Miaka mitano iliyopita, haikuwa jambo la ajabu kutembea katika mitaa ya Kariakoo jijini Dar es Salaam na kusikia ngurumo za jenereta karibu kila kona.
Maduka ya jumla, maghala, karakana, viwanda vidogo na hata ofisi nyingi zilikuwa na jenereta kama sehemu ya kawaida ya shughuli za kila siku. Kukatika kwa umeme kulimaanisha uzalishaji kusimama, biashara kuchelewa na gharama za mafuta kuongezeka.
Leo, hali hiyo imebadilika kwa kiasi kikubwa.
Jenereta bado zipo, lakini katika maeneo mengi zimebaki kama vifaa vya dharura badala ya kuwa sehemu ya kawaida ya biashara.
Kukatika kwa umeme bado hutokea, lakini si kwa kiwango na muda uliokuwa ukizoeleka miaka michache iliyopita. Katika maeneo mengi ya biashara, sauti zilizokuwa zikitawala mitaa zimepungua na nafasi yake kuchukuliwa na shughuli za kawaida za uchumi.
Mabadiliko hayo hayaonekani Kariakoo pekee. Yanaonekana katika viwanda vinavyozalisha kwa uhakika zaidi, katika hospitali zinazotoa huduma bila hofu ya kukatika kwa umeme, katika shule zinazotumia teknolojia za kidijitali na katika vijiji vya pembezoni vilivyopata umeme kwa mara ya kwanza.
Kwa kifupi, hadithi ya miaka mitano ya sekta ya nishati nchini Tanzania si hadithi ya nguzo, nyaya na transfoma pekee. Ni hadithi ya jinsi uwekezaji katika umeme ulivyoanza kubadilisha uchumi.
Takwimu za Wizara ya Nishati zinaonesha kuwa uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini umeongezeka kutoka megawati 1,601.84 mwaka 2020/21 hadi megawati 4,522.54 mwezi Machi 2026. Hii ni sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 180 ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Katika kipindi hicho hicho, idadi ya wateja wa TANESCO imeongezeka kutoka takribani milioni 3 mwaka 2021 hadi zaidi ya milioni 5.3 mwaka 2026. Vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vimefikiwa na huduma ya umeme huku zaidi ya asilimia 52 ya vitongoji tayari vikiunganishwa na gridi ya taifa.
Kwa maneno mengine, miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa kipindi ambacho Tanzania imeongeza uzalishaji wa umeme, kupanua upatikanaji wa huduma na kuanza kutumia nishati kama nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi.
Nishati yageuka Kipaumbele cha Taifa
Katika mwaka wa fedha 2026/27, Bunge lilipitisha bajeti ya Sh trilioni 2.53 kwa ajili ya Wizara ya Nishati na taasisi zake. Kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh trilioni 2.46 sawa na asilimia 97.5 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Uwiano huo unaonesha nafasi ambayo sekta ya nishati imepewa katika ajenda ya maendeleo ya taifa.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni, Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi alisema Tanzania imeendelea kuwekeza katika vyanzo mbalimbali vya nishati ili kuhakikisha usalama wa upatikanaji wa umeme kwa maendeleo ya uchumi.

“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ikiwemo maji, gesi asilia, jua, upepo, jotoardhi na urani vinavyotuwezesha kuwa na uhakika wa nishati kwa maendeleo ya Taifa,” alisema.
Katika maono ya muda mrefu, Serikali inalenga kufikisha uwezo wa uzalishaji wa umeme hadi megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 na megawati 70,000 ifikapo mwaka 2050.
Kwa wataalamu wa uchumi, uwekezaji huo si uwekezaji wa sekta ya nishati pekee. Ni uwekezaji katika sekta zote zinazotegemea nishati kuendesha shughuli zao.
Mradi Uliobadili Hesabu za Umeme
Hakuna mradi uliobadili taswira ya sekta ya umeme nchini kama Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).
Mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 na gharama inayokadiriwa kufikia zaidi ya Sh trilioni 6.5 ni mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme kuwahi kujengwa nchini.

Machi 2024, mtambo wa kwanza wenye uwezo wa megawati 235 ulianza kuzalisha umeme. Kufikia Aprili 2025, mitambo yote tisa ya mradi huo ilikuwa imekamilika na kuunganishwa katika gridi ya taifa.
Rais Samia Suluhu Hassan ameueleza mradi huo kama uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa viwanda, biashara na huduma za kijamii.
Kwa wataalamu wa nishati, JNHPP ndiyo sababu kubwa iliyowezesha Tanzania kuvuka kiwango cha megawati 4,000 kwa mara ya kwanza katika historia yake.
Lakini thamani ya mradi huo haiishii kwenye takwimu za uzalishaji pekee.
Thamani yake inaonekana katika kupungua kwa gharama za uzalishaji, kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji na kuongezeka kwa uwezo wa nchi kuhudumia mahitaji ya sekta ya viwanda.
REA na Mwanga wa Maendeleo Vijijini
Wakati JNHPP ikiongeza uzalishaji wa umeme, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kubadili maisha ya wananchi katika maeneo ya vijijini.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara.
Safari hiyo ilianza kupitia utekelezaji wa REA III ambapo maelfu ya vijiji, vitongoji na taasisi za umma ziliunganishwa na umeme.
Mbali na kaya, shule, vituo vya afya na miradi ya maji imeendelea kuunganishwa na huduma hiyo. Katika mwaka 2023/24 pekee, vituo vya afya 66 na pampu za maji 333 viliunganishwa na umeme.
Mwaka 2025, zaidi ya asilimia 52.3 ya vitongoji nchini vilikuwa tayari vimeunganishwa na huduma hiyo huku utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Umeme Vijijini ukiendelea katika maeneo yaliyobaki.
Athari za uwekezaji huo zinaonekana katika maeneo mengi ya nchi.
Katika Kitongoji cha Kisendema wilayani Namtumbo, mwakilishi wa vijana Athumani Sadik alisema ujio wa umeme umefungua fursa za uchomeaji, useremala na biashara ndogo ndogo.
“Umeme umetuletea fursa ambazo zamani zilionekana kama ndoto. Vijana wengi sasa wanaona uwezekano wa kujiajiri badala ya kusubiri ajira rasmi,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Allan Njiro, amewataka wananchi kulinda miundombinu ya umeme ili iendelee kuwanufaisha kwa muda mrefu.
Umeme na Uchumi wa Wananchi
Kwa wafanyabiashara wengi, athari za maboresho ya sekta ya umeme zinaonekana moja kwa moja katika gharama za uendeshaji.
Mariam Omari, mfanyabiashara wa bidhaa za matumizi ya nyumbani Kariakoo, anasema miaka michache iliyopita jenereta lilikuwa sehemu ya lazima ya biashara yake.
“Tulikuwa tunatumia fedha nyingi kwa mafuta. Leo jenereta lipo lakini mara nyingi linabaki kama tahadhari tu. Hiyo imepunguza gharama za biashara kwa kiasi kikubwa.”
Katika eneo la Tegeta, mmiliki wa karakana ya useremala, Juma Mkwizu, anasema uhakika wa umeme umeongeza uwezo wake wa kuzalisha, hali ambayo binafsi nimeipa jina la kutoka ngurumo za jenereta madukani, hadi milio sikivu ya AC.
“Kabla ya hapo ungepanga kazi ya siku nzima halafu ukapoteza muda mwingi kwa sababu ya umeme. Leo changamoto zipo lakini si kwa kiwango kile.”
Kwa wanawake wengi wa vijijini, umeme umefungua fursa mpya za usindikaji wa mazao, biashara za chakula, ushonaji na uhifadhi wa bidhaa.
Dk Victoria Kisyombe, mwanzilishi wa SELFINA na mmoja wa vinara wa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi nchini, amekuwa akisisitiza kwamba maendeleo ya kiuchumi huanza pale watu wanapopata zana za uzalishaji.
Katika maeneo mengi ya Tanzania, umeme umeanza kuwa moja ya zana hizo muhimu za uzalishaji.
Kutoka Mwanga Hadi Nishati ya Kisasa
Pengine ishara kubwa zaidi ya mabadiliko ya sekta ya nishati nchini si ongezeko la megawati pekee bali kupanuka kwa matumizi ya umeme.
Mwaka 2026, TANESCO ilizindua vituo vya kuchajia magari yanayotumia umeme pamoja na mpango wa kukopesha majiko ya umeme kwa wananchi kupitia mfumo wa On-Bill Financing.
Akizindua mpango huo, Waziri Ndejembi alisema:
“Hatua hii inapanua matumizi ya umeme kutoka kupikia hadi usafiri, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, kupunguza gharama za maisha na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.”
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowelle, alisema mpango huo utasaidia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuwa wananchi wataweza kulipa gharama za majiko kidogokidogo.
Hii ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Mapinduzi ya Kidijitali
Miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita haikuishia kwenye uzalishaji na usambazaji wa umeme. Imehusisha pia matumizi ya teknolojia.
Mwaka 2025, TANESCO ilizindua mita janja kwa wateja wake na mwaka uliofuata ikaanza kutumia ndege nyuki (drones) katika ukaguzi wa miundombinu ya umeme.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa teknolojia hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, alisema: “Leo tumeanza safari ya mapinduzi ya teknolojia ya kuturahisishia kufanya kazi zetu.”
Kwa mujibu wake, TANESCO sasa inasimamia zaidi ya kilomita 8,500 za njia za kusafirisha umeme na karibu kilomita 200,000 za njia za kusambaza umeme nchini.
Matumizi ya teknolojia hizo yanatarajiwa kuboresha ufanisi wa huduma, kupunguza muda wa kubaini hitilafu na kuongeza ubora wa huduma kwa wateja.
Urithi wa Miaka Mitano

Mwaka 2021, Tanzania ilikuwa na megawati 1,601 za umeme, takribani wateja milioni 3 wa TANESCO na maelfu ya wananchi ambao bado hawakuwa wamefikiwa na huduma ya umeme.
Mwaka 2026, nchi ina zaidi ya megawati 4,500 za umeme, zaidi ya wateja milioni 5.3 wa TANESCO na vijiji vyote Tanzania Bara vimefikiwa na huduma hiyo. Miaka mitano iliyopita Tanzania ilikuwa ikijadili jinsi ya kufikisha umeme kwa wananchi.
Leo Tanzania inajadili jinsi ya kutumia umeme huo kuendesha viwanda, magari, teknolojia, uwekezaji na uchumi wa kidijitali. Hiyo ndiyo tofauti kati ya taifa linalotafuta umeme na taifa linalotumia umeme kujenga uchumi.
Kutoka kwenye mingurumo ya jenereta za Kariakoo hadi mitambo ya megawati 2,115 ya Julius Nyerere, kutoka vijiji visivyokuwa na umeme hadi vijiji vyote 12,318 kufikiwa, na kutoka wateja milioni 3 hadi zaidi ya milioni 5.3 wa TANESCO, hadithi ya miaka mitano iliyopita si hadithi ya nyaya na transfoma pekee.