Dar es Salaam. Baraza la Wazee la Chadema) (Bazecha) linatarajiwa kukuketi kwa siku mbili mkoani Singida kujadili masuala mbalimbali ya chama na kutoa ushauri kwa viongozi kuanzia ngazi za chini hadi taifa.

Mkutano huo, unaotarajiwa kufanyika Juni 23 hadi 24, 2026, utawakutanisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kukumbushana majukumu yao ya kikatiba, kubadilishana mbinu za usuluhishi wa migogoro na kuhakiki uanachama wa wajumbe kufuatia mabadiliko yaliyojitokeza wakati kilipokuwa hakifanyi shughuli za kisiasa kwa kipindi fulani.

Awali, mkutano huo ulipangwa kufanyika Oktoba 2025 katika Kanda ya Serengeti, lakini uliahirishwa kutokana na zuio la kufanya shughuli za kisiasa lililoikumba Chadema kwa siku 309 kufuatia kesi iliyokuwa ikiendelea mahakamani.

Huo utakuwa mkutano wa kwanza wa ana kwa ana wa baraza hilo tangu wajumbe wake wachaguliwe katika mkutano mkuu wa Chadema uliofanyika Januari 2025.

Singida imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo kama sehemu ya kuonesha mshikamano na kumuenzi Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayeshikiliwa gerezani akikabiliwa na mashtaka ya uhaini.

Akizungumza Dar es Salaam leo Jumatatu Juni 15, 2026, kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Bazecha, Suzan Lyimo, amesema kila kitu kimekamilika na baadhi ya wajumbe tayari wameanza safari kuelekea Singida kushiriki kikao hicho.

 “Siku ya kwanza tutakuwa na mafunzo maalumu yatakayowakumbusha wajumbe majukumu yao ya kikatiba pamoja na kuwajengea uwezo wa kushughulikia migogoro katika jamii,” amesema Lyimo.

Kwa mujibu wake, mafunzo hayo yatatolewa na wataalamu wa masuala ya uongozi na afya ili kuwasaidia wazee kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya na kiuchumi wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku.

Lyimo amesema siku ya pili kutafanyika kikao cha kikatiba kitakachowahusisha wajumbe wanaostahili kwa mujibu wa katiba ya Chadema. “Katika kikao hicho cha kikatiba tutatoka na ushauri wetu kama Baraza kwa viongozi wa chama kama katiba inavyotuelekeza, ikiwemo kuangalia migogoro inayolikabili Taifa ni namna gani viongozi wetu wanapaswa kufanya,” amesema Suzan.

Amesema baada ya mkutano huo wajumbe watapata fursa ya kutembelea familia ya Tundu Lissu kwa ajili ya kutoa salamu za pole na kuonesha mshikamano.

Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo kutoka Zanzibar, Said Hamoud Said, amesema kikao hicho ni muhimu kwa kuwa kitajadili mustakabali wa chama na nafasi ya wazee katika kutoa ushauri kwa uongozi.

“Kama wazee tutatoa ushauri kuhusu masuala mbalimbali ya chama, na mapendekezo yetu yatawasilishwa katika kamati kuu. Hiki ni kikao muhimu kwa maendeleo ya chama chetu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *