Katika eneo hili la makazi yasiyo rasmi au mtaa wa mabanda ambapo, nyingi zikijengwa kwa mabati ya zamani yenye kutu, likiwa maskani ya takriban watu 200,000 kuna kituo cha urejelezaji. Ndani ya kituo hicho, maboksi yaliyofungwa kwa kamba na magunia makubwa yaliyosheheni taka yamesimama kama kuta. Katikati ya mrundikano huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, akiambatana na ujumbe wake na waandishi wa habari wenye kamera, wanakagua hatua kwa hatua namna ambavyo taka hizi zinapewa thamani mpya.

Ziara hiyo ilifanyika Juni 10, katika kituo cha MRF kilichopo jijini Nairobi, Kenya. Kituo hiki ni cha kwanza cha aina yake kujengwa kwenye makazi yasiyo rasmi jijini humo, kikilenga kuleta mabadiliko yanayoongozwa na jamii yenyewe. Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Italia na kutekelezwa na taasisi ya AVSI Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), Halmashauri ya Jiji la Nairobi, na shirika lisilo la kiserikali, Miss Koch Kenya.

© UNIS Nairobi Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock (katikati), amefanya ziara ya kihistoria nchini Kenya kwenye kituo cha kukusanya, kuchakata na kurejeleza taka cha Korogocho (Korogocho Material Recovery Facility – MRF) kujionea namna vijana wanavyogeuza taka kuwa fursa ya kiuchumi na silaha ya kutokomeza umasikini na uhalifu mitaani.

Akiwa kituoni hapo, Annalena Baerbock ameshuhudia namna miradi ya mazingira inavyotumika kama nguzo ya kudumisha amani na utulivu miongoni mwa vijana katika maeneo hatarishi, huku akidadisi kwa maelezo zaidi, kisha akatoa hotuba inayolenga kuhamasisha amani na utatuzi wa migogoro ili kulinda usalama wa kimataifa.

“Chata ya Umoja wa Mataifa si jambo la hiyari, bali Chata ya Umoja wa Mataifa iko wazi kabisa: kila nchi mwanachama inapaswa kutatua migogoro yao ya kimataifa kwa njia ya amani kwa namna ambayo amani, usalama, na haki za kimataifa hazitakuwa hatarini.”

Kauli hiyo inaungwa mkono na viongozi wa mradi huo, ambao wameeleza kuwa uwepo wa miradi ya mazingira kama uboreshaji wa Mto Nairobi na kituo hiki cha kurejeleza malighafi umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza viwango vya uhalifu, kudumisha utulivu na matumizi ya dawa za kulevya. Mwenyekiti wa muungano wa vikundi vya jamii yaani, CBOs, Joffrey Otieno, amefafanua kuwa kituo kinasaidia kurasimisha kazi za wakusanya taka na kinajumuisha mradi wa majaribio wa nzi weusi (Black Soldier Fly) unaochakata. taka kuwa mbolea na chakula cha mifugo. 

“MRF ni kituo cha kurejeleza malighafi, ambacho kinakusanya taka zote zinazoweza kurejelezwa na kuziuza tena kwa makampuni ya urejelezaji ili kuepuka uchafuzi wa mazingira. Tuliona kwamba tunahitaji kufanya mabadiliko kwenye mazingira kwa sababu kwenye eneo letu la bustani, kulikuwa na uchafuzi wa mazingira kutoka mtoni, plastiki nyingi zikitoka maeneo mengine tofauti, na zilikuwa zikiziba kwenye bustani yetu. Kwa hiyo, kimsingi, kikundi chetu, tuliiona hii kama fursa ya kufanya mazingira kuwa safi na kutengeneza kipato kwa kikundi kwa kukusanya plastiki na kuziuza tena kwa wakusanyaji wakubwa.”

Raymond Kimeu, mwenye umri wa miaka 32 na baba wa familia, amebainisha kuwa kituo kimewapatia ajira na kuwaingizia kipato kinachosaidia kulisha familia zao na kusomesha watoto, huku kikiepusha vijana wengi kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya.

“Tangu mradi huu uje umeweza kutupa mapato na sasa tunaweza kulisha hadi familia zetu. Nina mke na watoto wawili na watatu yupo njiani, mke ana ujauzito wa miezi mitano. Watoto wangu wanaenda shule, naweza kutoa pesa hapa kwa huu mradi na niweze kuwalipia ada na pia mradi umenisaidia naweza kujikimu kimaisha na kimahitaji.”

© UNIS Nairobi Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, alifanya ziara ya kihistoria nchini Kenya kwenye kituo cha kukusanya, kuchakata na kurejeleza taka cha Korogocho (Korogocho Material Recovery Facility – MRF) kujionea namna vijana wanavyogeuza taka kuwa fursa ya kiuchumi na silaha ya kutokomeza umasikini na uhalifu mitaani.

Mbali na vijana wa kiume, mradi huo umewajengea ushujaa wanawake wa Korogocho ambao hapo awali walisita. Mmoja wao, ni Mercy Atieno, mwenye umri wa miaka 35 na mama wa watoto watano, kazi hiyo imemsaidia kujishughulisha na kujiepusha na vishawishi hatarishi vya mitaani tangu alipofiwa na mumewe.

“Mwanzo nilianza na kubeba takataka za majumbani. Naweza sema kuingia majumbani ilikuwa ni tatizo sababu kupata msichana aingie kwenye kazi ya takataka si rahisi. Sasa… niliolewa lakini mume akafariki dunia, nikajipa ushujaa wa kuingia kufanya kazi ya takataka. Nikaanza kukusanya takataka kwenye kikundi, na hicho kikundi ndio kimenishikilia nikaona kumbe kazi ya takataka inaweza kunilelea watoto, inaweza kunitoa kwenye mambo mengi. Lakini tangu niingie, najikuta kila saa nipo kazini. Jamii ya Korogocho inafurahia sababu huduma zetu ziko vizuri.”

Baada ya kuonesha mazingira ya kituo hicho, Joffrey Otieno anatuma ujumbe kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akieleza changamoto wanazokabiliana nazo wakiwa vijana kumi, wanaofanya kazi kwa kujitolea.

“Hapa MRF changamoto yetu kubwa, ni tatizo la kifedha. Kwa sababu kama tungekuwa tunafadhiliwa vizuri, tungeweza kuajiri watu wengi iwezekanavyo na kununua bidhaa nyingi zaidi zinazoweza kurejelezwa na kuzigeuza kuwa fedha ili kuwalipa watu wanaofanya kazi hapa. Na pia, changamoto yetu kubwa katika eneo letu, nafikiri watu hawana uelewa mkubwa kuhusu miradi mingi ya serikali. Kwa hiyo tukiwekeza zaidi kwenye uelewa, watapokea programu zote na miradi yote ambayo serikali na washirika wetu wa kimataifa wanakuja nayo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *