Mwanza. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameagiza kusimamishwa kazi mara moja Meneja wa Usambazaji Maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), Mhandisi Ramadhani Mramba, kutokana na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi kuhusu huduma duni ya maji katika baadhi ya maeneo ya jiji la Mwanza.

Aweso ametoa uamuzi leo  huo Jumatatu, Juni 15, 2026, akiwa katika ziara ya ghafla mkoani Mwanza, ambapo alikutana na malalamiko makubwa ya wananchi wa kata za Mecco na Buhongwa kuhusu kukosekana kwa huduma ya maji safi na ya uhakika.

Akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mecco, Wilaya ya Ilemela, waziri huyo alielezwa changamoto za uzembe wa kiutendaji na kusuasua kwa huduma hiyo, hali iliyomlazimu kutoa maagizo ya haraka ya hatua za kinidhamu.

Waziri wa Maji, Juma Aweso akiwa katika ziara ya kikazi katika Chanzo cha Maji cha Butimba, Jijini Mwanza, kukagua miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa maji. Picha na PraiseGod Mgumba

Katika hatua nyingine, Aweso alimtaka Meneja wa Usambazaji Maji wa mkoa kujitokeza katika mkutano huo ili kutoa ufafanuzi, lakini hakufika, hali iliyochangia uamuzi wa kusimamishwa kazi mara moja.

“Sasa naelekeza Katibu Mkuu, Meneja wa Usambazaji Maji asimamiswe mara moja. Haya mambo siyataki. waziri nipo, meneja hayupo, acha nifanye kazi,” amesema Aweso.

Ziara hiyo pia ilimfanya waziri kutembelea kituo cha kusukuma maji cha Capripoint pamoja na chanzo cha maji cha Butimba, ili kujionea hali ya miundombinu na ufanisi wa mitambo.

Chanzo cha maji cha Butimba kilichopo Mkoani Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba.

Aweso pia amezitaka Mwauwasa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha huduma zinatolewa bila migogoro ya kiutendaji, akisisitiza kuwa migongano ya taasisi hizo inawaathiri wananchi moja kwa moja.

“Tanesco na Mwauwasa ni taasisi za Serikali. Inapotokea changamoto lazima mkutane mtafute suluhisho pamoja. Hakuna mafanikio kwa kulumbana,” amesisitiza.

Waziri wa Maji, Juma Aweso akizungumza na wananchi wa Kata ya Mecco, Wilaya ya Ilemela, Jijini Mwanza, katika ziara ya kikazi ya kukagua na kutatua changamoto za huduma ya maji safi. Picha na PraiseGod Mgumba

Kwa upande wake, Amir Mkalipa amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha maeneo yote yasiyo na miundombinu ya maji yanapatiwa huduma hiyo kwa wakati.

Baadhi ya wananchi wakizungumza katika mkutano huo wameeleza changamoto zinazoendelea, wakidai baadhi ya maeneo yamekosa miundombinu ya maji kwa muda mrefu bila majibu ya wazi kuhusu utekelezaji wa miradi iliyoahidiwa.

Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma endelevu na ya uhakika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *