Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imesema kuanzia Julai mosi, mwaka huu, daladala zote zinazotumia Barabara ya Kilwa hazitaruhusiwa kutoa huduma katika maeneo yanayohudumiwa na mradi wa mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi).

Kwa mujibu wa Latra, wananchi wanaotoka Mkuranga, Tuangoma na vitongoji vingine, daladala zitakuwa zikiishia Kituo cha Mwendokasi cha Mbagala Rangitatu, na abiria watatakiwa kuunganisha safari zao kwa kutumia mwendokasi kwenda katikati ya jiji na maeneo mengine.

Uamuzi huo wa Latra unakuja miezi mitatu tangu mtoa huduma wa mabasi hayo, Kampuni ya Mofat, ilalamikie kukosa faida ya uwekezaji wake, ikisisitiza kuwa uwepo wa daladala unafanya mabasi yake kutoa huduma chini ya uwezo wake.

Hata hivyo, uamuzi kama huo uliwahi kufanywa katika awamu ya kwanza ya mradi huo, unaohusisha njia ya Morogoro kuelekea Kariakoo, Posta na Morocco, lakini idadi ya abiria ilizidi uwezo wa mabasi ya mwendokasi yaliyokuwepo.

Kutokana na hali hiyo, abiria walikuwa wakirundikana vituoni, wakijazana ndani ya mabasi na hata kulazimika kutafuta njia mbadala za usafiri, ikiwemo bodaboda na bajaji.

Baadaye, Latra iliruhusu daladala 20 kuendelea kutoa huduma katika njia hiyo baada ya mabasi ya mwendokasi kuonekana kulemewa.

Taarifa ya kusitishwa kwa huduma za daladala katika njia hiyo ilitolewa leo, Jumatatu, Juni 15, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo.

Amesema wananchi wanaotoka maeneo ya Mkuranga, Tuangoma na vitongoji vingine watashuka katika Kituo cha Mbagala Rangitatu na kuunganisha safari zao kwa kutumia mabasi ya mwendokasi kwenda katikati ya jiji na maeneo mengine.

Tathmini iliyofanywa, amesema, imeonesha mabasi ya mwendokasi yanatumika kwa wastani wa asilimia 50 ya uwezo wake, hali inayotishia uwezo wa wawekezaji kurejesha mikopo waliyochukua kwa ajili ya mradi huo.

Amesema moja ya changamoto zilizobainika ni uwepo wa daladala zinazoendelea kutoa huduma katika maeneo yanayopitiwa na mabasi ya mwendokasi, jambo linalopunguza idadi ya abiria wanaotumia usafiri huo.

Kutokana na hali hiyo, amesema kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) na mamlaka nyingine za usafiri, wameagiza kufanyika tathmini ya haraka itakayowezesha baadhi ya daladala kuanza kutumia Kituo cha Mwendokasi cha Mbagala badala ya kituo cha sasa.

“Wawekezaji wakipata hasara, wengine watashindwa kuja kuwekeza katika sekta hii. Hivyo ni lazima tushirikiane kuhakikisha huduma hizi zinapata abiria wa kutosha na kuendelea kuwa endelevu,” amesema Suluo.

Amesema tayari maelekezo yametolewa kwa askari wa usalama barabarani kusimamia sheria kikamilifu, na daladala zitapaswa kushusha na kupakia abiria katika maeneo yaliyotengwa na si kusimama ovyo ndani ya eneo linalopitiwa na mradi wa mwendokasi.

Amesema Latra inaendelea kujadiliana na Dart kuhusu uwezekano wa kuunganisha mfumo wa tiketi kati ya daladala na mabasi ya mwendokasi ili kurahisisha safari za wananchi na kuongeza ufanisi wa huduma.

Pia, amesema mamlaka hiyo imefanya marekebisho ya ada za leseni yatakayoanza kutumika Julai mwaka huu, ambapo baadhi ya malipo yatamwezesha mtoa huduma kutumia miundombinu ya vituo bila kulazimika kulipa gharama za ziada kila anapoingia.

Mtendaji Mkuu wa Dart, Said Tunda, amesema maboresho yanayofanyika katika mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka yanalenga kulinda uwekezaji uliofanywa na sekta binafsi.

Amesema kwa sasa baadhi ya mabasi hayatumiki kwa kiwango kinachotarajiwa, hali inayosababisha changamoto kwa wawekezaji wanaopaswa kurejesha mikopo waliyochukua kwa ajili ya ununuzi wa mabasi hayo.

“Tunaye mwekezaji mzawa aliyewekeza fedha nyingi. Basi moja lina thamani ya takribani Sh900 milioni na yapo zaidi ya mabasi 200, lakini yanayofanya kazi kwa sasa ni machache. Hatuwezi kuona uwekezaji mkubwa kiasi hicho ukikosa tija,” amesema.

Amesema mpango wa kuunganisha huduma za daladala na mabasi ya mwendokasi haukusudii kuondoa ajira za mtu yeyote, bali kuleta mfumo wa kisasa wa usafiri utakaowanufaisha waendeshaji wa daladala, mabasi ya mwendokasi na wananchi kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Mofat, Mohammed Kassim, amesema kwa kiasi kikubwa mabasi yake hayajaanza kufanya kazi kwa uwezo uliokusudiwa kutokana na changamoto ya upatikanaji wa abiria.

Amesema kampuni ina mabasi takribani 200, lakini kwa sasa mabasi 50 pekee ndiyo yanayofanya kazi huku mengine 150 yakiwa yameegeshwa.

“Tumefanya uwekezaji mkubwa kwa kutumia mikopo ya benki. Leo hii mabasi mengi yamekaa bila kufanya kazi na hivyo ajira nyingi zimekosekana. Lengo letu si kulalamika, bali kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa wananchi huku tukinufaika sisi na wadau wengine wa sekta ya usafiri,” amesema.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Dart, Philimon Mzee, amesema Kituo cha Mbagala kimejengwa kwa uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya daladala, bajaji na bodaboda kwa wakati mmoja.

Amesema eneo hilo lina uwezo wa kupokea zaidi ya daladala 50 kwa wakati mmoja, pamoja na maeneo maalumu ya bajaji na bodaboda.

Pia, amesema kuna maeneo ya maegesho ya magari binafsi ambapo mtumiaji atalipa Sh1,500 kwa siku.

“Kituo hicho kimeundwa kwa mfumo unaowezesha vyombo hivyo vya usafiri kushusha na kupakia abiria kwa haraka bila kusababisha msongamano, na kimezingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya usafiri wa umma,” amesema Mzee.

Madereva na wananchi

Dereva wa daladala ya Mbagala Kisewe–Stesheni, Abdul Sultan, amesema amri ya Serikali haipingwi, lakini wasiwasi wao ni iwapo abiria wataelewa mabadiliko hayo.

“Madereva tunaweza kutekeleza amri iliyotolewa, lakini wasiwasi wetu ni kwa abiria. Mtu anapanda Stesheni akitaka kushuka Ufundi, leo tukimwambia hatushushi hadi Rangitatu, tunaweza kugombana naye na mwisho wa siku tukapelekana polisi,” amesema.

Mkazi wa Mbagala Kizuiani, Hadija Seif, amesema kuzuia daladala kupandisha na kushusha abiria wa maeneo ya katikati kunawaletea ugumu, kwani usafiri wa mwendokasi unahitaji matumizi ya kadi na tiketi za kielektroniki, jambo linalowapotezea muda.

“Kwa sasa hatuna muda wa kupoteza. Kupanda mwendokasi lazima uwe na kadi, hawataki pesa mkononi. Wakati mwingine mtu anasahau kadi, ndiyo maana tunapanda daladala ambayo haina masharti mengi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *