimisho

Diplomasia, ushirikiano wa kikanda katika masuala ya usalama na msaada wa kibinadamu vinaendelea kuwa muhimu katika kukabiliana na changamoto hizo. Hata hivyo, wajumbe wamesisitiza kuwa hatua za kijeshi pekee haziwezi kuleta utulivu wa kudumu bila maendeleo ya kijamii na kiuchumi, utawala wa kidemokrasia na uungwaji mkono endelevu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *