DAR ES SALAAM: Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa mafuta ya kula yanayozalishwa kwa kutumia mbegu zinazozalishwa ndani ya nchi unatarajiwa kuongeza uwekezaji, ushindani wa viwanda vya ndani na kuchochea uzalishaji wa mazao ya mafuta nchini.

Hayo yamesemwa na mchambuzi wa uchumi, Marandu Marwa, akizungumzia hatua mpya za Serikali zilizotangazwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema hatua hiyo itawapa motisha wawekezaji kutumia malighafi zinazozalishwa ndani ya nchi kwa kuwa zitawasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza faida.

“Kila mwekezaji ataona kutumia mbegu zinazozalishwa ndani ya nchi kama njia rahisi ya kuongeza faida na kupunguza gharama za kodi. Hii itaongeza ushindani na kuwanufaisha wazalishaji wa ndani,” amesema.

Marwa amesema kwa muda mrefu tofauti ndogo ya ushuru kati ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na zinazozalishwa nchini imekuwa ikidhoofisha ushindani wa viwanda vya ndani na kupunguza hamasa ya uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo.

Kauli hiyo inakuja baada ya Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, kutangaza kuwa Serikali imependekeza kusamehe VAT kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa kwa kutumia mbegu zinazozalishwa ndani ya nchi.

Akiwasilisha bajeti ya Serikali ya Sh62.3 trilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri huyo amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha sekta ya viwanda.

Mbali na msamaha huo, Serikali imeendelea kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 35 au dola za Marekani 300 kwa tani moja ya mafuta safi ya kula (refined edible oil), kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa zaidi.

Pia, Serikali imeandaa kanuni za uagizaji wa mafuta ya kula kwa lengo la kudhibiti uingizaji wa mafuta hayo kutoka nje ya nchi na kuhamasisha ukuaji wa tasnia ya mafuta yanayozalishwa kwa kutumia mbegu za ndani.

Aidha, imependekeza kuanza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ghafi ya soya, karanga, nazi, mnyonyo na haradali, kutoka kiwango cha sasa cha asilimia sifuri.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hiyo inalenga kuoanisha viwango vya ushuru wa mafuta hayo ghafi na vile vya mafuta ghafi ya alizeti, pamba na mahindi ambayo tayari yanatozwa ushuru wa asilimia 10.

Serikali inaeleza kuwa hatua hizo zitasaidia kulinda na kukuza uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kula nchini, kuongeza ajira na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *