
Leo ni Jumapili 28 Mfunguo Tatu Dhulhija 1447 Hijria sawa na 14 Juni 2026.
Tarehe 28 Dhulhija siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita, yaani miaka miwili baada ya harakati na mapambano ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) katika ardhi ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria, kulijiri tukio la Harrah.
Mwaka huo watu wa mji mtukufu wa Madina waliokuwa wamechoshwa na dhulma na ukatili wa mtawala Yazid bin Muawiya, walimfukuza gavana wake mjini humo Marwan bin Hakam. Baada ya tukio hilo Yazid alituma jeshi likiongozwa na mtumishi wake mmwaga damu na mtenda dhulma Muslim bin Uqbah katika mji mtakatifu wa Madina na kuliamuru kufanya mauaji makubwa mjini humo na kupora mali.
Mauaji kama hayo hayakuwahi kushuhudiwa katika historia ya zama za awali za Uislamu na wanahistoria wamesema kuwa Waislamu zaidi ya elfu kumi wakiwemo maswahaba wa Mtume, waliuawa katika shambulizi hilo. Vitabu vya historia pia vinasema utawala wa Yazid bin Muawiya ulihalalisha mji wa Madina kwa askari wake kwa muda wa siku tatu na kwamba wasichana na wanawake wa maswahaba walinajisiwa katika tukio hilo. *****
Katika siku kama ya leo miaka 290 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa kwa jina la Charles Augustin de Coulomb.
Msomi huyo alianza kufundisha masomo katika nyanja za umeme na sumaku baada ya kuhitimu masomo yake na kuandika vitabu vingi katika uwanja huo.
Mbali na kufundisha, mwanafizikia Augustin de Coulomb aliendelea pia kufanya utafiti na hatimaye akafanikiwa kubuni kanuni katika sayansi ya fizikia iliyojulikana kwa jina lake. De Coulomb aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70. ***
Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Kamanda Muhammad Ali Pasha waliishambulia Sudan na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Wakati huo huo Waingereza pia walilishambulia eneo la kusini mwa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Hata hivyo wananchi wa Sudan wakiongozwa na Mahdi al Sudani mwaka 1881 walianzisha harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Misri na Uingereza na mwaka 1885 wakafanikiwa kutoa pigo kubwa kwa vikosi vamizi vya Misri na Uingereza na kuyakomboa maeneo hayo. ***
Miaka 196 iliyopita katika siku kama ya leo wanajeshi wa Ufaransa waliwasili katika pwani ya Algeria huko kaskazini mwa Afrika.
Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa oparesheni za kijeshi za Ufaransa zilizokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria. Hata hivyo uvamizi huo wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria ulikabiliwa na mapambano makubwa ya wananchi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa.
Mapambano hayo ya kupigania ukombozi ya wananchi wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa yalipamba moto baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia.
Hatimaye mwaka 1962 Rais wa wakati huo wa Ufaransa alilazimika kuipatia Algeria uhuru kamili kufuatia mashinikizo ya mapambano ya wananchi wa Algeria na upinzani wa fikra za waliowengi ndani ya Ufaransa kwenyewe na kimataifa. ***
Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, alifariki dunia Hadi Sabzavari au Hajj Mulla Hadi Sabzavari, mmoja wa maulama na wanafalsafa wakubwa wa karne ya 13 Hijiria.
Mulla Hadi Sabzavari alizaliwa mwaka 1212 Hijiria ambapo umri wake ulijaa baraka, huku mwishoni mwa maisha yake akijawa na izza ya nafsi, zuhdi na ucha-Mungu. Athari za Mulla Hadi Sabzavari zinaonyesha kwamba, alimu huyo mkubwa wa Waislamu mbali na kwamba alikuwa mmoja wa wanafalsafa wakubwa, pia alitabahari katika elimu ya sheria za Kiislamu (fiq’hi), tafsiri ya Qur’ani, mantiki, hisabati, fasihi na elimu ya tiba. Aidha Mulla Hadi Sabzavari pia alikuwa malenga mtajika. Katika uwanja huo, alikuwa akitunga mashairi ambayo yalifungamana na maqsuala ya kifalsafa na elimu ya irfani.
Miongoni mwa athari za mwazuoni huyo ni pamoja na ‘Mandhumah’ katika elimu ya mantiki, ‘Asraarul-Hikami’ na ‘al-Jabru wal-Ikhtiyaar.’ ****
Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita mto mrefu na mkubwa zaidi wa Asia wa Yangtze Kiang ulivunja kingo zake na kusababisha mafuriko ya kutisha.
Mvua kali za msimu zilizonyesha zilisababisha mawimbi na mafuriko makubwa yaliyovunja kingo na mabwawa yote ya kandokando ya mto huo. Maji hayo yaligubika ardhi ya majimbo 8 ya China.
Inasemekana kuwa tukio hilo kubwa liliathiri karibu watu milioni 50 wakiwemo waliopoteza maisha, kupoteza makazi, uharibifu wa mashamba, wale waliofariki dunia kutokana na maradhi ya aina mbalimbali na kadhalika. ***
Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, Wajumbe 120 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliwasilisha hoja ya kutokuwa na ustahiki wa kuongoza nchi Rais Bani Sadr.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya muqawama wa wananchi dhidi ya uvamizi wa Wanajeshi wa Baathi wa Iraq katika mipaka ya vita dhidi ya Iran kuanza kusambaratika kutokana na kukosa uungwaji mkono wa lazima kutoka kwa Bani Sadr kama Amiri Jeshi Mkuu, na kufikia kilele hitilafu za Rais na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Idara ya Mahakama na taasisi za kimapinduzi zilifikia kilele chake.
Baada ya kupasishwa hoja hiyo katika Bunge uamuzi huo uliwasilishwa kwa Imam Khomeni ambaye naye aliudhinisha na hivyo Bani Sard akaondolewa katika wadhifa wa urais. Kuondolewa Bani Sadr, kulipelekea kung’olewa moja ya mizizi mikuu ya njama na hitilafu za ndani na Bani Sadr akakimbia nchi na kuomba hifadhi nchini Ufaransa.