DAR City na Veins BC ndizo zinazoongoza kwa kuwa na nyota wazawa wengi ziliowasajili katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) 2026, jambo linaloonyesha kwamba nje ya uwanja zimeonyesha kutoa kipaumbele kwa vijana wa Kitanzania.

Veins BC inayoshiriki ligi hiyo kwa mara ya kwanza ilimsajili Ronaldo Kisobwe (JKT), Alex Muyanda (UDSM Outsiders) na Said Habibu (Kurasini Heat). Wengine ni Ishrak Khamisi (Pazi), Jordan Manang (JKT), Meshack Itenda (ABC), Alex Bwana (Dar City) na Englibert Machumu (KIUT).

Wachezaji hao wote ni wazoefu BDL na katika msimu uliopita walichezea timu walizotoka ambako wal-ikiwasha kwelikweli.

Kwa upande wa Dar City, licha ya kuwa na nyota wa kimataifa waliowasajili, pia ilisajili nyota wazawa ambao ni Sisco Ngaiza, Jonas Mushi, Evans Davies na Felix Luhamba waliotokea Stein Warriors, pamoja na Fotius Ngaiza aliyekuwa Vijana ‘City Bulls’.

Wazawa waliokuwapo tangu mwaka jana ni Haji Mbegu, Ally Abdallah, Amin Mkosa, Robert Shilla, Jamal Salum, Emmanuel Manyonyi na Mhangachi Atibu.

Uzoefu mkubwa walioupata wachezaji hao wazawa ulitokana na kushiriki mashindano ya Ligi ya Afrika (BAL) nchini Afrika Kusini pamoja na robo fainali ya BAL nchini Rwanda.

Wakati huo, Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) inatarajiwa kuendelea leo (Ijumaa) kwa michezo minne katika Uwanja wa Don Bosco, Upanga. Ratiba iliyotolewa na Kamishna wa Ufundi na Mashindano wa BDL, Shabani Mahobonya, inaonyesha kuwa mchezo wa kwanza utakuwa kati ya UDSM Queens na Real Dream.

Michezo mingine itakuwa kati ya Magone BC na Dar City, Srelio na Mchenga Stars, huku mchezo wa mwisho ukiwa kati ya Veins BC na Vijana ‘City Bulls’. Mchezo kati ya Veins BC na Vijana ‘City Bulls’ una-tarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora wa wachezaji wa timu hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *