Akizungumza katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Naibu Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Awa Dabo, ameeleza jinsi usumbufu wa usafirishaji katika njia nyembamba ya bahari ya Ghuba pamoja na vizuizi vya kijeshi vya majini vya Marekani dhidi ya meli zinazotumia bandari za Iran ulivyovuruga mtandao wa usambazaji wa nishati duniani.

Mgogoro huo umeathiri kwa kiasi kikubwa usafiri wa anga na kuzuia mtiririko wa misaada ya kibinadamu, hali iliyosababisha matatizo makubwa zaidi yanayoendelea kuwaathiri watu katika eneo hilo na kwingineko duniani.

Upungufu wa mbolea pia umetajwa kuwa changamoto nyingine inayoongeza wasiwasi.

“Wataalamu wa uchumi wanaonya kuwa ikiwa Mlango Bahari wa Hormuz hautafunguliwa, baadhi ya nchi zenye uchumi dhaifu zaidi duniani zinaweza kutumbukia katika machafuko, jambo litakaloongeza umaskini na njaa kwa mamilioni ya watu,” amesema Naibu Kamishna Mkuu Dabo.

© Unsplash/Planet Volumes Mlango wa bahari wa Hormuz kati ya Iran na Oman.

Kinga dhidi ya mgogoro wa chakula duniani

Akitoa taarifa kuhusu athari za mashambulizi ya Iran dhidi ya Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE) na Jordan, Dabo amesisitiza kuwa angalau mashirika maalumu ya Umoja wa Mataifa, yakiwemo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), lazima yawezeshwe kwa rasilimali zinazohitajika ili kuzuia mgogoro wa uhakika wa chakula unaotabiriwa kutokea duniani.

UAE yatumaini mazungumzo yatakomesha mashambulizi

Naye Mwakilishi wa Kudumu wa Falme za Kiarabu katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Jamal Al Musharakh, aesema ana matumaini kuwa mazungumzo yanayoendelea kuhusu mgogoro wa Mashariki ya Kati yatawezesha kusitishwa kwa mashambulizi.

Tangu tarehe 28 Februari, UAE imekumbwa na zaidi ya mashambulizi 3,000 ya makombora ya balistiki, makombora ya masafa marefu na ya ndege zisizo na rubani au droni ameeleza.

Iran yatetea hatua zake

Akikosoa uhalali wa mfumo wa kimataifa wa haki za binadamu katika kuitisha mjadala huo, Balozi wa Iran, Ali Bahreini, amesisitiza kuwa nchi yake ilitumia haki yake ya kujilinda kwa mujibu wa sheria za kimataifa wakati wananchi wa Iran wakikabiliwa na “mashambulizi ya anga yasiyochagua walengwa”.

“Iwapo Iran ilikubali usitishaji mapigano mwishowe, licha ya mapungufu yake na changamoto zilizofuata, imefanya hivyo kwa sababu ya dhamira kubwa ya kuwajibika kwa viongozi wa eneo hili na kwa usalama wa pamoja,” amesema Bahreini.

“Hatimaye tumeweza kumaliza vita ili tusilazimike tena kusikia kishindo cha silaha za kisasa zisizochagua walengwa juu ya shule na wanafunzi,” ameongeza.

Türk aunga mkono makubaliano hayo

Mapema leo, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, amekaribisha taarifa za makubaliano ya amani na kuzitaka pande zote kusitisha mapigano na kujitahidi kufikia usitishaji wa kudumu wa vita.

“Katika kipindi hiki nyeti, pande zote zinapaswa kuonesha kiwango cha juu kabisa cha kujizuia na kufanya kazi ya kuimarisha usitishaji mapigano na kuugeuza kuwa makubaliano ya amani ya kudumu,” amesema Volker Türk mbele ya Baraza la Haki za Binadamu.

Wito huo umefuatia kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye alieleza kuwa tangazo hilo ni “hatua muhimu kuelekea kumaliza mzozo huo.”

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu siku ya Jumapili, makubaliano hayo yanajumuisha usitishaji wa haraka na wa kudumu wa mapigano, kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz na mfumo wa mazungumzo zaidi katika siku zijazo.

Mlango huo wa kimkakati ni njia muhimu ya usafirishaji ambapo takriban asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa duniani hupitia hapo.

© IMO Mabaharia wawili wakiwa kwenye kazi zao melini. (Maktaba)

Wasiwasi kuhusu usalama wa mabaharia

Likizungumzia uwezekano wa mafanikio ya kidiplomasia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kimataifa la Masuala ya Bahari (IMO) limesema hatua hiyo ni muhimu katika kurejesha usalama katika njia hiyo muhimu ya usafiri wa baharini kwa mabaharia na meli, pamoja na kulinda kanuni ya msingi ya uhuru wa usafiri wa majini.

Baada ya vita kuanza tarehe 28 Februari kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel ndani ya Iran, jeshi la Iran lilijibu kwa mashambulizi dhidi ya Israel na nchi washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba.

Wananchi wa Lebanon pia walijikuta wakihusishwa katika vita hivyo baada ya wapiganaji wa Hezbollah walioko nchini humo kuanza kushambulia Israel.

Maelfu wauawa, wakiwemo watoto

Nchini Iran pekee, mashambulizi ya Israel na Marekani yanaripotiwa kusababisha vifo vya maelfu ya raia, “wakiwemo mamia ya watoto, pamoja na kuharibu hospitali, shule, makazi na miundombinu mingine muhimu,” Volker Türk ameliambia Baraza la Haki za Binadamu.

Akizungumzia mauaji ya halaiki ya wanafunzi wengi wa Iran yaliyotokea siku ya kwanza ya vita, mkuu huyo wa haki za binadamu ametaka matokeo ya uchunguzi wa Marekani kuhusu shambulio dhidi ya Shule ya Minab yawekwe wazi kwa umma.

Shambulio hilo linaripotiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 156.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *